Lowassa: "Nimechoka Kuitwa Fisadi .......Mwenye Ushahidi wa Rushwa dhidi Yangu Ajitokeze Ili Aeleze nilitoa lini, wapi na kwa nani." - LEKULE

Breaking

2 Jul 2015

Lowassa: "Nimechoka Kuitwa Fisadi .......Mwenye Ushahidi wa Rushwa dhidi Yangu Ajitokeze Ili Aeleze nilitoa lini, wapi na kwa nani."

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliwataka wanaomhusisha na ufisadi kuacha mara moja kwa sababu hakuna hata chembe ya ukweli katika tuhuma hizo.


Lowassa, aliyeonekana kuzungumza kwa hisia, alisema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Mbunge huyo wa Monduli alikuwa mmoja kati ya makada tisa waliorudisha fomu jana, ikiwa ni siku moja kabla ya kuisha kwa muda uliowekwa na chama hicho. 
 
Wengine waliorejesha fomu jana ni Elidephonce Bilohe, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Hassy Kitine, Mariki Marupu, Dk Asha Rose Migiro na Lazaro Nyalandu.

Hadi sasa, tayari wanachama 32 kati ya 42 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wamerudisha fomu na kazi hiyo itahitimishwa leo.

Hakuna mtu ambaye amejitokeza hadharani kumtuhumu Lowassa kwa ufisadi, lakini tuhuma hizo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na mbunge huyo wa Monduli kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kuibuka sakata la mkataba wa ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na Kampuni ya Richmond RDC ya Marekani ambayo ilionekana haina uwezo.

Wakati huo, Lowassa alisema kwenye hotuba yake ya kujiuzulu kuwa amefanya uamuzi huo “ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji, lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika wa kusema uongo ndani ya Bunge kwa kumsingizia mtu.”

Akizungumza jana kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, Lowassa alirudia wito wake wa kutaka wenye ushahidi wa tuhuma hizo wajitokeze hadharani.

“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo,” alisema.

“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?”

Alisema yeye ni mwadilifu na anaposema atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu na bila kumuonea haya yeyote.

“Ndugu wanachama wenzangu na wananchi kwa jumla, ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema.
Alisema tuhuma hizo zimeendelea hata wakati wa kutafuta wadhamini kwa baadhi ya watu kuzieneza.

“Tumefanya kazi ya kutafuta na kuomba udhamini kwa uadilifu na umakini mkubwa. Na hapa nitumie nafasi hii pia kuwashukuru makatibu na viongozi wote wa Chama katika mikoa na wilaya kwa maandalizi mazuri katika kuifanikisha zoezi hili,” alisisitiza.

Alisema kuwa walifanya kazi yao vizuri kinyume kabisa cha vijimaneno vilivyoenezwa kwamba kulikuwa na matumizi ya fedha katika kuwatafuta wadhamni.

“Hivi kweli, unahongaje watu zaidi ya laki nane?” alihoji.

Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alisema tuhuma hizo zimekuwa zikitolewa na watu ambao wamekosa hoja na zinatolewa bila ushahidi wowote.

Alisema akifanikiwa kushika wadhifa wa urais, ataendesha nchi kwa kufuata katiba na sheria.

Kuhusu safari ya kusaka wadhamini, Lowassa aliwashukuru wana-CCM waliomdhamini na kwamba walijitokeza kwa wingi jambo ambalo limempa picha ya kuungwa mkono na kukubalika.

Alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini walifanya hivyo kwa utashi wao na bila kishawishi chochote cha fedha au fadhila nyingine yoyote.

Alisema kuwa udhamini alioupata ni kielelezo cha vitendo kwamba wapo naye katika Safari ya Matumaini.

“Nina matumaini na imani kubwa kwamba mtaendelea kuniunga mkono ndani ya Chamna chetu ili kwa pamoja na mshikamano ndani ya Chama niweze kuteuliwa kugombea kiti cha urais,” alisema.

Lowassa alisema: “Kwa mafanikio haya ya hatua ya awali nina imani kwamba ni ishara njema kueleke hatua zilizobakia na uweza wake Mwenyezi Mungu Mungu, na kwa ushirikiano wenu kwa pamoja tutalivuka daraja ili hatimaye niwatumikie kwa utumishi uliotukuka nikiwa Rais wa Awamu ya Tano.”

Aliongeza kuwa: “Nina shauku kubwa ya kuunganisha nguvu na uwezo ya kila Mtanzania katika kupambana na umasikini wa nchi hii. Umasikini wa watu wetu siyo amri ya Mwenyenzi Mungu. Nina imani kabisa kwa pamoja tunaweza kutumia rasilimali tulizo nazo kwa bidii, maarifa na ufanisi zaidi ili kutokomeza umasikini huu.”

Ukumbi wa Whitehouse, jana ulijaa wana-CCM ambao walifika kushuhudia Lowassa akirudisha fomu tofauti na idadi iliyowahi kutokea kwa wagombea wengine kadhaa waliomtangulia. 
 
Hali hiyo ilisababisha foleni kwenye Barabara ya Mtaa wa Kuu unaopita mbele ya ofisi za CCM, na kusababisha usumbufu kwa wapita njia.

Lowassa alifika akiwa ameongozana na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru na wenyeviti wa chama hicho wa mikoa kadhaa pamoja na wabunge.

Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Diana Chilolo (Viti Maalumu), Profesa Juma Kapuya (Urambo Magharibi), Mary Chitanda (Viti Maalumu), Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga na Mary Mwanjelwa (Viti Maalumu).


Baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa waliomsindikiza ni Jesca Sambatavangu kutoka Iringa, Ramadhan Madabida (Dar es Salaam), Khamis Mgeja (Shinyanga), Mgana Msindai (Singida) na Joseph Msukuma (Geita).

No comments: