Urais 2015: January Makamba Apokelewa Kishujaa Mkoani Iringa, Apata Wadhamini 600 - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

Urais 2015: January Makamba Apokelewa Kishujaa Mkoani Iringa, Apata Wadhamini 600

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameungwa mkono na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Iringa ambako alipata wadhamini zaidi ya 600.

Akizungumza na wadhamini wake hao, January alisema endapo atafanikiwa kuwa rais atahakikisha CCM inalirudisha Jimbo la Iringa Mjini ambalo kwa sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwani ataweka kambi katika mji huo.

Alisema kuwa ataimarisha miundombinu, ikiwa ni pamoja na kutanua kiwanja cha ndege cha Nduli na kukifanya kuwa cha kimataifa ili wananchi waweze kupata ajira kitakappingiza watalii wengi na kuongeza pato la mkoa huo pamoja na  kuzijenga barabara kwa kiwango cha lami.

Aidha, January, alisema anaamini CCM kitamchagua kiongozi kwa kujiamini na kuwaomba wananchi wapuuze kauli za watu wanaodai kuwa endapo chama hakitawasimamisha katika  nafasi hiyo basi kitasambaratika.

Alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa dhamana ya nchi hii iko mikononi mwa CCM, hivyo akipata nafasi hiyo au asipopata atakuwa mstari wa mbele katika kukirudisha chama pamoja kutokana na kuwa na makundi katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Aliongeza kwa kuwaomba wananchi wa mkoa huo kupitisha ushawishi kwa viongozi wanaopitisha majina kuwa wamchague kijana anayekusudia kuleta mabadiliko ya kweli ambaye ndiyo yeye.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa UVCCM mkoani humo, Kaunda Mwaipiana, alisema vijana hao wanamuunga mkono January katika kipindi chote kwani wanaamini anaweza kuivusha nchi hapa ilipo kutokana na hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati akitangaza nia iliyobeba mikakati thatibi ya maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Wilaya ya Iringa, Abeid Kiponza, alimpongeza kwa uthubutu wake wa kuomba nafasi hiyo na kwamba kama alivyoona vijana wenzake wa mkoa wa Iringa wameonesha nia ya kumuunga mkono. 

No comments: