- Naye akabidhi nakala ya kitabu chake kipya kiitwacho; ‘KAMWE SI MBALI TENA’
Profesa Said Ahmed Muhammed (aliyevaa miwani) akimpa nasaha mwandishi wa ‘Paka wa Binti Hatibu’ Bwana Yussuf Shoka Hamad.
Profesa
Said Ahmed Muhammed akipokea nakala ya ‘Paka wa Binti Hatibu’ kutoka
kwa mwandishi wa kitabu hicho Bwana Yussuf Shoka Hamad.
Profesa
Said Ahmed akimkabidhi Bwana Yussuf Shoka Hamad nakala ya kitabu chake
kipya kiitwacho; ‘Kamwe si Mbali Tena’ nyumbani kwake Limbani, Wete.
Profesa Said Ahmed na Bwana Yussuf Shoka wakionesha nakala za vitabu vyao walivyoandika na kukabidhiana leo hii.
Mwandishi
mashuhuri wa kazi za fasihi ya Kiswahili nchini na mwalimu mzoefu
katika midani ya lugha na fasihi ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed
Muhammed amepokea nakala adhimu ya kitabu cha ‘Paka wa Binti Hatibu’
kutoka kwa mwandishi chipukizi wa tasnia hiyo Bwana Yussuf Shoka Hamad .
Tukio
hilo lilifanyika leo huko nyumbani kwa Profesa Said, Limbani Wete, Mkoa
wa Kaskazini Pemba wakati mwandishi huyo chipukizi alipomtembelea
mwandishi huyo nguli wa Afrika Mashariki na kujadili mambo mbali mbali
yahususyo uandishi na taaluma.
Katika
makabidhiano hayo, Profesa Said alimshukuru sana Bwana Yussuf Shoka
kwa juhudi zake na ujasiri alioonyesha wa kuandika kitabu hicho ambacho
kwa sasa kimejinyakulia umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa Kiswahili
duniani.
Akizungumza
kuhusu mapokezi ya kazi yake hiyo Bwana Yussuf alisema, kwa hakika
kitabu kimeuza na kupokelewa kwa kasi kubwa ambapo kwa sasa ameuza
nakala nyingi za kitabu hicho na bado kuna mahitaji makubwa ya kazi hiyo
hasa hasa visiwani Zanzibar.
‘Kwa
hakika nimeshangazwa sana na jinsi jamii ilivyompokea Paka wa Binti
Hatibu. Juzi juzi tu nilikuja na nakala hamsini (50) lakini kwa muda
usiozidi siku tatu niliuza nakala hizo zote. Na hadi sasa kuna orodha
ndefu ya wasomaji wanataka kitabu hicho. Kwa kweli nashukuru sana na
nimeemewa sana na mapokezi ya kazi yangu hii!’ Alisema Bwana Yussuf.
Akizungumza kuhusu washabiki wake wakubwa na wasomaji wa kazi yake hiyo Bwana Yussuf alisema;
‘Nimefurahishwa
sana kuona jinsi gani jamii yetu inathamini kazi za waandishi wazawa.
Tena hata kwa wasomaji wasiokuwa wa fani ya fasihi. Kwa mfano, nimeuza
nusu ya nakala zote kwa wafanyakazi wa PBZ, Pemba na zilziobaki kwa
wanafunzi na walimu wa Chuo kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Pemba. Kwa
kweli nashukuru sana kwa kuungwa mkono kiasi hiki!’
Pamoja
na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kitabu hicho, Profesa Said
alimnasihi mwandishi huyo chipukizi nchini kutovunjika moyo na
changamoto nyingi zinazomkabili kwa sasa na kumtaka aendelee kuandika na
kuielemisha jamii kwa kadiri ya vile anavyoimulika na kuiakisi kwa
minajili ya kuleta mabadiliko na maendeleo katika jamii ya Tanzania,
Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla.
Profesa
pia alimtaka mwandishi huyo anayejulikana zaidi kwa kazi yake ya ‘Paka
wa Binti Hatibu’ kuongeza kasi ya uandishi na kumtaka aisivunjike moyo
hata kidogo katika kukabiliana na shida zilizopo katika tasnia ya
uandishi hasa hasa za uchapishaji.
‘Nasaha zangu ni kukutaka tu uendelee kuandika kwa kasi hiyo hiyo. Usivunjike moyo kwani naona unaenda na kasi nzuri kwa sasa.’
Mwandishi
Yussuf Shoka Hamad hadi sasa ameshakamilisha kazi yake ya ‘Paka wa
Binti Hatibu’ na sasa anatarajia kuchapisha vitabu vyengine vitano mwaka
huu pindipo kazi hizo zitachapishwa kwa wakati unaofaa.
‘Kwa
kweli kuna msoyoyo mkubwa katika kuchapisha kazi siku hizi. Mchapishaji
anaweza kuchukua mua mrefu sana kukupatia majibu ya muswada wako na
hata kuuchapisha. Hii inarudisha nyuma kidogo kwa kweli’ Alisema Bwana
Yussuf Shoka kumwambia Profesa Said.
Kuhusiana
na kadhia hiyo, Profesa alimtaka Bwana Yussuf kujaribu kuwasiliana na
wachapishaji wengine ili kuharakisha juhudi zake za uchapishaji wa
vitabu.
Wakati
huo huo, Profesa Said alimweleza Bwana Yussuf kuwa hadi sasa
ameshaandika vitabu takribani 57 na moja ya kati ya kitabu chake
kinachotamba kwa sasa ni riwaya yake inayokwenda kwa jina la ‘Kamwe Si
Mbali Tena’ ambacho pia alimkabidhi Bwana Yussuf Shoka nakala ya kitabu
hicho.
Katika
mazungumzo yao, Profesa aligusia nukta mbali mbali zinazohusiana na
Elimu na maendeleo ya taifa pia sambamba nay ale ya uandishi wa vitabu
na kupanuka kwa kiwango cha taaluma nchini.
‘Jamii
ya Watanzania kwa sasa imepanuka kifikra na kimawazo. Ninaposema hivi
sikusudii wasomi tu, bali hata Watanzania wasiosoma wametanuka sana
kiupeo kiasi ambacho kasi ya maendeleo nchini inakuwa kubwa. Hivyo, ni
busara kabisa kwa wasomi kurejea nchini na kushirikiana na wenzao
wengine katika kuharakisha maendeleo hayo!’ Alisema Profesa Said.
Profesa
Said ni mwalimu mstaafu kwa sasa aliyeamua kwa makusudi kurejea nchini
kujiunga na wazalendo wengine katika kusukuma mbele maendeleo ya Taifa
ambapo kwa sasa na kwa nyakati tafauti amekuwa akifundisha katika chuo
kikuu cha Taifa (SUZA) na chuo kikuu kishiriki cha Elimu Chukwani.
Naye
Bwana Yussuf Shoka ambaye ni mzaliwa wa Wingwi, Wilaya ya Micheweni
mkoa wa Kaskazini Pemba ni mhadhiri wa Kiswahili na Fasihi katika chuo
kikuu cha London (SOAS) na pia anafundisha Kiswahili katika chuo kikuu
cha Cambridge nchini Uingereza.
No comments:
Post a Comment