Dar es Salaam.
Mvutano mkali ulioibuka jana katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.
Mvutano mkali ulioibuka jana katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.
Kutokana
na mvutano huo, viongozi wa vyama hivyo waliahirisha kikao hicho na
kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa watamtangaza
mgombea huyo Jumanne ijayo.
Kikao hicho
kilichowahusisha wabunge wote na viongozi wakuu wa vyama vya Chadema,
NLD, CUF na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa, kilifanyika jana katika
ukumbi wa Millenium, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba alishindwa kuwaeleza wanahabari
kilichowakwamisha kumtangaza mgombea, huku akisisitiza kuwa wanataka
kuweka mambo sawa.
“Hatuwezi kuwaangusha Watanzania na
kipindi hiki ndiyo chetu kwani tunaingia katika uongozi wa Serikali ili
kulikomboa taifa,” alisema: “Kuna mambo ya kukubaliana na kuweka sawa,
tutamtaja mgombea wetu Julai 14 (keshokutwa). Naomba niwaeleze
Watanzania kuwa Ukawa haiwezi kuvunjika tunachokifanya ni kuwa makini
katika maamuzi yetu.”
Alisema kikao cha Kamati ya Ukawa
kilifikia muafaka na jana kuwasilisha mrejesho kwa wabunge ndipo
ulipofikiwa muafaka wa kusubiri hadi keshokutwa, huku akisisitiza kuwa
katika kugawana majimbo wamekubaliana kwa asilimia zaidi ya 90.
Alipobanwa
aleleze ni mambo gani yaliyokwamisha kufikiwa kwa muafaka alisema:
“Kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama vyetu ila hayawezi kuleta
matatizo, tupo pamoja na tutatoa jibu la pamoja.”
Alisema
Ukawa imetokana na maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, hivyo kiongozi
atakayepitishwa na chama hicho lazima awe, mwadilifu, muwazi na
mwajibikaji.
“Lazima tuwe na mgombea atakayesimamia
mambo ya wananchi waliyotaka yawemo katika Katiba, mambo hayo ni yale
yaliyowekwa katika rasimu ya Katiba ya Jaji (Joseph) Warioba,” alisema
Profesa Lipumba.
Alisema kama katiba ya nchi ingekuwa na kifungu kinachoruhusu
vyama kuungana, vyama vinavyounda Ukawa vingeungana lakini kutokana na
sintofahamu hiyo katika Katiba, wanalazimika kutatua changamoto hiyo kwa
umakini mkubwa.
Kuhusu majimbo alisema; “ni kama
tumeshagawana yote isipokuwa ambayo yana wagombea wawili wawili, yaani
kutoka vyama zaidi ya viwili. Tumekubaliana majimbo zaidi ya 170 mpaka
sasa.”
Habari za ndani
Imeelezwa
kuwa katika kikao hicho kilichoanza saa tisa alasiri mvutano ulikuwa
kati ya viongozi wa juu wa CUF dhidi ya wabunge na viongozi wengine wa
vyama vyote vinavyounda Ukawa, wakiwamo wa CUF.
Habari
hizo zilieleza kuwa viongozi wa CUF wanashinikiza mgombea urais wa Ukawa
awe Profesa Lipumba, huku wabunge wa Ukawa wakimtaka Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa maelezo kuwa anakubalika zaidi.
“Unajua
Lipumba anataka kugombea urais wakati akitambua wazi kuwa upande wa
Zanzibar pia CUF inasimamisha mgombea urais. Wajumbe wa Ukawa wanataka
Chadema isimamishe mgombea upande wa Bara na kuiachia CUF Zanzibar,”
zilieleza taarifa hizo.
Ilielezwa kwamba viongozi wa
juu wa CUF, wakiwamo kutoka Zanzibar wametoa baraka zote kwa Dk Slaa
kugombea, lakini kikwazo kimebaki kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho
wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.
“Nakwambia wazi
muafaka hautapatikana na kikao hiki kitaahirishwa hadi Julai 14 au 15
maana huko ndani hakuna maelewano, kikubwa ni urais tu huko katika
majimbo hakuna shida,” zilieleza taarifa hizo.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, Dk Slaa, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Profesa Lipumba,
Katibu Mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe, Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Magdalena Sakaya.
No comments:
Post a Comment