Profesa Lipumba Aondoka Nchini Akiwa Chini ya Ulinzi - LEKULE

Breaking

7 Aug 2015

Profesa Lipumba Aondoka Nchini Akiwa Chini ya Ulinzi


Saa chache baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kujiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ametoweka nchini.

Hata hivyo, haikufahamika mara moja amekwenda nchi gani na atakaa kwa muda gani.

Profesa Lipumba aliondoka nchini baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacok jijini Dar es Salaam, ambako alitangaza kujiondoa katika chama chake na katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Taarifa zilizopatikana, baada ya kumaliza mkutano na waandishi, alielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na aliondoka nchini kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda (Rwanda Air).

Awali kiongozi huyo ambaye alivaa suti ya ‘dark blue’ na shati jeupe alikuwa apande ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) 485, lakini alibadili mwelekeo baada ya kufika uwanjani na kuamua kupanda Rwanda Air kuelekea Kigali saa 9 alasiri.

Chanzo cha uhakika kutoka uwanjani hapo, kilieleza  kuwa Profesa Lipumba, alifika saa 7:00 mchana akiwa na vijana wawili wa kiume ambao walionekana kama walinzi wake.

Katika muda huo ambao Profesa Lipumba alikuwa katika taratibu za kuondoka, palikuwapo na ndege nne tu za kwenda nje ya nchi.

Vijana hao ambao hawakujulikana majina yao, walikuwa wakifuatilia kila hatua ya kile alichokuwa akikifanya Profesa Lipumba, huku yeye akionekana mwenye wasiwasi na msongo mkubwa wa mawazo.

“Profesa Lipumba anaonekana hayuko katika hali ya kawaida, anaonekana ni mtu mwenye msongo wa mawazo, na pia ana wasiwasi kama vile kuna jambo linamsumbua.

“Macho yake yalionekana ni mekundu mithili ya mtu aliyekuwa akilia kwa muda mrefu, huku uso wake ukionekana hauna furaha,” kilisema chanzo chetu.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amelazimika kukatisha shughuli za kiserikali alizokuwa nazo Zanzibar na kwenda jijini Dar es Salaam kunusuru hali ya sintofahamu ndani ya chama hicho.


“Ndiyo hivyo imeshatokea, lakini tayari katibu mkuu amekuja bara kuhakikisha mambo yanakaa sawa na chama hakiyumbi,” alisema kiongozi wa CUF ambaye hakupenda kutajwa jina.

No comments: