UGONJWA wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na watu wawili wamethibitika kufa. Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni.
Kutokana
na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za uchaguzi
mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo kuwa
zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele. Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa akitoa
taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1).
Alisema
watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine ni mwanamke
na wanatoka Manispaa ya Kinondoni. Mkuu huyo wa Mkoa alisema ugonjwa
huo umethibitika baada ya vipimo vya maabara vya watu hao, kuthibitisha.
“Watu
wawili akiwemo mwanamume na mwanamke wamefariki dunia baada ya vipimo
vya maabara kuthibitisha ugonjwa huo. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote
za ugonjwa huo katika manispaa za Temeke na Ilala,” alisema Sadiki.
Alisema
endapo hali hiyo itaendelea kuwa mbaya, itabidi mamlaka za Dar es
Salaam kusogeza mbele kampeni za kisiasa, zinazotarajiwa kuanza mwisho
mwa wiki hii ili kuepusha mikusanyiko ya watu.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema wagonjwa wengine 30 wapo
chini ya uangalizi maalumu katika hospitali za Mwanayamala na Sinza,
ambapo 19 wapo Sinza na 11 Hospitali ya Mwananyamala. Wengine wanne
wameruhusiwa na kurudi nyumbani.
“Sampuli za wagonjwa sita zilizochukuliwa, wanne kati yao wamethibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo,” alisema Natty.
Alisema
wamepata dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa ajili ya
kukabiliana na ugonjwa huo. Jitihada mbalimbali zinaendea kuchukuliwa
ikiwemo kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji.
Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Dk Jackson Makanjo, aliwataka wakazi
wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni
kabla ya kula, na unapotoka chooni. Alitoa wito kwa wakazi wa Dar es
Salaam, kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuepuka kula ovyo
vyakula vya mitaani.
Alisema
ugonjwa huo ulianzia eneo la Kwa Ali Maua huko Kijitonyama na kisha
kuenea maeneo ya jirani ya Tandale, Manzese na Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment