Magufuli, Samwel Sitta Wamshambulia Lowassa - LEKULE

Breaking

27 Sept 2015

Magufuli, Samwel Sitta Wamshambulia Lowassa



Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga jana, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alimshukia Lowassa akisema mradi wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria ulianza miaka mingi na kusimamiwa na Serikali ya Tanzania na Uholanzi wakati huo Lowassa, ambaye alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo wakati wa utekelezaji wake, alikuwa bado mwanafunzi.

Sitta alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu mradi huo ndipo ulianza kusimamiwa na Serikali ya Tanzania chini ya mawaziri mbalimbali.

“Si Lowassa pekee aliyesimamia na kuanzisha mradi huu,” alisema Sitta. 
 
“Sasa mbona akisimama jukwaani anajitaja mwenyewe tu, mbona hawataji wenzake. Nawaambieni ndugu zangu viongozi wanaopenda kujikweza kama hawa waogopeni,” alisema Sitta na kushangiliwa.

Dk Magufuli naye alichangia hoja hiyo wakati akijinadi aliposema kuwa mradi huo, ambao umesaidia wakazi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kupata maji, ulianzishwa na kusimamiwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na si Lowassa.

Dk Magufuli, ambaye anajinadi kwa kutumia mafanikio ya ujenzi wa barabara, alisema Lowassa ni mmoja wa mawaziri waliosimamia mradi huo na si yeye aliyeubuni na kuuanzisha kama anavyojinadi katika mikutano yake ya kampeni.

Tangu kuanza kwa kampeni, Lowassa amewaahidi wananchi wa Kigoma, Bariadi na Chato kuwa akiwa, rais atahakikisha wanapata maji kutoka Ziwa Victoria, akieleza kuwa kama aliweza kufanikisha mradi wa maji kutoka ziwa hilo kwenda Shinyanga, hawezi kushindwa katika maeneo hayo.

Lowassa alipokuwa Shinyanga, pia aliwaahidi wananchi wa mkoa huo kuwa akiwa rais watapata maji kutoka ziwa hilo.

Akijinadi kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema amejenga barabara nyingi akiwa Waziri wa Ujenzi lakini hawezi kujisifu kuwa yeye ndiye aliyezijenga.

“Siwezi kujisifu kwa kujenga barabara zaidi ya kilomita 17,000 wakati nikiwa waziri wa ujenzi kwa miaka 15 katika Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne. Huwezi kuwa na mtoto ukamtuma shambani akachume pamba kisha azilete na kujisifu kuwa zile pamba ni zake,” alisema.

“Eti anasema alileta shule za kata. Hivi alibeba matofali kichwani wakati wa ujenzi wa shule hizi,” alihoji Dk Magufuli akimponda Lowassa ambaye pia, alisimamia ujenzi wa shule za kata wakati akiwa Waziri Mkuu.

Dk Magufuli alisema akiwa rais, atahakikisha kata zote zisizo na maji katika mji wa Shinyanga zinapata maji, huku akisisitiza kuwa maendeleo ni changamoto na kwamba haziwezi kuisha zote.

Waziri huyo wa Ujenzi aliahidi kujenga kilomita 10 za lami katika mji wa Shinyanga mbali na kimomita 32 zilizojengwa mpaka sasa, ujenzi wa soko la kisasa, chuo kikuu cha madini, kufuta ushuru kwa wakulima na kuanzisha viwanda kwa kuhusisha sekta binafsi.

“Shinyanga kuna kero ya kiwanda cha nyama ambacho kinasuasa mpaka kinatia kichefuchefu. Siku nikiapishwa kuwa rais, mwenye kiwanda hiki aidha kifanye kazi au kirejeshwe serikalini,” alisema na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.

Alisema ni aibu kwa Watanzania kuwa maskini katika nchi yenye kila aina ya rasilimali.