Siku tatu baada ya Baraza Kuu la Chadema kuridhia kumpumzisha kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya kutofautiana na Kamati Kuu kwa kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kiongozi huyo amesema yupo salama na wakati mwafaka ukifika atazungumza ya moyoni.
Akizungumza
kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwananchi tangu Chadema imkaribishe
Lowassa na hatimaye kumpitisha kuwania urais kupitia muungano wa Ukawa,
Dk Slaa amesema amekuwa akisikia mengi yakisemwa juu yake lakini yote
yamekuwa yakimchekesha tu.
Hakuhudhuria
vikao muhimu vya chama hicho na vile vya Ukawa, vikiwamo; wakati
Lowassa akitambulishwa rasmi, akichukua fomu, kikao cha Baraza Kuu na
juzi Mkutano Mkuu na hakuwa akipatikana kwa simu yake ya mkononi.
Wakati kimya kikitawala juu ya hatima yake, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuwa amejivua uanachama Chadema.
Lakini jana alisema: “Naangalia
mambo mengi yanayoendelea kwenye mitandao halafu ninacheka tu,
usifikiri sifuatilii, nafuatilia kinachoendelea na ninabaki nikicheka.”
Kuhusu
hatima yake kisiasa na madai ya kujiuzulu uanachama ndani ya Chadema,
alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa na atafanya hivyo wakati
mwafaka ukifika.
“Usijali wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
“Usijali wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
Kadhalika,
alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa maisha yake yapo hatarini
kwa kuwa anatishwa, Dk Slaa alisema hata hilo pia atalizungumzia wakati
mwafaka ukifika.
“Ndiyo hayohayo ninayosema, wala msijali nitazungumza wakati ukifika,” alisema na kusisitiza: “Nipo salama.”
Dk Slaa alisema kwa sasa yupo mapumzikoni nje ya jiji la Dar es Salaam ingawa hakutaka kueleza ni eneo gani.
Juzi,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifafanua tofauti iliyojitokeza
kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Dk Slaa wakati wa mchakato wa kumpokea
Lowassa.
Katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Chadema, Mbowe alisema wamekubaliana katibu mkuu huyo apumzike kwa muda... “Nina
hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na
yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri
wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.”
Ndesamburo na siri nzito
Mbunge
wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na makada wengine wa Chadema, jana
walikwenda kuonana na Dk Slaa nyumbani kwake na kufanya naye kikao cha
faragha.
Picha
zilizomuonyesha Ndesamburo akiwa na Dk Slaa na makada wengine akiwamo
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Jaffar Michael, zilisambaa kwa kasi
katika mitandao ya kijamii jana na kuibua mijadala.
Baadhi
ya waliochangia mijadala hiyo walidokeza kuwa huenda Ndesamburo
anayeheshimika ndani ya chama hicho alikwenda kujaribu kusawazisha hali
ya mambo.
Mkuu
wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwa picha hizo
ni halisi, baadhi zilipigwa juzi na nyingine jana mchana, lakini
hakutaka kuingia undani wa mkutano wa wanasiasa hao.
Ndesamburo alithibitisha kukutana na Dk Slaa: “Ni
kweli tulikwenda, kwani kuna tatizo gani? Si mzee mwenzangu? Halafu
bado ni mwanachama wetu, hajatoka Chadema, hivyo tuna kila haki ya
kwenda kumsalimia.”
Alipoulizwa
kama alikwenda kumsihi Dk Slaa arejee kuendesha mapambano ya kuing’oa
CCM, Ndesamburo alisisitiza kuwa walikwenda kumsalimia.
Michael alipoulizwa nia ya safari hiyo alijibu kwa kuuliza; “Dk Slaa ni katibu mkuu wetu kwani tunazuiwa kwenda kumsalimia?”
Dk
Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili baada ya Rais
Jakaya Kikwete na ndiye aliyekuwa akitajwa kuwania tena nafasi hiyo
kupitia Chadema na Ukawa kabla ya “kubadili gia angani” na kumteua
Lowassa.
No comments:
Post a Comment