MGOMBEA urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amesema hana muda wa kujibu matusi na kejeli zinazotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yake.
Badala yake amesema anatumia muda uliobaki wa kampeni kutafuta kura kwa wananchi kwa kunadi ilani ya chama chake.
Akizungumza
kwenye mikutano ya hadhara, Bunju na baadaye Mbezi mkoani Dar es
Salaam, Lowassa alisema kila alichoahidi ataanza kukifanyia kazi punde
tu baada ya kuapishwa:
“Nitajenga viwanda kukabiliana na ajira, ada za shule na mengine ndani ya siku hizo.
“Nikiingia
madarakani, hakuna mgeni atakayefanya biashara bila kuingia ubia na
wazawa. Lazima tuwajali vijana wetu kwa kuwajengea mazingira wezeshi,” alisema mgombea huyo aliyewasili Bunju saa 9.30 alasiri akitokea Tabora.
Ili kufanikisha hayo, aliwataka vijana kulinda kura zao siku ya uchaguzi ili zisiibwe.
Akizungumza
katika mkutano wake uliofanyika kwenye Uwanja cha Shule ya Msingi Bunju
‘A’, Lowassa alisema wananchi wana wasiwasi na NEC kwamba haitatenda
haki kwa sababu ya ukaribu wake na CCM.
Aliwataka
vijana kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kufanya kazi mbili,
kwanza kupiga kura na pili ni kulinda kura zao huku akisisitiza kwamba
ana uhakika kwamba hataibiwa kura ng’o.
Aliwataka
wananchi kufanya uamuzi mgumu kuiondoa CCM madarakani ili
wajihakikishie huduma bora za jamii katika serikali ya awamu ya tano.
Alisema
zimebaki siku 48 kwa wananchi kuamua hatima ya maisha yao yajayo
akiwataka kuwachagua wagombea wa Ukawa ili waondoe msongamano wa magari
jijini, kuboresha mfumo wa elimu kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza
ajira kwa wananchi.
Awali,
akimkaribisha Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema
ili kuepuka vurugu, lazima CCM wakubali kushindwa na kupisha serikali
mpya ya Ukawa.
Alisisitiza kuwa ameihama CCM baada ya kubaini kuwa mabadiliko hayawezi kupatikana ndani ya chama hicho.
Alimtaka
mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli kuzungumzia kashfa
mbalimbali zinazoikabili Serikali ya sasa ambazo ni pamoja na
usafirishwaji wa twiga, dawa za kulevya na pembe za ndovu.
“Ndani
ya CCM huwezi kufanya chochote, CCM ni shida,” alisema Sumaye na
kuongeza kuwa uchumi umeshuka tofauti na miaka 10 iliyopita.
Alisema
Ukawa ikiingia madarakani, itahakikisha fedha zote zilizofichwa nje ya
nchi zinarudishwa na wahusika wake kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “NEC watasababisha machafuko kwa
kuibeba CCM. Chama hicho kwa sasa hakibebeki, sasa wameanza kuwatumia
watu kumchafua Lowassa.”
Alisema
ziara ya kampeni za umoja huo katika mikoa saba, imeonyesha kwamba
wananchi wako tayari kwa mabadiliko na kuipokea serikali ya Ukawa.
Awali,
mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe (Chadema), Halima Mdee alimtaka Lowassa
kusaidia kutatua migogoro ya ardhi katika jimbo hilo hasa eneo la Boko.
Alisema uhakiki wa majina katika daftari la kudumu linaendeshwa kihuni kwa sababu wananchi wakienda kwenye vituo hawalioni.
Mgombea
huyo wa urais alihitimisha kampeni zake Bunju saa 10.30 jioni na
kuelekea Mbezi kwa ajili ya mkutano mwingine ambao ulimalizika saa 12.15
jioni.
Akiwa Mbezi
Baada
ya kuwasili Mbezi saa 11.15, Lowassa aliwaomba wakazi wa Jimbo la
Kibamba wamchague pamoja na mbunge na madiwani wa Ukawa ili waweze
kumsaidia kuleta mabadiliko yatakayoboresha maisha ya wananchi.
Alisema
kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi yake, lakini akasema ataendelea kufanya
kampeni za kistaarabu ili kuwaeleza wananchi nini anataka kukifanya.
“Wananikashifu kwa maneno mengi, eti wanashangaa mimi kupanda daladala sasa, lakini hawashangai twiga kupanda ndege,” alisema.
Awali, Sumaye alisema hawezi kujibizana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kwa sababu naye ataonekana amepungukiwa.
Sumaye
alisema Chadema ikishinda uchaguzi, kazi ya kwanza itakuwa kutaifisha
na kurudisha fedha zilizowekwa na vigogo wa serikali nje ya nchi.
“Kazi
ya kwanza itakuwa kurudisha fedha zilizoibwa na vigogo wa Serikali ya
CCM, tutazirudisha na kuziweka katika Hazina yetu,” alisema.
Sumaye
ambaye mara kwa mara alitumia kaulimbiu ya “CCM” na wananchi kumjibu ni
“shidaaa”, alisema tangu Lowassa ajiuzulu kashfa za ufisadi wa fedha za
Serikali umeongezeka.
Mbowe
ambaye pia Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, aliwataka wananchi hao
kuhakikisha wanatunza vitambulisho vya kupigia kura ili waweze kufanya
uamuzi sahihi Oktoba 25.
“Mlivyohamasika
mnaonyesha kwamba mmekubali mabadiliko, hivyo jambo la msingi ni
kutunza vitambulisho vyenu ili siku ya uchaguzi muweze kuwachagua
viongozi wa Ukawa,” alisema.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibamba (Chadema), John Mnyika aliomba kura kwa wagombea wote wa Ukawa ili waweze kuleta maendeleo.
“Umati huu unaonyesha kwamba wananchi mna imani na viongozi wanaogombea kupitia Ukawa, tunaomba mtuchague,” alisema.
Mgombea
Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia chama hicho, Saed Kubenea aliwaomba
wananchi wawachague viongozi wa Ukawa ili waende bungeni kuwatetea
wananchi
Ilivyokuwa
Wafuasi
wa Ukawa walianza kufika katika Uwanja wa Bunju A tangu saa nne asubuhi
wakiwa wamejipamba kwa mavazi ya sare za vyama vinavyounda umoja huo.
Baadhi
ya wafuasi hao wakiwa na bendera za vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi, muda wote walikuwa wakiimba na kucheza nyimbo za Chadema.
Wafuasi
hao walikuwa wakipuliza matarumbeta kwenye barabara inayopita jirani na
uwanja huo huku baadhi ya magari yaliyokuwa yakipita eneo hilo,
yakiunga mkono kwa kupuliza honi.
Madereva wengi kati ya hao, walikuwa wakinyanyua mikono juu na kuonyesha alama ya vidole viwili ambayo inatumiwa na Chadema.
Wafuasi
wa chama hicho walipouona msafara wa Lowassa ukiwasili katika viwanja
hivyo saa 9.30 alasiri walishangilia kwa sauti ya juu huku wakiimba
rais, rais, rais.
Baada
ya mkutano kumalizika kwenye viwanja hivyo na msafara wake kuanza
safari ya kuelekea Mbezi, saa 10.40 jioni, karibu kila eneo alikopita,
wananchi walionekana wakiwa wamejipanga kando ya barabara
wakimshangilia, wengi wao wakionyesha alama ya vidole viwili.
Mbali
ya kujipanga barabarani, katika baadhi ya maeneo, wananchi walipanda
juu ya miti ili wapate kuuangalia vyema msafara huo ulipitia Goba hadi
Mbezi.
Huko Mbezi, wananchi walikuwa wamefurika kwenye uwanja wa mkutano tangu saa nane mchana.
Sababu za kuchelewa
Akizungumzia
sababu ya kuchelewa kwa mikutano hiyo ambao wa Bunju ulipangwa kuanza
saa nne asubuhi na Mbezi saa tisa alasiri, Mbowe alisema hiyo
ilisababishwa na kuunganisha safari jana hiyohiyo kutoka Tabora kupitia
Dodoma.
“Tunawaomba radhi kwa kuchelewa kuanza kwa sababu ya safari ndefu,” alisema Mbowe.
Pamoja
na mkutano huo kumalizika dakika 15 zaidi ya muda uliowekwa na NEC,
Polisi waliokuwapo hawakuonekana kuchukua hatua yoyote.
No comments:
Post a Comment