Geoffrey Mwashiuya
Waswahili
husema, mwenye fedha siyo mwenzio! Hiki ndicho kinachoonekana kufanywa
na klabu ya soka ya Yanga ambayo imetumia jeuri ya fedha msimu huu
kuivurugia Simba kwenye usajili unaoendelea.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa wametumia Sh90 milioni kuvuruga usajili wa watani zao wa jadi, Simba.
Kiasi
hicho cha fedha kimetumiwa na Yanga kuwanasa wachezaji wanne waliokuwa
kwenye mipango ya kusajiliwa na Simba msimu huu, lakini wakashindwa
kutua Msimbazi kwa sababu ya dau.
Wachezaji hao ambao Yanga imewapokonya mdomoni mwa Simb ni Malimi Busungu, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke na Mateo Simon.
Dau la
usajili wa wachezaji hao na timu walizotokea kwenye mabano ni Busung,
Sh25 milioni (Mgambo JKT), Kaseke, Sh35 milioni (Mbeya City), Mateo,
Sh20 milioni (KMKM Zanzibar) na Sh10 milioni za usajili wa Mwashiuya
kutoka Kimondo FC ya Ligi Daraja la Kwanza.(P.T)
Mshambuliaji
Busungu aliliambia gazeti hili kuwa alishindwa kujiunga na Simba baada
ya Yanga kumpa kiasi cha fedha alichokuwa anakihitaji bila kusitasita na
ingawa Simba walizungumza naye wakafikiana.
“Simba
nilizungumza nao, tukaelewena, lakini niliwatajia kiasi ninachokihitaji
ili nisaini kwao wakawa wanajishauri. Mimi ni mchezaji, nategemea soka
kuendesha maisha yangu. Yanga walitoka nyuma wakaja na ofa nzuri ambayo
nisingeweza kuikataa,” alisema Busungu.
Mshambuliaji
Simon aliyekuwa KMKM baada ya kung’ara kwenye mashindano ya Kombe la
Kagame yaliyomalizika mwezi huu alinukuliwa wiki iliyopita akisema kuwa
kabla ya kusajiliwa Yanga kwa dau la Sh20 milioni, Simba walitaka
kumsanisha kwa Sh7 milioni.
Mshambuliaji
huyo aliyeng’ara na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo kwenye mashindano
ya Kombe la Kagame, alikuwa na nafasi kubwa ya kusajiliwa na Simba
ambayo iliweka kambi Zanzibar, lakini Yanga ilimpandia dau mara tatu na
kufanikiwa kumnasa.
Hata
hivyo, Simba ilikanusha mara kwa mara kuwa ilikuwa inawahitaji wachezaji
hao na kueleza kuwa wanalenga kutafuta umaarufu kupitia klabu hiyo.
Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara alisema klabu yao
haijawahi kufanya mazungumzo na wachezaji hao na wala hawakuwa kwenye
mipango yao.
“Hii ni
tabia iliyoanza kuota mizizi kwa wachezaji wanaosajiliwa Yanga. Kila
mchezaji anaposajiliwa huko anakuambia kuwa Simba walinitaka, lakini
tulishindana dau,” alisema Manara.
Hata
hivyo, hiyo siyo mara ya kwanza kwa Yanga kuipoka Simba mchezaji katika
kipindi cha usajili kwani ilifanya hivyo kwa Mbuyu Twite, Kelvin Yondani
na hata Mganda Emmanuel Okwi.
No comments:
Post a Comment