Membe: Watoseni wanaojaribu urais - LEKULE

Breaking

20 Jun 2015

Membe: Watoseni wanaojaribu urais

Shinyanga. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewataka Watanzania kuwa makini katika kuchagua viongozi, badala ya kukurupuka, kwa kuwa baadhi ya waliochukua fomu za kugombea urais wanataka kujaribu tu.

Membe alitoa kauli hiyo jana mkoani Shinyanga alikokwenda kutafuta wadhamini katika nafasi anayoomba ya kugombea urais.

Alisema makada hao wanajua kwamba hawana sifa, lakini wanachukua fomu kwa ajili ya kujipima.

“Lazima uwe na hekima na busara unapotaka kugombea nafasi ya ngazi ya juu ikiwamo urais, huwezi kwenda kuchukua fomu wakati hata hujawahi kushika wadhifa wowote ndani ya chama. Unataka kwenda kujifunza ukiwa madarakani? Watu kama hao kuweni nao makini,” alisema Membe.

Alisema mtu anayetaka kugombea urais anapaswa kuzingatia vigezo 13 vilivyowekwa na chama, lakini kuna watu wameshindwa kujipima kabla ya kuchukua fomu.

“Walitakiwa kujitathmini wenyewe kwani hata haya makofi mnayonipigia mimi na hao wengine mnawapigia nawaomba mchuje na kuwa makini,” alisema Membe.

Katika hatua nyingine, Membe alisema hakuna chama tawala chochote duniani kitakachoangushwa na wapinzani, bali chama chenyewe kinajimaliza na wanachama wake kutokana na kuwa na mamluki ndani yake.

Lowassa atikisa Mbeya

Wakati huohuo, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema akichaguliwa kuwa rais mbali na kuendesha nchi kwa mchakamchaka, atahakikisha anawatetea wafanyabiashara ndogondogo ‘Machinga’ ili wafanye biashara zao bila kuhangaika na kufukuzwa barabarani.

Alisema ataimarisha biashara za mipakani kwa kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi ili kuona kila mmoja anakuwa na uchumi ulioimarika kwa kupewa mikopo ya kutosha kwa ajili ya kuendesha biashara zao.
“Ikizingatiwa Mkoa wa Mbeya umepakana na nchi za Zambia na Malawi, lakini wananchi hamnufaiki chochote na mipaka hiyo. Nikiingia madakarani nitahakikisha naweka mipango ya kuwawezesha kiuchumi ili kuinua vipato vyenu kupitia biashara za mipakani,” alisema Lowassa.

Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Adam Kundya alisema viongozi wengi huingia na kutoka miyoyoni mwa watu wanaowaongoza, lakini kiongozi wa kweli huacha nyayo zake kwenye mioyo ya wananchi.

Kabla ya Lowassa kutua katika viwanja hivyo, ilitangulia helikopta iliyokuwa imembeba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wa Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni ambayo alizunguka hewani kwa takribani dakika saba akiwa usawa wa Ofisi za CCM kabla ya kutua nje ya ofisi hizo.

Makamba adai kujenga viwanda Tabora

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema pamoja na Mkoa wa Tabora kuchangia pato kubwa la Taifa hasa kupitia zao la tumbaku, haufaidiki na uchumi.

Akizungumza na wanachama waliomdhamini mjini Tabora alisema wananchi wanatumia nguvu kubwa kuzalisha, huku kipato chao kikiwa hakilingani na jasho wanalolitoa.

Alisema mkoa huo hauna viwanda kabisa licha ya kulima mazao ya tumbaku na pamba.

“Hapa mnalima pamba na tumbaku, lakini hakuna viwanda vya mazao hayo na hivyo ajira kuzipeleka nje ya mkoa na kuwaacha vijana wenu hawana ajira,” alisema.

Makamba alisema kukijengwa viwanda vya mazao ya tumbaku na pamba, vijana watakuwa wamepata ajira ambayo sasa hawana kutokana na viwanda kujengwa nje ya mkoa.

No comments: