Aliyekuwa
Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alihamia Chadema hivi
karibuni ameamua kurejea katika chama chake cha zamani kwa madai
alikosea njia.
Nkumba
ambaye alihamia Chadema baada ya kushindwa katika kura za maoni
kugombea ubunge Sikonge, aliteuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya
Chadema lakini wanachama wa chama hicho walipinga kitendo cha Kamati Kuu
ya chama hicho cha upinzani kumteua wakitaka mgombea wao, Hijja
Ramadhan arudishwe jambo lililofanya Nkumba kuondolewa na kukosa nafasi
ya kugombea ubunge.
Nkumba
alipojitoa CCM alisema alikipenda kwa dhati chama hicho lakini hakuona
sababu ya kuendelea kubaki kwa kuwa hasikilizwi na hakina mapenzi na
watu.
Lakini
akizungumza Dar es Salaam jana, Nkumba alisema amerudi nyumbani kwa
kuwa alipotea njia na hakuona kama kuna mwelekeo Chadema.
Alipoulizwa
kuhusu kupewa jimbo na Chadema alisema hayo yaachwe, amerudi nyumbani
kwa kuwa ni kama rebound katika mchezo wa kikapu na watu wanaendelea
kucheza.
Katibu wa CCM Wilaya ya Sikonge, Seleman Majilanga alisema hakuna tatizo kwa Nkumba kurejea ilimradi afuate taratibu.
. “Unajua ukishahama chama, kadi yako inakuwa haina kazi na inabidi uanze upya na yeye inabidi aende kwenye tawi lake,” alisema.
Majilanga
alisema hana tatizo kumpokea mwanachama mpya au anayerudi na hajawahi
kuzungumza na Nkumba kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ndani ya chama
katika kura za maoni.
“Sisi tumejipanga kufanya kampeni zetu na kushinda bila yeye na kwa uhakika ushindi ni mkubwa katika jimbo letu,” alisema.
Nkumba alikuwapo katika uzinduzi wa kampeni za urais za CCM zilizofanyika Jangwani jijini Dar es Salaam jana.
No comments:
Post a Comment