Mbunge Aiomba Serikali Ipige Marufuku Pombe za Kienyeji na Za Viwandani ( Bia) - LEKULE

Breaking

1 Jul 2015

Mbunge Aiomba Serikali Ipige Marufuku Pombe za Kienyeji na Za Viwandani ( Bia)

MBUNGE wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya (CUF), ameitaka Serikali kupiga marufuku unywaji wa pombe kwa kuwa ni kichocheo cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Akiuliza swali bungeni jana, Sanya alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kupiga marufuku uuzwaji wa pombe hizo zikiwemo za kienyeji na pombe za viwandani.
 
“Kama hilo haliwezekani basi katika bajeti ijayo iongeze tozo pombe kwa asilimia 100 ili fedha zitakazopatikana ziende zikasaidie waathirika wa Ukimwi au miradi ya REA (Mradi wa Umeme Vijijini),” alisema Sanya.
 
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema Serikali imepiga marufuku unywaji wa pombe haramu.
 
“Vile vile tunapiga marufuku unywaji wa pombe kupita kiasi, unywaji wa pombe kupita kiasi haukubaliki, unywaji wa bia sio kunywa kreti zima.
 
“Kwa jinsi tulivyoumbwa binadamu tuna uwezo wa kunywa bia moja kwa kila saa moja, hata hivyo kimaumbile kwa mwanamke anaruhusiwa kunywa angalau bia moja hadi tatu kwa saa 24 na mwanaume anatakiwa kunywa bia tatu hadi nne kwa saa 24,” alisema.
 
Awali akijibu swali la msingi la Sanya, Dk. Kebwe alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imetengeneza miongozo maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watumishi wa afya kutoa ushauri kuhusu lishe bora kwa waathirika wa VVU wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU.
 
“Ushauri huo ni pamoja na aina ya vyakula vinavyomfaa mtumiaji wa dawa ambavyo vinapatikana kwenye jamii yake.
 
“Pia waathirika wa VVU wote wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi wanafanyiwa uchunguzi mara kwa mara kubaini hali yao ya lishe na kupewa ushauri au matibabu stahiki ikiwa ni pamoja na virutubisho kama vile vitamin, madini na chakula na dawa,” alisema Dk. Kebwe.
 

Katika swali lake Dk. Kebwe alitaka kujua Serikali inawasaidiaje waathirika wa VVU wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU kupata lishe bora

No comments: