KATIKA kile ambacho kwa wakati huu kinaweza kuonekana kama kimemshtua Rais Jakaya Kikwete, ni hatua yake ya kurejea kauli ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi wa Afrika dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Kwamba
viongozi wa Afrika hawafurahii kwa namna ambavyo mahakama hiyo
inavyofanya kazi zake kwa kuwashughulikia zaidi viongozi wa mataifa ya
Afrika.
Kauli
hiyo ya Rais Kikwete ambayo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati
akifungua mkutano wa 16 wa Umoja wa Wanasheria wa Jumuiya ya Maendeleo
ya Uchumi Kusini mwa Afrika-SADC, imekuja siku moja baada ya ICC kueleza
kwamba inafuatilia mwenendo wa uchaguzi nchini.
Mwendesha
Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, amekaririwa na vyombo vya habari
vya Aljazeera na Gambia Today akisema kuwa Mahakama hiyo inatazama kwa
umakini mkubwa yanayotokea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu kama
ilivyofanya katika nchi za Kenya, Ivory Coast na Congo na kwamba
itachukua hatua za haraka kama kutakuwa na uvunjaji wa haki za binadamu.
Kauli
hiyo ya Bensouda ilitanguliwa na ile iliyotolewa siku chache zilizopita
na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Wiki
iliyopita akiwa katika ziara ya kutafuta wadhamini katika mikoa ya
Arusha na Mwanza, Lowassa alilitahadharisha Jeshi la Polisi juu ya uwepo
wa Mahakama ya ICC kutokana na kitendo chake cha kutumia nguvu dhidi ya
wapinzani kwa kuupiga mabomu msafara wake.
Zaidi
Lowassa pamoja na viongozi wa Ukawa walisema endapo vyombo vya dola
vitakiuka haki za binadamu hawatasita kumshtaki Rais Kikwete katika
mahakama hiyo huku wakisema tayari wameanza kukusanya ushahidi wa kwenda
kushitaki.
Hata
hivyo, Rais Kikwete akizungumza na wanasheria hao wa SADC, aliutaka
umoja huo kuwa imara katika kuzungumzia uonevu unaofanywa na ICC dhidi
ya viongozi wa Afrika.
“Kuna
hizi kauli zinazotolewa na viongozi wa Afrika kwamba Mahakama ya
Kimataifa inazionea nchi za Afrika na kuyaacha mataifa mengine ambayo
yanaonekana kabisa kuwa na machafuko lakini viongozi wake
hawashughulikiwi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema mfumo wa Mahakama hiyo unaonekana kuwa ni wa kibaguzi na hivyo kushindwa kutenda haki.
“Kuna viongozi katika sayari hii wanafanya makosa lakini mahakama hizi haziwashughulikii. Mahakama hizi zinatakiwa kutenda haki.
“Haiwezekani viongozi wa mataifa madogo ndio wanaonekana kufanya uhalifu lakini wale wa mataifa makubwa wanaachwa,”
alisema Kikwete huku akitolea mfano wa Rais wa Syria, Bashir Al-Asaad,
ambapo alisema aliwahi kuzungumza na Luis Ocampo kipindi akiwa Mwendesha
Mashtaka Mkuu wa ICC kuhusu kushughulikia mataifa haya makubwa.
“Nilimuuliza
Ocampo mbona mataifa makubwa yanaonekana waziwazi kufanya uhalifu dhidi
ya binadamu lakini ICC haifanyi kitu? Lakini cha ajabu alinijibu
itafanya nini…hii inaonyesha hakuna usawa,” alisema Rais Kikwete.
Pamoja
na hayo, Rais Kikwete alisema ataachia madaraka kwa amani na kwamba
baada ya hapo atarejea kijijini kwake kujishughulisha na kilimo na
ufugaji.
No comments:
Post a Comment