Magufuli Aahidi Kuboresha Masilahi ya Polisi ili Waweze Kukabiliana na Majambazi.......Kaongelea Pia Afya Yake - LEKULE

Breaking

30 Aug 2015

Magufuli Aahidi Kuboresha Masilahi ya Polisi ili Waweze Kukabiliana na Majambazi.......Kaongelea Pia Afya Yake



Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amesema serikali yake itaimarisha masilahi ya wafanyakazi wote wakiwamo polisi, ili wasiwe wanalinda na kukosa fedha za kula nyumbani na hatimaye kusinzia vituoni na kunyang’anywa silaha.
 
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kuzungumza kwa kina mpango wake wa kudhibiti wimbi la uvamizi wa vituo vya polisi, linalozidi kukua nchini na kuhatarisha maisha ya polisi na wananchi.
 
Akiwahutubia wakazi wa Makete, Dk Magufuli alisema anataka polisi wawe wanakwenda kazini wameshiba, hata jambazi akivamia wanamwua hapohapo bila kusubiri polisi jamii.
 
“Nazungumza kwa ukweli kwa sababu jeshi letu linatakiwa liheshimike, siyo mnakaa kwenye kituo watu wanachukua silaha wakati na ninyi mna silaha, “ alisema na kushangiliwa.
 
“Ninataka jeshi ambalo likimuona jambazi linamwasha kwa sababu yeye alikuja kuwawasha. Nataka iwe jiwe kwa jiwe, moto kwa moto, mguu kwa mguu, kichwa kwa kichwa, sikio kwa sikio, hayo ndiyo tunayoyataka.”
 
Dk Magufuli alisema maneno hayo huenda yakaonekana makali kwa baadhi ya watu lakini “hilo ndilo jibu”, na kwamba suala hilo linatakiwa kufanywa kwa kuzingatia sheria na utu wa binadamu.
 
Kauli hiyo aliirudia tena Njombe Mjini akisisitiza wakati wake “jambazi akija mchape risasi,” ili nchi iwe na amani na kuwafanya wananchi wafanye biashara zao kwa usalama kama nchi nyingine zilizoendelea.
 
Barabara
Dk Magufuli aliahidi kujenga barabara ya lami kuanzia Njombe kupitia Makete hadi Mbeya, na kueleza kuwa usanifu na upembuzi yakinifu vimeshafanyika na kilichobaki ni kuanza ujenzi akiingia madarakani.
 
Pia, aliahidi kuboresha maisha ya wasanii nchini, akiahidi kuwaanzishia mfuko maalumu hivyo kuwataka wasihofu kuwa anawatumia tu kwa sasa wakati wa kampeni, bali atawajali hata baada ya kushinda.
 
Mgombea huyo aliyeingia mkoa wa tano wa kampeni zake alizungumzia ilani ya CCM, hasa suala la elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kila kata, kuboresha huduma za umeme, afya, maji, pembejeo na kuimarisha masoko kwa wakulima.
 
Waziri huyo wa Ujenzi, jana alikutana na Naibu wake, Gerson Lwenge katika mkutano uliofanyika Makoga, Njombe Magharibi na kila mmoja kumnadi mwenzake.
 
Lwenge alisema Dk Magufuli kuwa amefanya naye kazi na kwamba ni mfanyakazi na “mkali kwelikweli anayetenda haki.”
 
Azungumzia afya yake
Akizungumzia afya yake, aliwataka Watanzania kutohofia akisema yupo imara. Aliwaambia wakazi wa Makoga wilayani Wanging’ombe kuwa yuko timamu na atapambana hadi mwisho.
 
Alieleza kuwa kuna uzushi umezuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaumwa na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), jambo ambalo siyo kweli.

No comments: