INATISHA! Hivi ndivyo unavyoweza
kusema mara tu unapofika katika hospitali ya serikali ya Kijitonyama,
iliyopo Sinza Mapambano jijini Dar es Salaam kwani kuna uchafu mwingi
unaoenda tofauti kabisa na mazingira yanayostahili katika kituo hicho
cha huduma za afya, Risasi Mchanganyiko linakuthibitishia.
OFM ilishuhudia vyumba vya vyoo vikiwa
gizani, matundu matatu ya vyoo hivyo yakiwa yameharibika vibaya kwa
uchakavu na mbaya zaidi, kutokuwepo na maji ya kutosha.
Baadhi ya wagonjwa waliwaambia OFM kuwa
wanawake ndiyo wako kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi, kwa sababu
ya uchafu uliokithiri huko, kwani upo uwezekano mkubwa wa mtu kuondoka
na ugonjwa mwingine licha ya uliompeleka katika zahanati hiyo.
Katika vyumba vya vyoo, licha ya kuwa na
giza, kulikuwa na uchafu mwingi unaomzuia mgonjwa kuingia ndani hivyo
kuwaweka katika hali ngumu wale wanaohitaji kupima haja ndogo na kubwa
kabla ya kupatiwa matibabu.
Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mfawidhi
wa Zahanati hiyo, Lazarius Mhojah, alikiri kuwepo kwa mazingira hayo
machafu, lakini akajitetea kuwa uongozi wao una muda mfupi tangu uanze
kazi.


No comments:
Post a Comment