MGOMBEA ubunge anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) jimbo la Bunda mjini, mkoani Mara, Esther Bulaya anajivuna kuwa amefanikiwa kumdhibiti mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi mkuu, Stephen Wassira.
Akizungumza
na MwanahalisiOnline, Bulaya ambaye alikuwa mbunge wa Viti Maalum
akitokea Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), amesema kwamba amedhoofisha
ngome ya Wassira, ambaye amekuwa kiongozi serikalini tangu awamu ya
kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere.
“Kulikuwa
na matukio ya mikutano yetu kuvamiwa, wafuasi wetu kuvamiwa na
kubambikiziwa kesi, hata hivyo tulijipanga na kudhibiti huku
tukishirikiana na Jeshi la Polisi,” anasema akizungumzia mikakati iliyopangwa kumkwamisha kukubalika kwa wananchi.
“Ninavyoongea
na wewe gari yangu ipo Polisi kwa madai kuwa imehusika na uhalifu wa
kutumia silaha, dereva wangu pia anashikiliwa lakini wananchi kwa hasira
wamenipatia gari sita za kampeni,” anasema Bulaya aliyejiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kuhama CCM mara tu bunge lilipovunjwa.
Bulaya
ambaye pia kitaaluma ni mwandishi wa habari, amesema mpaka jana
ameshafanya kampeni katika Kata 14 za jimbo hilo huku akipita kila
kijiji na kila kitongoji na sasa anatarajia kuanza awamu ya pili ya
kampeni akiwa ameimarika zaidi.
Kuhusu upinzani anaokumbana nao kutoka kwa Wassira, Bulaya anasema “pamoja na mbinu chafu dhidi yangu nipo imara sana, ninamkabili kisawasawa na anakosa watu kwenye mikutano mingi.”
Jimbo
la Bunda mjini ni moja ya majimbo yenye upinzani mkali likishikiliwa na
Wassira ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), aliyewahi
kuwa NCCR-Mageuzi na kushinda ubunge kabla ya kuvuliwa na Mahakama Kuu
kwa kosa la kununua kura. Alikuwa ameshindana na Joseph Warioba wa CCM.