Nembo ya TBS inawanyanyua wajasiriamali wadogo nchini? - LEKULE

Breaking

30 Jul 2015

Nembo ya TBS inawanyanyua wajasiriamali wadogo nchini?

Hamasa imekuwa ikitolewa kwa walaji kutumia bidhaa ambazo zina nembo ya ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuepuka kutumia vitu vya kughushi, kama vinavyojulikana kwa wengi; feki.
Hali hii imekuwa ikiyafanya kampuni nyingi kubwa kuhakikisha wanafikia viwango ambavyo watatumia nembo hiyo ili bidhaa zao zisitiliwe shaka na watumiaji.
Hii ni fursa wanayoipata wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo, Tanzania ni nchi ambayo inapaswa kujenga mazingira mazuri kwa ustawi wa viwanda vidogo na vya kati.

Huu ni mfumo unaoweza kuifanya Tanzania kupiga hatua katika mapinduzi ya viwanda. Lakini swali, ni je, hawa wafanyabiashara wadogo wanaotaka kustawi, wanaweza kutumia nembo ya TBS?
Ofisa Masoko wa TBS, Gladness Kaseka anasema wana kanuni ambazo pia zinawapa haki wajasiriamali wadogo kutumia nembo hiyo tena bila malipo, tofauti na ilivyo kwa viwanda vikubwa.
Kaseka anasema hii ni fursa ya kipekee kwa wajasiriamali kuchangamkia fursa hiyo ya kuruhusiwa kutumia nembo ya ubora ya TBS bila kulipilia. Anasema Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe kwa ubora.

Lengo la kupewa bila malipo, anasema ni kuwapa fursa ya kujitanua na kukua zaidi na hasa ikizingatiwa mitaji yao bado ni midogo na wengi wanarejesha fedha walizokopa kwenye taasisi za fedha.

“Hadi hivi sasa wajasiriamali wadogo na wa kati karibu 200, wameomba na kupatiwa alama ya TBS,” anasema Kaseka.
Anawataja wajasiriamali wadogo ambao tayari wamepewa vibali vya kutumia nembo hiyo kuwa ni wauza maziwa, asali, unga wa lishe na mafuta ya alizeti.
Anasema lengo ni kumhakikishia mlaji kuwa bidhaa ya mjasirimali huyo ina ubora na imethibitishwa na TBS.

Pamoja na hali hiyo, anasema TBS inahakikisha mjasiriamali ametekeleza kanuni zote zinazolingana na aina ya biashara anayoifanya.
“Kwa wale wajasiriamali wa vyakula wanatakiwa wawe na taarifa fupi kutoka idara ya afya iliyo karibu na mahali pa uzalishaji au cheti cha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),” anasema Kaseka akifafanua:

“Ni vyema kuhakikisha kuwa barua inafafanua vizuri na kwa kina shughuli zinazofanywa na mjasiriamali huyo,” anasema Kaseka. Ofisa Viwango wa Chakula na Kilimo wa TBS, Zena Issa anasema wajasiriamali waliokwishapata leseni ya kutumia alama ya ubora wanapaswa kutunza taarifa za uzalishaji na mauzo ambazo wanatakiwa kuzionyesha kwa wakaguzi wa Shirika la Viwango.
Anasema alama ya ubora huthibitisha kuwa bidhaa husika inafaa kwa matumizi husika, huongeza ubora wa bidhaa, huongeza wateja zaidi, hulinda mazingira ya eneo husika na kumhakikishia mlaji usalama wake wa kiafya katika matumizi.

“Alama ya ubora wa TBS huwafanya wanunuzi kununua bidhaa bila wasiwasi. Kwa upande mwingine alama hiyo humlinda mzalishaji katika ushindani dhidi ya bidhaa hafifu na humwezesha kulihakikishia soko lake katika kiwango na hivyo ni bora na salama kwa matumizi yaliyokusudiwa,” anasema Issa.

Mjasiriamali wa kuuza maziwa katika mtaa wa Negamsii wilayani Babati Mkoani Manyara, Magreth Tluway anasema mteja anaponunua bidhaa anapaswa kuangalia endapo ina alama ya uthibitisho wa ubora. Mjasiriamali wa kuuza asali, John Aloyce, mkazi wa mtaa wa Nangara, anasema kupitia nembo ya TBS, ameongeza idadi ya wateja wananunua bidhaa.

“Napenda kutoa wito kwa wajasiriamali wenzangu wadogo na wa kati, waliopo Manyara na mikoa mingine, tujitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata fursa hii kwani itatusaidia katika kutuongezea soko la bidhaa zetu,” anasema Aloyce.

Wajasiriamali waliofanikiwa kutumia nembo ya TBS wanaonyesha kuwa bidhaa zao zinakubalika, hivyo ni moja ya njia za kuwainua kibiashara.
Jambo muhimu ni kwamba nembo hiyo pia inapaswa kuwachochea wajasiriamali hawa kuongeza juhudi za kutengeneza bidhaa bora ambazo zitashindana na zile za viwanda vikubwa.


No comments: