Mbunge wa Sikonge, CCM, Said Nkumba ametangaza kukihama hicho na kujiunga na Chadema, kwa madai CCM ‘haina mapenzi na watu’.
Nkumba anakuwa mbunge wa sita kutoka CCM kutimkia upinzani katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja.
Wabunge waliokihama chama hicho ni Edward Lowassa (Monduli), Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi), Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya.
Lowassa ametimkia Chadema na ndiye aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho kwa mwavuli wa Ukawa, kugombea urais katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana kutoka Tabora, Nkumba alisema: “Sikushawishiwa, nimejiondoa CCM kwa uamuzi wangu na nimefanya hivi kwa kuwa sikuwa nasikilizwa kwa kile nilichokisema.
“Niliipenda CCM kwa dhati kabisa, lakini sikuona sababu ya kuendelea kubakia CCM, sisikilizwi, chama hakina mapenzi na watu, ndiyo maana tunaondoka.”
Nkumba aliyekuwa kinara wa kuipinga Ukawa ambao baada ya kutoka bungeni kwenye Bunge la Katiba, alisimama kidete na kuanzisha “Tanzania Kwanza, Mbili yatosha” alisema amejiunga na upinzani ili kujenga chama cha Chadema.
“Mimi najiamini, ninakubalika ndani ya chama, sasa nimekuja huku, nataka kuendelea mazuri ya Chadema, ninaona huku kunanifaa,” alisema Nkumba.
Akizungumzia kuwa wanaokwenda upinzani ni makapi, Nkumba alisema kuwa hata makapi bado yanakuwa na faida.
“Unajua kuwa wakati mwingine makapi ya asali labda ukamua sawasawa, lakini kwa hapa, sisi bado tuna asali, si makapi yasiyokuwa na kitu.”
Kuhusu hatma ya CCM na kuondokewa watu mbalimbali na kujiunga upinzani, Mbunge huyo alisema kuwa wakuu wa chama hicho, lazima washtuke na wasipokuwa makini, huu utakuwa mwisho wa CCM.
“Hivi wewe hushtuki, wanaona kabisa chama kikubwa lakini watu wanaondoka, wanaona kabisa mwelekeo haupo, halafu wanaendelea na yao, ni wazi kuwa wataanguka,” alisema.
No comments:
Post a Comment