Rais Kikwete Amjibu Lowassa 'Kimtindo'. - LEKULE

Breaking

21 Aug 2015

Rais Kikwete Amjibu Lowassa 'Kimtindo'.



Rais Jakaya Kikwete, amefunguka na kusema hatishwi wala hashtushwi na maneno ya watu wanaosema serikali yake kwa miaka 10 haijafanya kitu.

Badala yake amesema kitakachomshtusha ni taarifa zozote za uchochezi kwa kutumia kivuli cha dini ama ukabila kwa kuwa vitu hivyo ni hatari na vinaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.

Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipotembelea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  (THBUB) na kuzungumza na watumishi wake ambao walitumia nafasi hiyo kumuaga.

Alisema watu wanaobeza mafanikio ya serikali yake hawezi kuhangaika nao kwa kuwa anajua kuna mafanikio mengi yamepatikana katika kipindi cha miaka 10 mpaka sasa na wanao uhuru na kusema chochote wanachotaka.

“Kuna watu wanasema sana serikali yangu haijafanya chochote, lakini hawa sitahangaika nao kwa kuwa najua kuna mafanikio mengi yamefanyika katika uongozi wangu,” alisema  Rais Kikwete.

Alisema mtu atakayehangaika naye ni yule atakayetoa kauli za kuashiria uchochezi kwa kutumia dini na ukabila kwa kuwa vitu hivi ni hatari kwa amani ya nchi na kwamba kwa hilo atakuwa mkali.

“Kuna uhuru wa kutoa maoni na kama kuna mtu anataka kusema au kukosoa serikali yangu, mimi sina tatizo na yeye aende hata pale Jangwani aseme siku nzima sina tatizo naye, lakini atakayejaribu kuleta uchochezi kwa kutumia dini na ukabila, huyo tutashughulika naye,"alisema.

Ingawa Rais Kikwete hakumtaja mtu yeyote, Julai 29, mwaka huu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anayegombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuwa Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kuwapatia wananchi maendeleo.

Lowassa baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, akiwahutubia wafuasi wa Chadema na wananchi katika ofisi za chama hicho mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na mambo mengine, alisema Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kusimamia uchumi kiasi cha bei za vitu kupanda kila uchao vikiwamo vibiriti, mafuta na vyakula.

Katika ziara zake za kutafuta wadhamini kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Zamzibar, Lowassa alirudia kauli hiyo na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, ilisimamia vizuri uchumi kuliko Serikali ya Awamu ya Nne.

No comments: