Hali
ya hewa ndani ya Chama cha ACT- Wazalendo ambacho kinaongozwa na Zitto
Kabwe, imechafuka, baada ya Kamati Kuu kumpitisha na kumchukulia fomu ya
urais, Prof. Kitila Mkumbo, huku mwenyewe akisita kulipokea jukumu
hilo.
Kufuatia
hatua hiyo, Prof. Kitila ameandika katika mtandao wa kijamii kuwa
hajaandaliwa kisaikolojia kupeperusha bendera ya chama hicho katika
nafasi ya urais na jukumu hilo wapewe viongozi wengine waandamizi.
Tofauti
na ilivyozoeleka kwa wagombea kwenda na wafuasi wao Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) kuchukua fomu za kugombea urais, kwa upande wa ACT –
Wazalendo, Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, jana alikwenda Nec kumchukulia
fomu Prof. Kitila ambaye inadaiwa viongozi wakuu wa chama hicho
wamekutana naye kwa mazungumzo ya kumshawishi akubali kupeperusha
bendera ya chama hicho kuelekea Ikulu.
Mapema
asubuhi jana Prof. Kitila alifika ofisi za chama hicho Kijitonyama na
kuondoka na majira ya saa 5:00 asubuhi wafuasi zaidi ya 100 wakiwa na
mabango yenye ujumbe mbalimbali walivamia ofisi hiyo na kumbana Mwigamba
kuwaeleza kwanini chama hicho kinachelewa kuweka wazi mchakato wa
mgombea wake wa urais.
Habari
zinasema kuwa licha ya Prof. Kitila kutokuwapo kwenye kikao cha Kamati
Kuu (CC) kilichopitisha uamuzi wa kumtaka apeperushe bendera ya chama
hicho katika nafasi ya urais, lakini ulipitishwa uamuzi wa kwamba abebe
jukumu hilo zito.
Wakati
Kamati Kuu ikiamua hivyo, hadi jana alasiri hapakuwapo na makubaliano
na Prof. Kitila, lakini viongozi wakuu wa chama walikuwa kwenye
mazungumzo naye.
Akizungumza
na mtandao huu jana, Mwigamba alisema alichukua fomu hiyo saa 4:00
asubuhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu iliyokutana Agosti
15, mwaka huu.
Alisema
pamoja na azimio hilo, Kamati Kuu ilipitisha majina ya wagombea ubunge
nchi nzima, wagombea udiwani na kupokea ripoti ya wataalamu washauri juu
ya ushiriki katika harakati za uchaguzi wa rais.
“Baada
ya kupokea taarifa na mapendekezo yao tukajiridhisha kwa mustakabali wa
taifa, chama kinahitaji kusimamisha mgombea urais, ndipo nilipoagizwa
kwenda kuchukua kwa sababu muda unaenda zianze kujazwa ili Ijumaa ambayo
ndiyo siku ya mwisho zirudishwe,” alisema Mwigamba.
Alisema
Kamati Kuu imeamua hivyo kwa kuwa Prof. Kitila ni mwadilifu, mzalendo
wa kweli, anaweka mbele maslahi ya Taifa na kwamba ana sifa zote za
kuliongoza taifa na mgombea mwenza atakuwa ni Mwandishi wa habari
mkongwe, Hawra Shamte.
Hata
hivyo, Hawra, alipoulizwa kuhusu maamuzi hayo ya Kamati Kuu, alisema
hana taarifa zozote na kwamba hadi jana jioni hakuarifiwa chochote.
Alisema
wakati mgombea huyo anakutana na viongozi wakuu wa chama hicho, fomu
hiyo itaendelea kusambazwa mikoani ili kusaka wadhamini na kwamba
walianza kufanya hivyo jana.
“Tofauti
yetu na wengine hatutakuwa na ziara kwenye kusaka wadhamini, nimeenda
na wanachama wengine watatu kuchukua fomu na sikuwa na msururu wa watu
na hivyo hivyo kwenye kusaka wadhamini itakuwa kimya kimya,” alisema Mwigamba.
Alipoulizwa juu ya utayari wa Prof. Kitila kupeperusha bendera hiyo, alisema: “Hatuna wasiwasi, tunaamini atakubali uamuzi wa Kamati Kuu, anajua ni wajibu kubeba jukumu chama kinapomuhitaji.”
Aidha,
Mwigamba alisema kama itashindikana kwa Prof. Kitila, ni lazima chama
hicho kisimamishe mgombea mwingine katika nafasi hiyo.
Kitila: Sina Maandalizi
Katika
kundi la mtandao wa kijamii la chama hicho la Whatsaap, lijulikanalo
kama ACT Taasisi Imara, Prof. Kitila aliandika taarifa ya kuwashukuru
wanachama na viongozi kwa imani yao kwake, lakini alisema hawezi kubeba
jukumu hilo.
“Naomba
niwashukuru nyote kwa imani kubwa mliyonayo juu yangu katika
kukiwakilisha chama katika nafasi ya urais, naishukuru Kamati Kuu kwa
imani yake kwangu hata kufikia hatua ya kupitisha azimio la kuniomba
kugombea urais kwa chama chetu. Jana CC (Kamati Kuu) ilituma ujumbe
maalum nyumbani kwangu kwa ajili ya kuzungumza na familia na jamaa zangu
juu ya ombi hilo,” alisema katika andiko hilo na kuongeza:
“Nimekuwa
nikitafakari tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari uwezekano wa
mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea kushindikana.
Nimefanya mawasiliano mapana ndani ya familia, chama, chuoni
ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali
ninazohusiana nazo.”
Alisema
baada ya tafakari na mawasiliano mapana (consultations), ameona hana
utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na kisiasa
kumuwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Najua
nimewaangusha sana katika uamuzi wangu huu, lakini naamini kwamba
mtaheshimu uamuzi wangu na kwamba hamtaacha kuthamini mchango wangu
katika chama kwa sababu ya kukataa kugombea urais,” alisema na kuongeza:
“Nasikitika
kwa tuhuma ambazo baadhi ya wanachama wetu wanarusha katika mitandao ya
kijamii na sehemu nyingine. Nathamini na kuheshimu haki ya wanachama
kuonyesha hasira kwa jambo wasilolipenda…nawasihi wanachama wajizuie
kuzusha mambo yatakayochochea chuki ndani ya chama na kukatishana
tamaa.”
Aidha,
alishauri wanachama wengine waandamizi waombwe wachukue jukumu hilo na
kuwataja kuwa ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo na Katibu Mkuu, Mwigamba
na kwamba wakati hayo yakitafakariwa wasisahau malengo mapana ya chama
waliyojiwekea katika uchaguzi huo.
Alisema mafanikio waliyofikia ni kuweka wagombea ubunge na udiwani kata na majimbo mengi nchini.
Mwigamba alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, alijibu: “Sina simu ya whatsaap ila naenda kwenye kikao hadi leo (kesho) nitawapa taarifa.”
Wafuasi wakusanyika
Baadhi
ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanachama na wafuasi wa
ACT-Wazalendo yalikuwa na ujumbe wa ‘wamenunuliwa’ na mgombea wa
Chadema, Edward Lowassa ili wasisimamishe mgombea urais.
Wafuasi hao walikaa kwa saa nne nje ya ofisi hizo wakiimba nyimbo mbalimbali.
Mabango mengine yalisomeka: “Viongozi
hatuwaelewi mmekaa muda mrefu bila kutuambia mgombea urais ni nani
wakati muda unaisha, kama hamsimamishi mgombea ni bora mfunge ofisi,
tusijihusishe tena na siasa, liko wapi azimio la Tabora?”
No comments:
Post a Comment