MAGUFULI: FILIKUNJOMBE NI MAGUFULI AJAYE - LEKULE

Breaking

31 Aug 2015

MAGUFULI: FILIKUNJOMBE NI MAGUFULI AJAYE



Mgombea Urais kwa Tiketi ya CCM John Pombe Magufuli akimsikiliza Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa aliyepita bila kupingwa kueleza matatizo yanalolikabili jimbo hilo
Katikati ni John Pombe Magufuli mgombea Urais CCM, Kushoto ni Deo Filikunjombe aliyepita bila kupingwa Jimbo la Ludewa, na kulia ni Khamis Kayombo mgombea udiwani CCM Kata ya Mlangali
Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe aliyepita bila kupingwa akizungumzia jimboni humo akisisitiza jambo
Waziri wa nyumba, ardhi na makazi, Willium Lukuvi akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.
Filikunjombe akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mlangali


Katika hali iliyotegemewa na wengi Wilayani Ludewa ya kuungwa mkono kwa mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt John Pombe Magufuli imejidhihirisha hii leo katika uwanja wa mpira wa miguu Ludewa baada ya wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki mgombea huyo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Magufuli alimpongeza mbunge aliyepita bila kupingwa katika jimbo hilo Deo Filikunjombe, kutokana na washindani wengine wa vyama vya upinzani kushindwa kukidhi vigezo.
Magufuli ameingia Wilayani Ludewa akitokea Wilaya ya Songea Vijijini Jimbo la Madaba huku akiongozana na aliyekuwa Waziri wa ardhi, Nyumba na Makazi ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Isimani, Willium Lukuvi.
Magufuli amesema kuwa Filikunjombe ni mfano wa kuigwa na anastahili kuendelea kuwa mbunge wa Jimbo la Ludewa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Wilayani Ludewa kwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha shughuli za maendeleo zinasonga mbele.
Sawia na hayo ameeleza kuhamasika na utendaji kazi wa mbunge huyo huku akimuita kuwa ni mwamba wa Ludewa ambapo alimtaka kueleza matatizo yanalolikabili Jimbo hilo ikiwa ni pamoja na barabara huku akimuahidi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Akizungumza katika mkutano wa awali uliofanyika katika kitongoji cha Mgombezi, Kata ya Mavanga, Filikunjombe alisema kuwa wananchi wake wanakabiliwa na tatizo la maji, umeme na barabara ya lami ambapo ni pamoja na ile itokayo Njombe hadi Ludewa.
Hata hivyo Filikunjombe amemuahidi ushindi wa kishindo kwani wananchi wake wana imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi CCM hivyo wanachama wa CHADEMA, CUF na vyama vingine vya upinzani watampatia kura nyingi na imani yake kubwa kwamba Wilaya hiyo itaongoza Kitaifa kwa ushindi mkubwa.
"Umekuwa waziri wa ujenzi umetusaidia barabara mbalimbali tunakupongeza lakini tunaomba pia utusaidie barabara ya lami Kutoka Njombe kupitia Malangali, Ludewa mpaka Manda hivyo ikiwa kwa kiwango cha lami utakuwa umetatua changamoto kubwa na muhimu kwa wananchi" Alisema Filikunjombe
Magufuli amefikia hatua ya kumuita Mbunge huyo kuwa ni Magufuli ajaye kutokana na uwezo wake mkubwa wa utendaji kazi ambao umejidhihirisha Jimboni kwake na Tanzania nzima huku akijilinganisha naye kwani Tanzania inamfahamu vyema akiwa akiwa serikalini hususani Wizara ya Ujenzi.
Wakati huo huo alisema kuwa serikali ya awamu ya tano haitakuwa serikali ya lelemama kwani watendaji atakao wachagua ikiwa ni pamoja na mawaziri watakuwa ni wachapakazi na endapo kama watachelewesha maendeleo wataisoma namba.
Aidha Magufuli alisema kuwa serikali ya tano itakuwa ya watu makini wanaosimamia wananchi wake na kuwapenda ili kuweza kufanya kazi kwa makini na utatu uliotukuka kwani shida za watanzania anazifahamu vizuri hazisomi kwenye kitabu wala hahitaji kusimuliwa na mtu yeyote.
Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa ilani ya CCM imeelekeza vyema kuhusiana na mikopo ya wananchi ambapo kila kijiji kitapewa milioni 50 ili kutoa mikopo iliyo nafuu na kuwafanya wananchi wote kuweza kukopa na kukuza kipato chao cha kila siku.
"Natamka hadharani serikali yangu wanafunzi watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha Nne kwani inawezekana kwa sababu tayari wezi wachache wamekwisha anza kukimbia hivyo nitawanyoosha wote na kudhibiti ubadhilifu wa fedha unaobwinywa na wachache" Alisema Magufuli
Amesema alipokuwa waziri alikuwa anatumwa kufanya kazi lakini sasa atakuwa anawatuma viongozi wote ambao atawateuwa huku akieleza wazi kupita kwa Filikunjombe bila kupingwa kwa mara ya pili sasa ni kama yeye alivyopita Jimbo la Chato mara mbili bila kupingwa.
"Nimalize kwa kuwaomba wana Ludewa wote kuchagua diwani, Mbunge na Rais wa CCM ili maendeleo yaweze kutekelezwa kwa kasi" Alimaliza Magufuli
Akiwa njiani kuelekea Wilayani Ludewa, Magufuli amefanya mikutano zaidi ya Mitano kwa siku moja huku baadhi ya maeneo wananchi wakizuia msafara kutaka walau awasalimie.

No comments: