Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele. (Picha na Maktaba).
Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewataka wadau wote wanaojihusisha na
usafirishaji na uuzaji wa kemikali kujisajili kabla ya hatua za kisheria
hazijachukuliwa dhidi yao.
Kauli
hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali
Prof. Samwel Manyele wakati wa warsha ya siku moja iliyolenga
kuwaelimisha wadau wa uuzaji na usafirishaji kuhusiana na usimamizi wa
kemikali hatari na zenye madhara kwa afya na mazingira kwenye maeneo ya
bandari na wakati wa usafirishaji.
Amefafanua
kuwa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na
Majumbani Na. 3 ya mwaka 2003 inawataka wadau kusajiliwa ili kuhakikisha
kuwa kemikali zinatumika katika hali iliyosalama wakati wa
kusafirishwa,kuuzwa na kuhifadhi.
“Katika
kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa
Kemikali za Viwandani na Majumbani, Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali umekuwa ukifanya jitihada kadhaa kuhakikisha wadau wote
wanauelewa wa kutosha kuhusiana na maswala ya sheria” alisisitiza Prof.
Manyele.
Alisema
kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu
kwa wadau kupitia warsha, mikutano, ukaguzi, kushiriki kwenye maonyesho,
mafunzo kwa wasimamizi wa shughuli zinazohusiana na masuala ya kemikali
na madereva wanaosafirisha kemikali ili kuhakikisha kuwa wadau na
wananchi wanatumia kemikali katika hali iliyosalama kwao na mazingira.
Mbali
na hayo warsha hiyo imewakutanisha wadau muhimu wa Bandari kwa lengo la
kupeana elimu na kujadili juu ya namna bora ya kusimamia upakiaji,
upakuaji, na uhifadhi wa shughuli yeyote inayohusu kemikali hatari
katika maeneo ya Bandari.
Aidha
Mkemia Mkuu huyo wa Serikali alisema kuwa Ofisi hiyo inaanda warsha
nyingine ya kuelimisha wadau juu ya kuchukua taadhari juu ya kujikinga
na tukio ambalo linaweza kutokea kutokana na mlipuko wa kemikali kama
ilivyokea nchini China.
No comments:
Post a Comment