Nchimbi Afunguka baada ya CCM Kulikata Jina lake Kwenye Kinyang'anyiro cha Ubunge - LEKULE

Breaking

22 Jul 2015

Nchimbi Afunguka baada ya CCM Kulikata Jina lake Kwenye Kinyang'anyiro cha Ubunge


Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi (pichani), amefunguka kuhusu mambo kadhaa na kueleza kuwa  Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa kutofautiana katika vyama vya siasa ni jambo la kawaida katika nchi yenye demokrasia.

Dk. Nchimbi alisema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea Mjini kuikataa fomu ya kuomba kuwania ubunge aliyochukuliwa na wananchi kwa madai haikuwa imekidhi vigezo.

“Ninachowambia Watanzania tuzoee kutofautiana, kutofautiana katika vyama vyetu ni jambo la kawaida katika demokrasia, tunaweza kutofautiana katika mapendekezo, lakini tukifika kwenye maamuzi tunakuwa kitu kimoja kuunga maamuzi tuliyoafikiana na huo ndio utaratibu mzuri wa kujenga demokrasia,” alisema.

Dk. Nchimbi ambaye alikuwa akihojiwa na kituo cha Radio One jana asubuhi, alisema demokrasia ya kutoelezana ukweli siyo demokrasia bali demokrasia ya kweli ni ya uhuru wa fikra.

Alisema mtu ambaye hapendi CCM iwe shwari ni mtu ambaye  haitakii mema nchi na kwamba hana mpango wa kuhama chama hicho kwa sababu amelelewa na CCM.

Aliongeza kuwa taarifa za kwamba yeye na makada kadhaa wamehojiwa na chama kuhusiana na kauli walizozitoa wakati wa vikao vya uteuzi wa mgombea urais kuwa hawakuridhishwa na mchakato huo hazina ukweli.

”Mimi nimekulia CCM na bado nitaendelea kuwa CCM kutokana na misingi ya kifikra na kisera, sasa kama kuna mtu anayewaza kuwa naweza kuhama CCM hiyo ni fikra ya kijinga sana,” alisema.

Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Songea Jumapili iliyopita ilikataa kupokea fomu ya kugombea ubunge ya aliyojaziwa Dk. Nchimbi na baadhi ya wakazi kwa madai kuwa haikukidhi vigezo.

Hata hivyo, mwezi uliopita Dk. Nchimbi aliandaa mkutano wa wanachama wa CCM, viongozi na wananchi na kuwashukuru kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chake cha uongozi kisha kuwatangazia kwamba hatagombea tena ubunge katika jimbo hilo mwaka huu.


Dk. Nchimbi alikuwa akitajwa kuwa huenda atagombea katika Jimbo la Mbinga Magharibi lililopo wilayani Nyasa ambalo lilikuwa likishikiliwa na marehemu Kapten John Komba, aliyefariki  dunia mapema mwaka huu


No comments: