Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo jijini Dar es salaam, Afisa Mwandamizi wa Taasisi hiyo anayeshughulikia Sera na maendeleo ya kilimo Bw. Stanley Wood amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali Barani Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizopewa kipaumbele na kunufaika na taasisi hiyo.
Amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kufanikisha ukusanyaji na usambazaji wa takwimu mbalimbali ambazo zimekuwa na matokeo chanya, taasisi hiyo inaangalia uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa takwimu bora za kilimo.
" Juhudi kubwa imefanywa na Tanzania katika kufanikisha mambo mbalimbali, kwa upande wetu tumeona vipaumbele vilivyopo ili tuweze kuona namna tunavyoweza kutoa mchango wetu kusaidia ukusanyaji wa takwimu Bora za kilimo , kikubwa ni kuendelea kujenga ushirikiano wa kuwezesha ufanisi wa tafiti mbalimbali" Amesema.
Wood ameeleza kuwa taasisi ya Bill na Melinda Gates imekuwa ikichangia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo Barani Afrika kupitia mashirika ya kimataifa yanayohusika na utoaji wa huduma kwa umma na kuitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi chache za Bara la Afrika zinazonufaika na miradi hiyo.
Amesema taasisi ya Bill na Melinda Gate kwa kipindi kirefu imekuwa ikitoa kipaumbele kusaidia miradi ya afya hasa mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, kusaidia huduma za Afya ya mama na mtoto pamoja na kuweka mkazo katika kuimarisha huduma za maji safi na maji Taka Barani Afrika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania Dkt.Albina Chuwa amesema kuwa Sekta ya Kilimo imeajiri watu wengi na inachangia asilimia 27 kwenye pato la Taifa.Amesema kutambulika kwa Takwimu za kilimo kuna umuhimu mkubwa katika uchumi wa Tanzania na kazi kubwa inayofanywa na NBS ni kuhakikisha kuwa inakwenda na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia katika kukusanya takwimu zake.
Dkt.Chuwa ameipongeza Taasisi hiyo ya kimataifa ya Bill na Melinda Gates kutokana na jinsi inavyosaidia kufanikisha miradi mbalimbali ya maenedeleo Barani Afrika Amesema Chini ya Mradi wa kuimarisha na kuboresha Takwimu za kilimo ambao uko chini ya shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) Taasisi ya Bill na Melinda Gate imekuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.
Amefafanua kuwa Chini ya mradi huo Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa mpango mkakati wa miaka 5 wenye lengo la kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa Takwimu za Kilimo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Prof.Innocent Ngalinda amesema kuwa Tanzania inaendelea kujenga uwezo wake wa ndani katika kuimarisha shughuli za tafiti kwa kutumia wataalam waliopo nchini.
Amesema Tanzania kupitia chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika ambacho kiko miongoni mwa vyuo vichache barani Afrika vinavyotoa mafunzo kwa watakwimu, kinaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani ili waweze kufanya tafiti za kilimo zenye matokeo chanya katika maendeleo ya taifa na sekta ya kilimo.


No comments:
Post a Comment