Marais EAC wataka uchaguzi wa Rais Burundi uahirishwe - LEKULE

Breaking

1 Jun 2015

Marais EAC wataka uchaguzi wa Rais Burundi uahirishwe

WAKUU wa Nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), wameitaka Burundi kuahirisha uchaguzi kwa takribani mwezi mmoja na nusu ili kurejesha hali ya amani nchini humo na kulitaka Bunge kusimamia mchakato huo.
 
Aidha, wametoa wito wa Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN)na wadau wengine kuunga mkono juhudi za EAC katika kumaliza matatizo ya Burundi.
 
Akisoma maazimio ya viongozi hao yaliyofikiwa kwenye kikoa cha pili cha dharura cha kujadili hali ya Burundi kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera alisema maamuzi hayo yanazingatia hali ilivyo nchini Burundi na kutaka kusogeza mbele uchaguzi ili kuweza kurejesha amani nchini humo.
 
“ Tunazitaka mamlaka zote nchini Burundi kuhakikisha inasitisha uchaguzi kwa muda usiozidi mwezi mmoja na nusu na kuliomba Bunge kusimamia uahirishwaji wa uchaguzi huo,” alisema.
 
Alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya wakuu hao kupokea taarifa ya mawaziri wa mambo ya nje na wanasheria wakuu au mawaziri wa sheria wa nchini wanachama, ripoti ya mwakilishi wa UN katika Ukanda wa Maziwa Mkuu na ile ya timu ya Wazee wa Jumuia ya Afrika Mashariki inayoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba..
 
Uchaguzi wa Wabunge nchini Burundi ulipangwa kufanyika Juni 5 mwaka huu na ule wa rais uliopangwa kufanyika Juni 26.
 
 Hii ni mara ya pili kwa EAC kuagiza uchaguzi huo kusogezwa mbele, kwani katika kikoa cha kwanza waliagiza uchaguzi huo kusogezwa mbele kwa muda usiozidi kipindi cha uongozi uliopo madarakani.
 
Katika kikao cha jana kilichoanza saa 8:20 mchana na kumalizika saa 11:09, ambacho Rais Pierre Nkurunziza aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Alain Nyamitwe, kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame aliwakilishwa na Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Uhusiano Valentine Rugwabiza.
 
Pia kilihudhuriwa na Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Mwenyeikiti wa Kamishna ya AU, Dk. Nkosazana Dlamini Zuma huku Mwenyekiti wa Ukanda wa Maziwa Makuu, Eduardo Dos Santos aliwakilishwa na katibu wa jumuia hiyo, Profesa Ntumba Luaba.
 
Sezibera alisema pia EAC imeagiza vikundi vya vijana ambavyo vinaushirika na vyama vya siasa nchini Burundi kunyang’anywa silaha na kuitaka serikali kuweka mazingira mazuri ambayo yatawafanya wakimbizi kurejea nchini mwao.
 
Aidha, EAC imepongeza kurejea kwa utawala wa kikatiba nchini Burundi baada ya kutokea jaribio la mapinduzi. 
 
Akiwa Tanzania kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa kwanza wa EAC waliokutana Mei 13 kujadili mgogoro wa kisiasa nchini humo, majenelali wa juu wa nchi hiyo walifanya jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza ambalo lilizimwa na majeshi ya nchi hiyo.
 
“ EAC inasikitishwa na hali ya nsitofahamu inayoendelea nchini Burundi. Tunawataka wadau kuacha vurugu na machafuko yaliyosababisha vifo, uharibifu wa mali na wengine kukimbia nchi yao.”
 

Machafuko yalianza nchini humo tangu Aprili 26, mwaka huu na kusababisha zaidi ya vifo 20, huku maelfu wakikimbia nchi yao, yametokana na hatua ya Rais Nkurunziza kutangaza azima ya kuwania muhula wa tatu wa uongozi, jambo ambalo linalalamikiwa na wapinzani kwa madai kuwa ni kinyume na katiba ya nchi hiyo.

No comments: