Membe awaonya waangalizi wa uchaguzi kutotoa matamko kabla ya NEC - LEKULE

Breaking

11 Sept 2015

Membe awaonya waangalizi wa uchaguzi kutotoa matamko kabla ya NEC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema waangalizi wa uchaguzi hawatakiwi kutoa tamko lolote linalohusu uchaguzi au kampeni kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza matokeo.

Akizungumza jana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, Membe alisema waangalizi hao wanaweza kutoa ripoti zao baada ya kuthibitishwa na wizara ya mambo ya nje, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) na Nec.

Membe alisema waangalizi wote watakuwa huru kufanya kazi zao na serikali itahakikisha kuwa wanakuwa salama muda wote watakapokuwa nchini. Amesema waangalizi wa uchaguzi hawataruhusiwa kufika baadhi ya maeneo ambayo yatabainishwa na Nec.

“Waangalizi watapewa fomu na Tume za uchaguzi ili kuwatambua kama waangalizi wa uchaguzi. Hawataruhusiwa kufanya kazi zao kwenye baadhi ya maeneo, kwa mfano maeneo ya kijeshi na mengine,” alisema waziri huyo

Amewataka waangalizi kutofungamana na upande wowote, badala yake wafanye kazi yao bila kuingilia mchakato wa uchaguzi wa Oktoba, 25. Amesisitiza umuhimu wa amani wakati wa uchaguzi na kuwataka waangalizi hao kutokuwa chanzo cha vurugu.


“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba amani na usalama vinakuwepo siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Vikosi vya usalama havitahusika na mchakato wa uchaguzi, kazi yao itakuwa ni kuhakikisha kuna amani na usalama,” alisema waziri huyo.

No comments: