MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema Serikali atakayoiongoza itajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kuongeza ajira na mapato ya Serikali, huku akiwaahidi wakazi wa Morogoro kufufua viwanda vyao.
Amesema
hayo katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika moja ya mikutano
mikubwa ya kampeni za uchaguzi, uliorushwa moja kwa moja na televisheni
mbalimbali nchini.
Akizungumza
katika mkutano huo, Dk Magufuli alisema mbali na kujenga viwanda, pia
Serikali hiyo itatoa Sh milioni 50 kwa kila mtaa na kijiji kwa ajili ya
wanawake na vijana kukuza mitaji yao ya biashara na kuanzisha biashara
mpya, huku akiwahakikishia kutobughudhiwa.
Kuhusu
elimu na afya, Dk Magufuli alisema kuanzia mwakani wanafunzi kutoka
darasa la awali mpaka kidato cha nne, hawatalipa ada ya shule kwa kuwa
Serikali atakayoiongoza itatoa huduma hiyo bure. Pia, alisema atashusha
bei ya vifaa vya ujenzi ili wananchi wanaofanya kazi na biashara na
kujipatia kipato halali, wajenge nyumba kwa gharama nafuu.
Kabla
ya Dk Magufuli kuhutubia, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
alipanda jukwaani na kusema akistaafu kwa kumkabidhi nchi Dk Magufuli,
atalala usingizi.
Rais
Kikwete alisema hakwenda mkoani huko kuhudhuria mikutano ya Dk
Magufuli, bali alikwenda kuhudhuria kikao cha mkakati cha Umoja wa
Wanawake Tanzania (UWT), kilichofanyika mkoani humo.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, kwa kuwa mgombea huyo alikuwa na ratiba ya
kuhutubia mkutano katika uwanja huo, akaona ni vyema na yeye ahudhurie
mkutano huo.
Alipopewa
nafasi ya kumkaribisha mgombea huyo, Rais Kikwete alitumia fursa hiyo
kuzungumza kidogo kilichofanyika Dodoma, wakati wa mchakato wa kumpata
mgombea urais wa chama hicho.
Alisema
walitumia muda mrefu kujadili kila mgombea kati ya wagombea 38
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, mpaka wakapata wagombea watano
akiwemo Dk Magufuli, Balozi Amina Salum Ali, Dk Asha-Rose Migiro,
Bernard Membe na January Makamba.
Baada
ya hapo, alisema walikwenda katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM ambako wafuasi wa mmoja wa wagombea ambaye hakuingia katika
tano bora, Edward Lowassa, walipewa nafasi kubwa ya kuzungumza baada ya
mgombea huyo kutopenya tano bora.
Kwa
mujibu wa Kikwete, walizungumza yote na sababu ya kupata wagombea hao
na sifa zao dhidi ya za wenzao na wakaafikiana na kupiga kura, ambapo
Lowassa ambaye baadaye alitoka na kuhamia Chadema, alipiga kura.
Baada
ya hapo walipatikana watatu, Magufuli, Balozi Amina na Dk Migiro ambapo
katika Mkutano Mkuu, alipita Magufuli ambaye alisema ana kila sifa ya
kuwa rais na kuongeza kuwa wananchi walisema yeye Kikwete ni mpole,
hivyo baada ya kupata rais mpole, Tanzania inahitaji rais mkali.
Rais
Kikwete alisema kampeni zinavyokwenda, anaona baada ya Uchaguzi Mkuu
vyama vya upinzani vilivyojiunga katika mwavuli wa Ukawa, vitageuka jina
na kuwa Ukiwa.
No comments:
Post a Comment