Dar/Dodoma.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.
Rais Kikwete
alisema hayo baada ya Magufuli kutangazwa kuwashinda makada wengine
wawili waliopigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kuzoa kura
2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi ambao alisema unaakisi kumalizika
kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za kuwania kuteuliwa na CCM
kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Balozi
Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 253 (sawa na
asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro alikuwa wa mwisho kwa kupata
kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura zilizopigwa kwenye mkutano huo
mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio ziliharibika.
“Kila
mtu anaitwa jembe,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akianza kutaja sifa
za Magufuli ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
“Lakini huyu ni zaidi ya
jembe. Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga,
ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”
Kikwete
aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa
alipokuwa akifuatilia wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki
kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na
makubaliano.
“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.
“Tulikuwa
na wagombea 338 lakini sasa tunaye mmoja na tuna kundi moja tu la CCM.
Timu Magufuli imeshaondoka. Wengi walidhani CCM itafia hapa, lakini
ushindi huu ni ishara kuwa CCM ni moja.
“Tunatakiwa
kuacha kuteuwa watu kwa urafiki na kujuana ili tushinde kwa sababu imani
huzaa imani. Sina shaka kuwa tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi
lazima tuwe na mikakati mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,”
alisema.
Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi
waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa
akitajwa kama kinara kwenye mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya
kujadiliwa na vikao vya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi
ya miaka 10, alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu
wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Iyombe
alisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa
hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila
anachofanya.
“Ninachoweza kusema ni kuwa huyu hataki
mchezo, kwa hiyo wale wavivu wavivu najua watashindwa kuendana na kasi
yake ya utendaji kazi,” alisema.
Iyombe alimmwagia sifa
Magufuli kuwa hapatani na wazembe na wavivu, jambo ambalo alisema
liliwahi kuwakimbiza baadhi ya wahandisi walioajiriwa wizarani hapo.
“Tangu
alipoingia wizarani 2005, kama naibu waziri alianza kufanya kazi
vizuri, sina sifa zaidi kuwa ni mchapa kazi, hawezi kuwa na upendeleo
kulingana kabila, wala undugu. Hajali kitu, ukiharibu kazi atakuponda
tu,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Segolena
Francis alimsifu Magufuli kuwa ni mtu anayejali muda, anayependa kazi
yake na asiyetaka mtu legelege.
“Nimejifunza mambo
mengi kwake na ninatumaini kuwa kama atakuwa Rais, basi Taifa litakuwa
limepata mchapakazi. Anafuatilia kila kitu yeye mwenyewe, hana makundi,
hana ukabila wala udini,” alisema.
Segolena alisema
Magufuli ni miongoni mwa viongozi ambao hawapendi kupindisha mambo na
wanataka kila kitu kiende kama kilivyopangwa.
Aliyesoma naye alonga
Sifa kwa
Dk Magufuli pia zilitolewa na Ndyesumbilai Florian, mmoja wa watu
waliosoma naye Shule ya Sekondari ya Katoke Biharamulo na ambaye sasa ni
mhariri msanifu wa gazeti la Mwananchi.
“Magufuli
aliwahi kusema kuwa siku moja atakuwa kiongozi mkubwa na hivyo ndoto
hizo zinaweza kutimia baada ya kuteuliwa kuwania urais kupitia CCM,”
alisema Ndyesumbilai.
Ndyesumbilai alisema hata
walipokuwa kidato cha tatu, Magufuli alizungumzia nia ya kugombea Jimbo
la Biharamulo wakati huo likishikiliwa na Chief Kasusula.
“Nafikiri
aliwahi kugombea lakini hakufanikiwa, lakini mara kadhaa alikuwa
akisema kuwa anatamani majimbo ya ubunge yashikiliwe na vijana,”
alisema.
Ndyesumbilai alieleza zaidi kuwa hata baada ya
kufanikiwa kuwa mbunge wa Chato, bado Magufuli aliendelea kusema kuwa
safari ya uongozi bado ni ndefu kwake.
Wananchi wamkubali
Ushindi
wa magufuli pia ulikuwa gumzo na faraja kwa baadhi ya wananchi, akiwamo
wakuru Sinde warioba, ambaye aliamua kujipongeza kwa kupata bia mjini
Dodoma.
“Magufuli hajanipa chochote, lakini tangu
niliposikia anagombea urais nilikuwa nasali siku zote ili ashinde na
bila shaka Mungu kanisikia kwa sababu ni masikini mwenzangu, ametoka
kwenye kwenye tabu kama mimi. Sina hela ila nimekuja kunywa pombe kwa
sababu Magufuli kapita,” alisema Warioba (60) mkazi wa Samora.
Dereva
wa teksi mjini hapa, Chausi Katuma alisema Dk Magufuli ni mtu asiye na
makundi na kwamba atasaidia kukirudisha chama hicho, lakini anatakiwa
kujipanga zaidi kwa sababu ana changamoto kubwa sana.
“Dk
Magufuli ni mtu “neutral’ (asiyefungamana na upande). Ukiangalia tangu
awali hakuwa na kambi na hata kama ilikuwepo haikuwa kali. Lakini lazima
ajipange kwa sababu asije akawa kama JK, wakati anaingia tulikuwa na
matumaini makubwa lakini alichokifanya sicho tulichotarajia,” alisema
Katuma.
Uteuzi huo unaonyesha kubadilisha upepo kwa
baadhi ya vijana waendesha bodaboda ambao juzi baada ya kukatwa Lowassa
waligadhabika na kutishia kuwa hata kama walikuwa ni makada wangehamia
upinzani.
Omari Haule, mwendesha bodaboda wa Area D
mjini hapa, alisema uteuzi huo si mbaya kwa sababu Magufuli hakuwa na
kundi na utendaji wake ni mzuri hivyo kidogo CCM imeonyesha kutafuta mtu
anayekabiliana na mtu waliokuwa wanamtaka.
“Nafsi
kuridhika sana baada ya Lowassa kukatwa bado kwa sababu hatuwezi kujua
huyu aliyeteuliwa bila kujali chama chake. Hatuwezi kujua kuwa
atatusaidia kama tulivyotarajia kwa Lowassa,” alisema Haule.
Hata wakati wengine wakifurahia kukamilika mchakato huo, baadhi hawataki kuamini kuwa mambo yameshakamilika.
Mkazi
wa Nkuhungu, Alex Kilatu alisema mchakato haujenda vizuri kwa sababu
inaonekana kwa makusudi walimuandaa Dk Magufuli kushika cheo hicho
lakini “aliyestahili alikuwa Edward Lowassa”.
“Sina
mashaka na Dk Magufuli kuteuliwa kuwa Rais, lakini kwa sababu yametokea
basi ndiyo hivyo. Ila kutoka moyoni sijafurahi asilimia 100 kwa kuwa
mchakato haukuwa sawa kwa sababu hata wajumbe wa NEC (Halmashauri Kuu)
walionyesha wazi mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuwa walimtaka Lowassa,”
alisema Kilatu.
No comments:
Post a Comment