LOWASSA: Ujinga, umasikini na maradhi vitakuwa historia kwenye serikali yangu - LEKULE

Breaking

2 Sept 2015

LOWASSA: Ujinga, umasikini na maradhi vitakuwa historia kwenye serikali yangu



Mgombea urais wa Chadema kwa mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amesema akiwa rais wa Awamu ya Tano atafuta maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini waliodumu tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Lembuka katika Kijiji cha Madaba mkoani Ruvuma, Lowassa aliyekuwa akitumia staili ya kuwauliza wananchi matatizo yanayowakibili na kisha kuwajibu atakavyoyatatua, alisema tangu nchi ipate uhuru maisha ya Watanzania ni duni na kuahidi kuwaondoa katika umasikini.

Wakati Lowassa akisema hayo, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliwataka wananchi kuipa Chadema na Ukawa miaka mitano tu ili iweze kuwaletea maedeleo na kama wakishindwa, warudi tena CCM.

“Jambo kubwa ni kupiga kura na kuzilinda na ikiwezekana akina mama mpike chakula kabisa nyumbani ili waume zenu wakifika nyumbani wajipakulie wenyewe. Tusipoitoa CCM madarakani hatutaweza kuwatoa tena na lazima wang’oke safari hii. Hata wana-CCM wenzangu nawashauri waondoke huko na kujiunga na sisi. Ondokeni huko nyumba inawaka moto,” alisema Lowassa.

Katika mkutano huo, wananchi walieleza kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa maji na umeme, migogoro ya ardhi, ada na michango iliyokithiri katika shule pamoja na ushuru katika mazao.

“Tutamaliza tatizo la umeme ndani ya mwaka mmoja, tutamaliza suala la kuporwa ardhi,” alisema Lowassa huku akiwahoji wananchi wa kijiji hicho kwanini wakubali kuporwa ardhi.

Wananchi hao walisema katika vituo vya afya wagonjwa wanaruhusiwa kurudi majumbani kutokana na vituo hivyo kukosa maji sambamba na kutozwa ushuru wa mazao usiokuwa na kichwa wala miguu.

Akizungumza katika mkutaano huo, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema maendeleo ya Tanzania hayafanani na rasilimali zilizopo nchini, akiwataka wananchi kuyakubali mabadiliko ili kuepuka matatizo mengine.

“Nilikuwa waziri mkuu kwa miaka 10 lakini nchi haikuwa na vita. Mkichagua upinzani kutakuwa na amani kama kawaida,” alisema Sumaye huku akitolea mfano yaliyotokea Masasi ambapo wananchi walichoma moto vituo vya polisi na Halmashauri baada ya bodaboda kugongana na gari la polisi.
  
 “Hali hiyo inatokana na wananchi kuchoka kuona viongozi waliowachagua wananeema na wao wanaendelea kuwa masikini.”

No comments: