MAGUFULI NA KAMPENI ZA KUJIKOSOA, NAMFANANISHA NA MWALIMU NYERERE NA KAULI YA TUJISAHIHISHE
Kumekuwa
na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mgombea Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kupitia CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kuibua na
kuzungumzia mapungufu ya serikali ambayo yeye ni waziri. Baadhi ya watu
wanaofuatilia kampeni zake wameenda mbali zaidi na kuhisi kuwa kwa
kufanya hivyo, Magufuli anawafanyia kampeni labda bila yeye kujua
wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha Urais.
Bila
shaka, kwa watu wenye mtizamo huo, kampeni za Magufuli zingekuwa
zinatawaliwa na maneno yaliyoyajaa sifa nzuri za utendaji wa serikali na
chama tawala. Kwa hiyo, kwa mtizamo huo, ni jambo la kushangaza kuona
kuwa Magufuli anakosoa serikali aliyomo badala ya kuisifia na kuipamba
majukwani. Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanasema kuwa Magufuli
anazungumza kama vile anagombea kupitia vyama vya upinzani.
Maoni ya
namna hii pia yamekuwa yakielekezwa kwa katibu mkuu wa CCM, Ndg.
Abdulrahaman Kinana, ambaye katika shughuli zake za kisiasa za chama
chake katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesikika mara nyingi
akiikosoa serikali ya chama ambacho yeye ni katibu mkuu. Watanzania
watakumbuka kuwa Ndg. Kinana aliwahi kuwaita baadhi ya mawaziri wa
serikali hii 'mizigo' na kutaka wawajibishwe kwa kushindwa kutimiza
wajibu wao kwa ufanisi. Kwa baadhi ya watu Ndg. Kinana hakufanya vizuri
kuikosoa serikali yake hadharani na hasa kwa kuongea kama mpinzani.
Kitendo
cha Magufuli na viongozi wa chama chake kuibua mapungufu na kuikosoa
serikali yao hadharani inaonekana kama ni lugha ya wapinzani wa kisiasa.
Hakika utamaduni huo ni sawa na kujikosoa mwenyewe. Hata hivyo, ili
tuweze kuelewa kama kujikosoa ni jukumu pekee la vyama vya upinzani na
wagombea wao, inabidi tujiruhusu kuelimishwa na maneno ya hekima
aliyekuwa Rais na mpigania uhuru wa Guinea Bissau, kamarade, Amilcar
Cabral ambaye alishawahi kusema kuwa kwa kiongozi au anayetaka kuwa
kiongozi wa umma sharti awe na mwenendo wa kutoficha ukweli: Kwa maneno
yake;
"Hide
nothing from the masses of our people.Tell no lies.Expose lies whenever
they are told. Mask no difficulties, mistakes, failures. Claim no easy
victories."
Tafsiri
yake ni kuwa, kiongozi asifiche chochote kwa wananchi. asiseme uongo,
afichue uongo kila unapoibuka. Asifiche matatizo, makosa, mapungufu na
kushindwa. Asijipe sifa nyepesi nyepesi.” Kutokana na hekima ya Amilcar
Cabral ilivyoelezwa hapo juu, ni wazi kuwa anachofanya Magufuli ndicho
haswa kinachotakiwa kufanyika. Kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha
wazi kuwa anajua matatizo na mapungufu yaliyopo na badala ya kuyafunika
na kuyapaka rangi anayaweka wazi. Bahati nzuri Magufuli amekuwa
akielezea namna atakavyoshughulikia hayo matatizo na mapungufu. Bahati
nzuri tabia hii ya Magufuli siyo mpya. Watanzania watakumbuka kuwa hulka
hii ya Magufuli ilijionyesha wakati hata alipokuwa waziri chini ya Rais
Benjamin Mkapa alipoikosoa Ofisi yake hadharani kwa baadhi ya watumishi
wa ofisi hiyo kujimilikishia magari ya umma isivyo halali. Katika
kipindi hiki cha kampeni, Magufuli amekuwa akitoa mapungufu ya serikali
hata pale ambapo Rais Kikwete yupo.
Sambamba
na Amilcar Cabral, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi
kuandika kitabu mwaka 1962 kiitwacho "Tujisahihishe" akitaka Watanzania
na hasa viongozi wawe tayari muda wote kujisahihisha. Katika kitabu
hicho Baba wa Taifa, alisema kuwa “makosa ni makosa bila kujali ni nani
ameyafanya. Muhimu ni kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Katika
kitabu hicho, Mwalimu Nyerere aliendelea kusema;
“Kujielimisha
ni kujua ukweli wa mambo na kuwa na ujuzi wa sababu mbalimbali za
mambo; na kama mambo hayo ni mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama
ni mema, jinsi ya kuyadumisha. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu
zisizo za kweli na kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu
za matatizo na jinsi ya kuyaondoa(Nyerere, 1962, 5).”
Kwa
maelezo hayo ya Baba wa Taifa, ni wazi kuwa Magufuli ameamua kuwa mkweli
katika kampeni zake na ameepuka kuwa mpumbavu kama alivyobainisha Baba
wa Taifa.
Kujikosoa
anakofanya Magufuli kunadhihirisha aina ya Rais tunayemhitaji. Itakuwa
ni hatari kubwa kuwa na Rais asiyetayari kujikosoa au kukosolewa. Ni
janga kubwa kwa nchi kuwa na Rais ambaye anaamini kuwa yeye ni mtakatifu
asiyekosea. Rais wa namna hiyo ni lazima atakuwa ni dikteta na
watakodhubutu kumkosoa na kuibua makosa yake watakiona cha moto. Kama
historia za nchi mbalimbali inavyoonyesha, hili likitokea, Tanzania
itakuwa katika dhahama kubwa.
Maandiko
ya vitabu vitakatifu yanatuelekeza kuwa ukamilifu wa binadamu huja kwa
kusimama katika ukweli, kujikosoa na kukubali kukosolewa na kuepuka
hadaa. Vivyo hivyo, ukamilifu na uhai wa taasisi zinazoundwa na binadamu
kama vile vyama vya siasa na serikali lazima viwe na uthubutu wa
kujikosoa na kukubali kukosolewa kama anavyofanya Magufuli.
Kwa
maelezo hayo hapo juu, ni ni wazi kuwa ukosoaji siyo jukumu pekee la
vyama vya upinzani bali ni jukumu la kila mmoja hasa wale wanaotaka kuwa
viongozi wetu. Hivyo, badala ya kumshangaa Magufuli kwa kubainisha
makosa na mapungufu ya serikali ambayo yeye ni sehemu yake, tujielekeze
katika kuwataka wagombea wengine katika nafasi mbalimbali waepuke hadaa
na badala yake wafanye kampeni zao kwa kueleza ukweli.
Hadaa
katika kampeni zitatupatia viongozi matapeli ambao bila shaka uongozi
wao utakuwa wa hadaa kwa wananchi. Kinyume chake kiongozi mkweli na
aliye na uthubutu wa kujikosoa anaonyesha kuwa ana uwezo wa kutafuta
suluhisho la kweli la matatizo yaliyopo.
Kwa
kuitimisha, Magufuli hajachemka katika kuikosoa serikali aliyomo bali,
kwa kufanya hivyo, anaonyesha ufahamu wake wa hali halisi ilivyo. Zaidi,
anaonyesha kuwa yeye ni mtu aliyetayari kusimamia ukweli jinsi ulivyo
na hivyo ndivyo inapaswa kuwa.
Humphrey Polepole
@Twitter
No comments:
Post a Comment