MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba jana alianzisha mchakato wa kuwania urais kupitia muungano wa kambi ya upinzani nchini unaofahamika kama Ukawa, huku akisema yeye ndiye mtu pekee anayefaa kupeperusha bendera ya vyama vya upinzani.
Akitangaza azma yake ya kuwania urais baada ya kuchukua fomu jijini Dar es Salaam, alisema kutokana na kubobea katika masuala ya uchumi, amefanya tafiti nyingi kuhusu matatizo ya umaskini yanayowakabili wananchi wakati nchi ina rasilimali nyingi; hivyo anajua mahali pa kuanzia mara atakapochaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Kama akifanikiwa kutimiza ndoto hiyo, itakuwa historia ya kipekee kwa kambi ya upinzani nchini, kwani tangu uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, CCM ndiyo inayong’ara na hivyo kuendelea kuishika dola.
Aidha, katika chaguzi zilizotangulia tangu 1995, Profesa Lipumba amekuwa akiwania urais mfululizo, lakini kura zake zimekuwa ‘zikipwaya’. Hii ina maana kwamba, anawania urais kwa mara ya tano.
Jana, akizungumza kwa kujiamini, alisema anaamini kuwa rasilimali za taifa hili zikisimamiwa vizuri na kupunguza ufisadi na wizi, fedha za kuiendesha Serikali zipo nyingi na hivyo akasema kuwa iwapo akiteuliwa na Ukawa na kisha kuchaguliwa kuwa Rais hatakuwa na mswalie mtume na mafisadi.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema yuko tayari kumpigia debe mgombea mwingine wa Ukawa ambaye atasimamishwa na umoja kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa, iwapo yeye hatapitishwa.
Umoja huo wa kambi ya upinzani uliokusudia kusimamisha mgombea mmoja wa urais, na pia kuungana mkono kwenye majimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unaundwa na CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vipaumbele vyake
Mwanasiasa huyo alivitaja vipaumbele vyake iwapo atateuliwa na kisha kuchaguliwa kuwa Rais, kuwa ni kuwekeza kwa watoto wadogo katika kupata lishe bora.
Alisema jambo hilo wanasiasa walio wengi hawalizungumzi wakati ni tatizo kubwa nchini kwani kati ya watoto 100 watoto 42 wana udumavu, hali inayofanya wasiwe na uwezo wa kupata elimu kutokana na kudumaa kiakili.
Kipaumbele kingine ambacho atashughulika nacho ni suala la ajira ambalo alisema atahakikisha bandari za Tanzania zinakuwa chanzo cha upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Alitolea mfano wa bandari ya Mtwara akisema kwa kuwa ina kina kirefu kila meli ina uwezo wa kutia nanga bandarini hapo, hivyo atahakikisha eneo hilo kunajengwa viwanda vingi ambavyo vitatoa ajira kwa vijana.
Alisema pia ataitumia bandari ya Tanga kuhakikisha eneo hilo linakuwa maalumu kwa kilimo kwani kila zao lina uwezo wa kustawi katika wilaya za mkoa huo.
Aliongeza kuwa anaamini kuwa kilimo kikisimamiwa vizuri kinaweza kuwa chenye manufaa kwa Watanzania. Kipaumbele chake cha tatu ni kuwekeza katika sekta ya afya ambako alisema atahakikisha anaweka udhibiti wa magonjwa sugu kama kifua kikuu na mengineyo ambayo yanawasumbua Watanzania.
Pia alisema atasimamia vyema miundombinu ili kuongeza ufanisi na usafirishaji wa mizigo hasa kwa nchi jirani zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ukuaji wa uchumi.
Kuhusu utawala bora, Profesa Lipumba alisema atasimamia utawala bora ili atakapomaliza muda wake wa uongozi ashinde tuzo maalumu inayotolewa kwa viongozi wa Afrika walioongoza vizuri ijulikanayo kama tuzo ya ‘Mo-Ibrahim’.
Katiba Mpya
Mwanasiasa huyo alisema mara atakapochaguliwa kuwa Rais atahakikisha Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo tume yake ilikuwa chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, anairudisha kwa wananchi, akidai Katiba Pendekezwa ya sasa imeacha mambo ya msingi.
Alidai mambo ya msingi ambayo yameachwa kwenye katiba pendekezwa kuwa ni kuhakikisha kiongozi wa umma anayepewa zawadi anaikabidhi serikalini, jambo ambalo katika katiba pendekezwa limeondolewa.
Vita ya Rushwa
Alisema kutokana na kukithiri kwa rushwa hapa nchini hata ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hazifanyiwi kazi.
Alisema watu ambao wameghushi nyaraka na kuiba fedha za umma bado wanakula raha na wengine walioiba fedha hizo wanazitumia kusaka urais.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Alisema akiteuliwa na kuchaguliwa kuwa Rais cha kwanza atakachokifanya ni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kujenga taifa lenye umoja.
Profesa Lipumba ni kiongozi wa kwanza miongoni mwa viongozi wa Ukawa kuchukua fomu ya kuwania urais, lakini tayari mwanachama wa NCCR-Mageuzi, Dk George Kahangwa ameshachukua fomu ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mgombea wa Chadema hajapatikana, lakini ndani ya chama hicho mchakato wa kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ukiwemo urais bado zinaendelea.
Baada ya mchuano huo wa ndani ya vyama vya upinzani, mshindi wake atakabiliana na mgombea kutoka chama tawala, kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayetarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba mwaka huu.
Rais Kikwete meiongoza nchi tangu mwaka 2005 na kuthibitishwa tena kwa kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment