Lembeli ashinda kura za maoni Chadema, Bulaya almanusura.......Viti maalumu vyamuokoa - LEKULE

Breaking

31 Jul 2015

Lembeli ashinda kura za maoni Chadema, Bulaya almanusura.......Viti maalumu vyamuokoa


Wabunge wawili waliohama CCM hivi karibuni, James Lembeli na Ester Bulaya wamepitishwa katika kura za maoni kuwania ubunge kupitia chama chao kipya.

Wakati Lembeli akipitishwa kwa kura za kishindo kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini, Bulaya alishinda katika nafasi ya viti maalumu baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Jimbo la Bunda Mjini.

Wanasiasa hao sasa wanasubiri uteuzi wa Kamati Kuu ya Chadema utakaofanyika Agosti 5 na 6.

Ushindi wa Lembeli
Katika uchaguzi huo wa juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kahama aliwabwaga wenzake 13 aliogombea nao akipata kura 168 kati ya 262 zilizopigwa, akifuatiwa na John Katibu aliyepata kura 45, Peter Shita (17) na Emmanuel Madoshi aliyepata kura 10.

Wengine ni Muta Nyerere (4), Felician Maige (4), Zacharia Obadia (3), Tadeo Mwati (2), Arnold Mtajwaka (2), Prosper Denga (2), Deusdedit Madinda (1), Reuben Macheyeki (1). Victor Mbwana na Richard Makingi waliambulia patupu. Katika uchaguzi wa viti maalumu, Winfrida Mwinula alishinda kwa kura 34 akifuatiwa na Salome Makamba aliyepata kura 30.

 Bulaya
Kama isingekuwa ni kura za maoni za viti maalumu zilizomfuta machozi, Bulaya alikuwa tayari ametupwa nje baada ya kuanguka katika Jimbo la Bunda Mjini.

Bulaya aliyekuwa miongoni mwa makada saba wa chama hicho waliokuwa wanawania kuliwakilisha jimbo hilo, alipata kura 37 kati ya 182 zilizopigwa akiwa nyuma ya Pius Masururi aliyeibuka mshindi kwa kura 65 na  Magembe Makoye aliyepata kura 40.

Baadaye katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), uliofanyika baadaye usiku, Bulaya alipata kura 71 kati ya 110 zilizopigwa na kuwabwaga Godliver Masamaki aliyepata kura 31, Joyce Sokombi (4), Minza Shani (3), Dk Jane Nyamsenda (1) na Alice Wandya aliyeambulia patupu.

Awali, Bulaya alikwaa kisiki baada ya jina lake kuwa miongoni mwa waliokatwa na kamati ya utendaji inayosimamia majimbo hayo wakidaiwa ni wageni katika chama; wapenda fujo na matabaka, akiwa pamoja na Chacha Nyamhanga, Sulemani Daudi lakini walirudishwa kundini baada ya kikao cha viongozi na watiania.


Katika Jimbo la Bunda Vijijini, Sulemani Daudi aliibuka mshindi kwa kura 84 kati ya 127 zilizopigwana kuwashinda John Masenza aliyepata kura 14, Dk Lucas Webiro (11), Frank Mongateko (8), Edgar Chibura (5) na Mathias Bandio aliyepata kura moja.

No comments: