Hatimaye waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekitosa
chama chake cha CCM na kutua Chadema. Huko ndiko anatarajia kuendelea na
safari yake ya matumaini aliyoianza na sasa anatarajiwa kupambana na
ikiwezekana kukidhoofisha chama kilichomlea katika harakati za kuingia
Ikulu.
Serikali ya CCM ilimpa fursa nyingi za uongozi
kuanzia ukurugenzi katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC)
na uwaziri. Amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sheria na
Bunge 1990–1993), Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi (1993–1995),
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Umaskini
1997–2000), Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo (2000–2005) na Waziri
Mkuu (2005–2008).
Alipata kila aina ya msaada
aliouhitaji, akawa na nguvu za kiutendaji, kudhoofisha upinzani katika
jimbo lake na hata kuthubutu kufanya maamuzi magumu katika nafasi
mbalimbali alizoshika. Lakini baada ya kufanyiwa fitina wakati wa
mchakato wa kuteua mgombea urais kupitia CCM, mbunge huyo wa Monduli
tangu 1990 ameamua kuungana na wapinzani kuitia adabu CCM.
Lowassa
atakuwa kada wa tatu mwenye nguvu kuitikisa CCM na kuidhoofisha katika
baadhi ya maeneo. Makada wengine waliowahi kuitesa CCM, kwa upande wa
Bara ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema; na kwa
Zanzibar aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharrif Hamad.
Je,
Lowassa ataujenga upinzani? Je, anaingia Chadema peke yake au pamoja na
mafuriko ya watu waliokuwa wanakanyagana kumdhamini alipokuwa anagombea
urais kupitia CCM? ni maswali ya msingi kujiuliza. Makada kadhaa
wamewahi kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani lakini yeye anakuwa kada
wa kwanza aliyewahi kuwa waziri mkuu kukihama chama tawala
Mrema ndani ya NCCR
Upinzani
dhidi ya chama tawala nchini una historia ndefu. Kada wa kwanza kupinga
sera za chama tawala ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kombona
enzi za Tanu na kwa kuwa mfumo wa vyama vingi uliharamishwa mwaka 1965,
alikosa sehemu ya kupumulia hivyo alikimbilia uhamishoni, Uingereza.
Miaka
ya 1980 waliibuka wanaccm kadhaa waliotaka mabadiliko, akiwamo mwasisi
wa Chama cha Wananchi (CUF), James Mapalala. Harakati zake zilihesabika
kuwa uhaini hivyo watu waliogopa kujiunga naye hasa walipomwona
akikamatwa na kuwekwa kizuizini mara kwa mara.
Miaka ya
mwanzoni mwa 1990 akajitokeza Mrema. Kwanza, alipokuwa Waziri wa Mambo
ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, alikuwa kizuizi cha mageuzi.
Pamoja
na vigingi hivyo, mwaka 1991 wanaharakati walianzisha vyama vya
kiharakati. Mapalala alianzisha Chama cha Wananchi na wengine kama
Mabere Marando wakianzisha National Committee for Constitutional Reforms
(NCCR) ambayo baadaye iligeuzwa kuwa chama cha NCCR-Mageuzi.
Waanzilishi
waliotoka CCM walikejeliwa kwa kuitwa majina kama vibaraka waliotumwa
na mataifa makubwa kuisambaratisha nchi; malaya tu wa kisiasa. Pia
walifananishwa na mchwa ambao watakufa kwa jua kali kwenye mwamba.
Haikutosha.
Siku Mrema alipotembelea kwa helikopta
wilaya ya Namanyere, Rukwa na kukuta imesimikwa bendera ya NCCR,
alirejea Dar es Salaam na mikakati ya kuiangamiza kabla haijawa tishio.
Baadhi
ya wajumbe wakashawishiwa kujiondoa waanzishe vyama vyao ili NCCR
idhoofike. Ikawa hivyo, mmoja aliasisi UMD huku waliobaki waliibadilisha
NCCR na kuunda chama kwa jina la NCCR-Mageuzi, kikipewa maana ya
National Convention for Construction and Reform yaani Chama cha Mageuzi
na Ujenzi wa Taifa.
Baada ya upinzani kuruhusiwa rasmi
Julai 1992 vikasajiliwa vyama vingine kama DP, FORD, NLD, NRA, PONA,
Tadea, UPDP, CUF, Chadema, TLP, na UDP na vingine vinaendelea
kusajiliwa.
Pili, mambo yalipokuwa magumu serikalini
Mrema aliitosa CCM na kuipaisha NCCR alipojiunga nayo mwaka 1995 na
akateuliwa kuwa mgombea urais.
Mrema alipeleka mawimbi
mazito CCM lakini kwa vile hakuwa na mtaji wa wanaccm aliohama nao, kura
hazikutosha kumwezesha kuongoza nchi. Hata hivyo, aliingiza wapinzani
kadhaa bungeni miongoni mwao ni waliojiondoa CCM kama Steven Wassira
(Bunda), Makidara Mosi (Moshi Mjini), Dk Masumbuko Lamwai (Ubungo),
Wengine
ni Thomas Ngawaiya (Moshi Vijijini), Festus Limbu (Magu), MwinyiHamisi
Mushi (Siha), James Mbatia (Vunjo), Paulo Ndobho (Musoma Vijijini),
Mfalamagoha Kibasa (Iringa Mjini), Marando (Rorya) na wengineo.
Mapalala na Hamad
Baada
ya Mapalala kukutana na viongozi wa chama cha Kamahuru ya Zanzibar
kuunda Chama cha Wananchi (CUF), hakudumu, aliondolewa baada ya kutokea
kutoelewana na wenzake. Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad ndiye
alibaki kuwa nguzo imara ya chama hicho na kutikisa kuta za CCM visiwani
Zanzibar.
Kama ilivyokuwa kwa Mapalala, Maalim Seif
amepitia masahibu mengi ya kutisha lakini yu imara hadi leo. Alipokuwa
CCM alikuwa madhubuti, kiongozi mwenye mvuto na aliyeamini katika
misingi.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kuwania urais wa
Zanzibar kupambana na Mzee Idrid Abdul Wakil uliwachefua CCM.
Wakamfitinisha. Januari 1988 alitemwa kwenye Baraza la Mapinduzi na
akavuliwa cheo cha Waziri Kiongozi. Mei 1988 akafukuzwa uanachama wa CCM
pamoja na wenzake sita kutoka Baraza la Wawakilishi. Mei 1989 alitiwa
mbaroni na akafunguliwa kesi kwa madai ya kukutwa na nyaraka za siri za
Serikali. Tangu mwaka 1989 hadi 1991 alikuwa mahabusu ya Polisi
Zanzibar.
Pamoja na mateso hayo, Maalim Seif amejenga
upinzani wa nguvu Zanzibar na kuitokomeza CCM kisiwani Pemba
akishirikiana na makamanda kadhaa baadhi wakiwa ni waliowahi kukabiliwa
na kesi ya uhaini kama Zulekha Ahmed Mohamed, aliyewahi kuwa naibu
waziri wa Fedha Tanzania, Hamad Rashid Mohamed, Machano Khamis Ali,
Hassan Mbarouk Hassan, Mohamed Ali Maalim, Shariff Haji Dadi, Ramadhan
Shamna Abdi, Soud Yusuf Mgeni, Said Zam Ali, Pembe Ame Manja, Abbas Zam
Ali, Nassor Seif Amour, Abdallah Said Abeid na Zeina Juma Mohamed.
Baadhi
ya makada wa zamani wa CCM wanadai kuwa Maalim Seif hajawahi kushindwa
katika chaguzi za Zanzibar, japokuwa hajaachiwa ikulu. Nguvu yake
ilisababisha kubadilishwa katiba ili chama chake kishirikishwe katika
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kwa upande wa Bara,
CUF ilipata wafuasi wengi akiwamo Mwenyekiti, Prof Ibrahim Lipumba
aliyerithi mikoba ya Musobi Mageni. Mwaka 2000 na 2005 amewahi kushika
nafasi ya pili katika mbio za urais.
Safari ya Lowassa
Kwa
wiki tatu sasa upepo wa siasa umekuwa ukivuma kwa Lowassa aliyetawala
siasa za hapa nchini tangu mwaka 2008 alipojiuzulu nafasi ya waziri mkuu
kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni isiyo na uwezo wala mtaji
ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Kamati
Maalumu ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Dk Harrison Mwakyembe ilifanya
uchunguzi wa kina na kuwasilisha ripoti bungeni kwamba kulikuwa na mkono
wa Lowassa katika utolewaji wa zabuni hiyo. Serikali inasema
aliwajibika kisiasa.
Lowassa hakuwa na neno alipokatwa
kuwania urais mwaka 1995 lakini mazingira yaliyojitokeza ya kukatisha
safari yake ya ikulu mwaka huu yamezua nongwa na kuteka siasa za nchi
kwa wiki tatu sasa.
Waliomkata wamekuwa wakihaha, bila
mafanikio, kumsihi asihame chama. Amepuuza na ameamua kuondoka, tayari
amepokewa na Ukawa ambao wanatarajia kumteua kugombea urais kupambana na
mgombea wa CCM, Dk John Magufuli.
Safari yake ya
matumaini ni kuishi ikulu. Matarajio ya Ukawa ni kupanga ikulu.
Matarajio ya Watanzania ni kupata mabadiliko nje ya CCM. Ikiwa Lowassa
atamega nusu ya wanachama na mashabiki wa CCM, chama hicho tawala
kitaanza kuonja joto ya jiwe na kuwa chama pinzani.
Dk Slaa na Dk Kabouru
Watu
wengine waliowahi kuhama CCM ni mwasisi wa Chadema aliyewahi kuwa
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei na wanasiasa wengine
kama Bob Makani. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye mwaka
1995 alishinda kura za maoni ndani ya CCM katika jimbo la Karatu, lakini
wenye chama walimtosa wakamteua Patrick Qorro (marehemu). Wananchi
walimwambia Dk Slaa aende chama chochote watamfuta na alipojiunga na
Chadema mwaka huo, akashinda na hadi leo CCM ni chama cha upinzani
Karatu.
Wanasiasa wengine mashuhuri waliowahi kumeguka
CCM ni aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema Dk Amani Wallid Kabouru
ambaye leo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.

No comments:
Post a Comment