Hoja Ya U-Imara Wa CCM Na Kama Uchaguzi Ungefanyika Jumapili Ijayo.. - LEKULE

Breaking

28 Sept 2015

Hoja Ya U-Imara Wa CCM Na Kama Uchaguzi Ungefanyika Jumapili Ijayo..


Ndugu zangu,
Nchi yetu inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu. Yamebaki majuma matatu hivi.
Kwenye Urais mchuano mkali ni kati ya mgombea wa UKAWA na wa CCM. Kwa mtazamo wangu, wengine ni wasindikizaji tu.
Nina bahati ya kutembea mijini na vijijini. Huko nazungumza na watu pia. Inanisaidia kuupima upepo wa kisiasa unavyovuma. Nina bahati pia ya kushuhudia chaguzi kuu nne tangu ule wa 1995. Nimesoma pia historia ya chaguzi za nchi hii hata kabla ya Uhuru wa Tanganyika. Ni pamoja na kampeni zake zilivyoendeshwa.
Kuna yaliyo tofauti kwa mwaka huu na nyakati hizo, lakini, kuna yenye kufanana pia. Kufahamu mwelekeo wa chaguzi Tanzania ni vema mtu akaiangazia electoral base ya nchi kwa maana ya ngome za wapiga kura. Kwenye siasa, kila chama na mgombea huwa na ngome ya wapiga kura wake.
Ili tuweze kujadili vema hili, ni vema tukubaliane kwanza kuwa asilimi 80 ya Watanzania, hivyo, wapiga kura, wanaishi vijijini.
Kwa mantiki hiyo, tuseme, kwa hesabu rahisi, kuwa robo tatu ya wapiga kura iko maeneo ya vijijini. Ina maana ya asilimia 75 ya wapiga kura. Robo iliyobakia kwa maana ya asilimia 25, iko maeneo ya mijini. Electoral base ya CCM iko vijijini, ni asilimia hiyo 75.
Sasa basi, ninavyofuatilia upepo wa kisiasa ikiwamo mazungumzo tu na makundi ya wapiga kura wa mijini na vijijini, ninachokiona, na ni mtazamo wangu binafsi, ni kuwa CCM katika kubanwa kwake sasa, na kama Uchaguzi ungefanyika Jumapili ijayo, inaweza kupoteza robo moja ya ngome yake ya kura za vijijini. Hivyo, ikabaki na robo mbili.
Ni kwa sababu, hata katika maeneo yale yanayosemwa kuwa CCM inakabiliwa na upinzani mkubwa, kama Mikoa ya Kusini Lindi na Mtwara, bado, kwenye maeneo ya vijijini kwenye mikoa hiyo, CCM inaonekana bado iko imara.
Kwa hali ilivyo sasa, CCM inaweza kupoteza robo ya kura za mijini, kwa maana ya asilimia 25 ya kura zote ambazo zinapigwa mijini kwenda UKAWA, lakini, bado CCM wana uwezo wa kupambana kuwapokonya UKAWA asilimia hata 15 za kura za mijini. Tafsiri hapa, UKAWA wasibwete na sapoti kubwa wanayoipata mijini kupitia mikusanyiko mikubwa kwenye mikutano yao, CCM wana uzoefu wa miaka mingi, wa kimbinu na kimikakati ya kuzitafuta kura hata kwenye mazingira ya kubanwa sana.
Hivyo, UKAWA kama Uchaguzi ungefanyika Jumapili ijayo, na kwa upepo ninaouona sasa, wanaweza kuzipokonya asilimia 25 kwa maana ya robo ya kura za CCM kwenye ngome yake ya kura za vijijini. Na UKAWA wakiweza kupambana kuhakikisha wanapata robo nzima ya kura za kwenye ngome yao ya kura za mijini, hapo UKAWA watakuwa wamefikisha asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa. Bado hawatakuwa na nafasi ya kuunda Serikali bila mazungumzo na CCM hata kama UKAWA wakipata asilimia 51.
Lakini, wapanga mikakati wa CCM, bila shaka nao hawalali katika kuhakikisha wanapata walau asilimia 15 ya kura za mijini.
Hivyo, kama CCM nao wataifanya kazi hiyo kwa bidii, kazi ya kuzisaka asilimia 15 ya kura za mijini, na kama Uchaguzi ungefanyika Jumapili ijayo, basi, naamini, kuwa CCM ndio watakaounda Serikali huku wakipoteza baadhi ya majimbo muhimu hususan maeneo ya mijini.
Nini kinakosekana kwa sasa?
Kinachokosekana kwa sasa ni misingi ya kiitikadi katika kuendesha kampeni za kisiasa. Vyama vimejikita katika kutoa ahadi. Lakini, katika siasa, lililo kubwa ni itikadi. Kama chama kinafuata itikadi ya kibepari, basi, kuahidi kutoa elimu na afya bure kunakinzana na misingi ya itikadi husika. Katika ubepari hakuna cha bure. Vyama lazima vijipambanue kiitikadi.
Katika itikadi ya kijamaa, huduma za kijamii kama vile elimu na afya ni kawaida kutolewa bure au kwa gharama nafuu sana. Fedha za kugharamia huduma hizo hutokana na kodi inayokusanywa kutokana na shughuli za uzalishaji. Wajamaa wanaamini katika kuwatoza kodi zaidi wenye nacho ili kuwamegea wasio nacho. Ndio mantiki hapa, kwamba anayetaka Urais ni vema akawaonyesha wazi wapiga kura, kwamba Serikali yake itafuata misingi gani ya kiitikadi katika kuendesha uchumi wa nchi.
Hapa kwetu vyama na wagombea wameshindwa kujipambanua katika itikadi. Mgombea anayetokea kwenye chama chenye sera za kibepari anasikika kama anatoka kwenye chama cha kijamaa na kinyume chake. Wakati mwingine unaingiwa mashaka, kama kweli vyama vina itikadi zenye kueleweka. Inatokea pia, kuwa itikadi ya mgombea, mara nyingi haionekani wazi anapoongea.
Duniani hapa Chama cha kisiasa chenye nguvu kinatokana na kazi ya timu iliyoandaliwa vema. Si kazi ya mtu mmoja. Kielelezo cha nguvu na umakini wa chama cha kisiasa ni uwingi na ubora wa makada wake. Chama ni makada kwa vile chama ni itikadi, malengo na shabaha na wala si nasaba na umaarufu wa mtu mmoja mmoja ndani ya chama.
Chama chenye makada wengi wenye kuielewa itikadi, malengo na shabaha ya chama, huwa hakimtegemei mtu mmoja katika kuwepo kwake. Hakimtegemei mtu mmoja katika kufanikisha ushindi wa chama. Hakimtegemei mtu mmoja katika kuhamasisha wanachama au umma.
Katika kampeni tunazokwenda nazo tunaona, kuwa baadhi ya vyama havina kabisa hazina ya makada. Kazi ya kuwahamasisha wapiga kura inapaswa kufanywa kwa kuanzia ngazi za chini kabisa, na huko chama kinahitaji makada wa kuifanya kazi hiyo. Hata kama uchaguzi huu utapita, vyama vijizatiti kuifanya kazi hiyo ili kujiandaa kwa chaguzi zijazo.
Na hatari ya kukosekana itikadi za vyama zenye kueleweka, ni uwezekano wa kama tunavyoona sasa. Hali ya kujipenyeza kwa nguvu hasi zenye kutaka kuisukuma jamii kuelekea kwenye machafuko.
Ni bahati mbaya sana siku hizi; unaposema au kuchambua mambo kama nifanyavyo sasa, haraka kuna wanaokimbilia kutafuta kabati la kukupachika; CCM, UKAWA, Dini, Kabila na mengineyo.
Tumelisahau kabati muhimu sana, nalo ni kabati la Tanzania. Na hakika, katika kila tuyafanyayo, tutangulize kwanza maslahi ya nchi yetu.