CHAMA cha Wananchi (CUF) kimepasuka wilayani Mafia, mkoani Pwani, baada ya aliyeidhinishwa kugombea ubunge Mafia, Mohammed Albadawi, kuhama chama hicho na kujiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Albadawi
pamoja na kuidhinishwa na CUF kuwa mgombea wake katika jimbo hilo, siku
chache baadaye alikatwa na nafasi yake hiyo kupewa aliyekuwa mgombea wa
jimbo hilo kwa tiketi ya CCM lakini alishindwa kwenye kura za maoni,
Omary Kimbau.
Akizungumza
katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia
Suluhu Hassan, kada huyo wa zamani wa CUF alisema chama hicho
kimemdhalilisha na kumshusha thamani kwa kumuondoa na kumuweka mwingine
aliyeshindwa alikotoka.
“Mimi
nilikuwa kada wa CUF, hii ni mara ya kwanza kuhutubia mkutano wa CCM,
nimefanya kazi kubwa ya kukinadi CUF lakini kwa sasa sina hamu kabisa na
chama hicho,” alisema.
Alisema
alikuwa ni mmoja wa wanachama wa CUF waliochukua fomu za kuwania ubunge
ambapo Kimbau aliyepewa nafasi hiyo ya kugombea ubunge, kwa upande wake
alichukua fomu kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Alisema
katika mchakato wa ndani wa chama chake, alipitishwa na Baraza Kuu la
CUF ikiwa ni pamoja na kupigiwa simu na Katibu Mkuu wa chama hicho
Maalim Seif Sharif Hamad, akimtaarifu kuwa amepita.
Alisema
wakati mchakato wa kura za maoni ukiendelea CUF, kwa upande wa CCM,
Kimbau alipigwa chini baada ya kupata nafasi ya pili na kukimbilia CUF
ambako walimpatia nafasi hiyo ya kuwania ubunge Mafia na kumkata
Albadawi.
“Nilishinda
kabisa kura za maoni nilipata kura 99 mwenzangu alipata kura nne,
lakini kutokana na mchezo wa biashara, Kimbau akafanya anavyofanya mimi
nikatolewa,” alisisitiza.
“Nawaambia
leo walichokifanya ni upumbavu, na nachukua fursa hii kuwaambia ndugu
zangu hapa hakuna CUF tena, kura zote za ubunge, urais na udiwani ipeni
CCM kwa sababu kiongozi yeyote aliyepata nafasi kwa dhuluma hawezi
kuwatumikia wananchi."
No comments:
Post a Comment