Washiriki
wa Kongamano la Wasaidizi wa Kisheria Magerezani kutoka Magereza Mkoani
tanga wakiendelea na majadiliano katika Kongamano hilo linalofanyika
Mkoani Morogoro kwa siku tatu.
Na, Lucas Mboje, Morogoro
Jeshi la Magereza nchini limeahidi kuendelea kushirikiana na Asasi
ya Envirocare katika kuimarisha Madawati ya Msaada wa Kisheria
Magerezani ili kuleta tija katika utatuzi wa changamoto ya Msongamano wa
Mahabusu inayolikabili Jeshi hilo.
Kauli hiyo imetolewa jana Mkoani Morogoro na Kamishna Jenerali wa
Jeshi la Magereza, John Casmir Minja alipokuwa Mgeni rasmi wakati wa
hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Wasaidizi wa Kisheria Magerezani na
Mahabusi za Watoto.
Jenerali Minja amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukulia kwa
uzito stahiki suala la Msongamano wa Mahabusu Magerezani ikiwemo
kushirikiana na Wadau wa Haki Jinai katika kupunguza changamoto ya
Msongamano wa Mahabusu Magerezani.
"Napenda kutoa rai kwa Asasi zingine zenye malengo yanayofanana na
Asasi hii nazikaribisha kuja kufanya kazi na Jeshi la Magereza kwani
mwelekeo wa Jeshi kwa sasa ni Urekebishaji wa Wafungwa(From Prisons to
Corrections) ambapo Jeshi la Magereza watafanya kazi kwa karibu na Asasi
za Kiraia na Jamii kwa ujumla". Alisema Jenerali Minja.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare,
Bi. Loyce Lema amesema kuwa imekuwa ni faraja kwao kupata ushirikiano
kama huo kutoka Jeshi la Magereza kwani umewezesha kutekelezwa kwa mradi
huo wa kutoa Msaada wa Kisheria kwa Mahabusu waliopo Magerezani kwa
matokeo chanya kwa muda mufupi.
Bi. Lema alisema kuwa mradi huo umetekelezwa kwa miaka mitatu(2012
- 2015) na umetekelezwa kwenye Magereza 20 na Mahabusu 04 za Watoto
katika Mikoa 05 ambayo ni Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro
na Dar es Salaam.
Asasi ya Envirocare kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza ilifanya
utafiti wa awali wa kuangalia hali halisi ya Msongamano katika Magereza
yaliyopo katika Mikoa mitano ya mradi. Matokeo ya jumla ya utafiti huo
yalionesha kuwa kuna tatizo kubwa la Msongamano ambao unasababishwa na
idadi kubwa ya Mahabusu katika Magereza ya Mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment