Obama Aitaka Kenya iongeze Mapambano dhidi ya al Shabaab - LEKULE

Breaking

26 Jul 2015

Obama Aitaka Kenya iongeze Mapambano dhidi ya al Shabaab

Rais wa Marekani Barack Obama  jana  (25.07.2015) alifanya mashauri na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi na kujadili maswala kadhaa yakiwemo usalama, uwekezaji na uongozi.

Rais wa Marekani Barack Obama ameitaka Kenya kuongeza jitihada za kulikabili kundi la wanamgambo wa al Shabaab kutoka Somalia.

Obama amesema Marekani inahitaji kushirikiana kwa karibu zaidi na Kenya kuliangamiza kabisa kundi hilo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi.

Kiongozi huyo amesema mitandao ya kundi la al Shabaab imedhoofishwa katika Afrika Mashariki lakini kitisho bado kingalipo.

"Tumelipunguza eneo linalodhibitiwa na Al-Shabaab. Tumefaulu kupunguza udhibiti wao nchini Somalia na kuidhoofisha mitandao yao hapa Afrika Mashariki. Hiyo haina maana tatizo limetatuliwa," alisema Obama wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na mwenyeji wake rais Uhuru Kenyatta.

"Tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa makundi ya kigaidi, lakini bado yanaweza kusababisha maafa," akaongeza kusema Obama.

Rais Obama aliandaliwa gwaride la heshima katika Ikulu ya Rais kabla ya kufanya mashauri na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta.

"Tumekuwa na mazungumzo ya kufanya na Rais Barack Obama juu ya maswala muhimu yanayohusu Kenya na Marekani kama vile usalama na uhusiano wa kimaendeleo miongoni mwa maswala mengine," alisema Uhuru.

Mikataba yasainiwa
Mikataba kadhaa ya ushirikiano imetiwa saini ukiwamo ule wa ushirikiano katika swala la ugaidi. Rais Obama alisema, "Leo( jana )  tumezungumzia suala la kuimarisha uhusiano wetu wa kiusalama kama sehemu yetu ya maongozi pia tumezungumzia mikakati ya kukabiliana na itikadi kali hapa nchini na dunia nzima kwa ujumla."

Marais hao wawili  jana asubuhi walifungua kongamano la sita la ulimwengu kuhusu ujasiriamali katika ofisi za kabla Rais Obama kuzuru eneo la shambulizi la bomu la Agosti 7 mwaka 1998 na kuweka shada la maua kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa shambulizi hilo lililotekelezwa katika ubalozi wa Marekani wakati huo.
Kwenye kongamano hilo la ujasiriamali Rais Kenyatta alisema, "Nchi hii na bara hili hatuwezi kusema hatufanyi makosa lakini bila shaka tunaweza kudai kwamba tunasonga mbele. Cha msingi nikwamba tuko katika safari tunayowaalika mjiunge nasi. Tunaona nafasi nzuri inahitaji kuheshimu haki za binadamu."

Kongamano hilo la ujasiriamali linahudhuriwa na wajumbe wapatao 4,000 kutoka mataifa 120 ulimwenguni.

 "Changamoto ni nyingi. Ni vigumu kupata mikopo, ni vigumu kupata mafunzo na ujuzi wa kuendesha biashara na zaidi ya yote ni vigumu kwa wanawake na vijana ambao hawapati nafasi za juu za uwekezaji."

Viongozi hao wawili wamewahimiza vijana kuzingatia ufumbuzi unaolenga kutatua matatizo ya bara la Afrika.

Kutokana na makubaliano hayo ya kibiashara, mipango inafanywa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Marekani.

Ziara ya Rais Barrack Obama nchini Kenya haikuwa tu ziara ya kikazi bali pia kukutana na familia yake kwani alipata fursa ya kujiunga na jamaa zake kutoka kijiji cha Kogelo kaunti ya Siaya kwa chakula cha jioni katika hoteli moja ya kifahari alipowasili jijini Nairobi hapo juzi.

Leo Rais Obama  anatarajiwa kutoa hotuba ya hadhara katika uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani na kisha kuondoka nchini kwenda Addis Ababa Ethiopia kwa kongamano la viongozi wa Umoja wa Afrika.


No comments: