Wasomi Wampuuza Profesa Lipumba.......Wasema Amekurupuka - LEKULE

Breaking

7 Aug 2015

Wasomi Wampuuza Profesa Lipumba.......Wasema Amekurupuka


Wasomi mbalimbali nchini, wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake wa Mwenyekiti wa CUF Taifa wengine wakisema suala hilo si jipya bali ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa nchini.
 
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti, wasomi hao pia walimshangaa Prof. Lipumba kwa uamuzi huo kwani alishiriki tangu mwanzo katika kumpokea mgombea urais aliyepitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Bw. Edward Lowassa, tangu alipohama CCM na kujiunga na CHADEMA.
 
Dkt. Lazaro Swai wa OUT
Akizungumzia uamuzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Jamii katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dkt. Lazaro Swai, alisema anamshangaa Prof. Lipumba kwa uamuzi aliouchukua.
 
"Hizo ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa tangu vilipoanzishwa,  hilo ni shinikizo kutoka upande mmoja lakini si kutoka UKAWA wala CUF," alisema Dkt. Swai.
 
Aliongeza kuwa, hivi sasa katika vyama vya siasa kila mtu ana mvuto wa aina yake lakini kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kutakuwa na mtikisiko kwa UKAWA na CCM kutokana na kuhama kwa Bw. Lowassa.
 
"Ujio wa Lowassa hauwezi kuipasua UKAWA, kujiuzulu kwa Lipumba kuna kitu ndani yake na kuleta mashaka kwa Watanzania, kwanini iwe sasa ndipo ajiondoe katika nafasi hiyo wakati alishiriki tangu mwanzo kumpokea Lowassa," alihoji.
 
Askofu Bagonza
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Karagwe, mkoani Kagera, Benson Bagonza, alisema kujiuzulu kwa Lipumba kunaashiria kuna jambo nyuma ya pazia, kwani wananchi hawataelewa.
 
"Tangu mwanzo alikuwa msingi imara kwenye UKAWA, ghafla anajiuzulu hiyo inashangaza watu wengi na sitaki kuamini kama amefikia uamuzi huo," alisema na kuongeza;
 
"Kutakuwa kuna jambo jingine limetokea nje ya UKAWA lakini swali la kujiuliza, kwanini alichelewa kuchukua uamuzi huo...huyo si Lipumba tunayemjua," alisema.
 
Dkt. Benson Bana
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa ya Jamii, Dkt. Benson Bana, alisema kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kulitarajiwa kutokana na mvutano uliokuwepo tangu awali.
 
"Ameona ni wakati mwafaka kuachia ngazi pia ni haki yake ya msingi kwani ndani ya muungano wa UKAWA, hauwezi kumpokea mtu wakati  huo huo akawa maarufu kushinda chama.
 
"Hilo ni pengo la kudumu ambalo haliwezi kuzibika kwa siku moja, uamuzi wa Lipumba na Slaa utakuwa wa halali kwani waliwekeza sana kwenye vyama vyao," alisema na kuongeza kuwa, kiongozi yeyote anapimwa kwa uadilifu na walikuwa tayari kujitoa kafara katika nyadhifa zao.
 
Julius Mtatiro
Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Bw. Julius Mtatiro, alisema hilo ni pigo kubwa kwa CUF na UKAWA hasa kipindi hiki cha kutafuta ushindi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa ujumbe wake alioutuma kwenye akaunti yake ya Facebook, Bw. Mtatiro alisema uamuzi huo ni mgumu kwani hajawahi kuusikia tangu awe mwanachama wa CUF miaka nane iliyopita.
 
Alisema kidemokrasia lazima kukubali matokeo na uamuzi binafsi wa mtu yeyote kwani mwisho wa siku, mtu hufanya uamuzi wake na tunalazimika kuyaheshimu ili maisha yaendelee.
 

 Aliongeza kuwa, si vizuri kumshutumu Prof. Lipumba kwenye mitandao na kwingineko bali akumbukwe kwa mchango wake mkubwa kisiasa ambapo jemedari anapoanguka vitani bunduki yake huchukuliwa na vita kuendelea. 

No comments: