Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunja Baraza hilo itakayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein leo.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunja Baraza hilo itakayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein leo.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya Spika wa
Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kutoa utangulizi kwa wajumbe akiwataka
watengue kanuni ili viongozi wa kitaifa watakaohudhuria shughuli hiyo
waweze kuingia ukumbini badala ya kukaa sehemu ya kawaida ya wageni
waalikwa.
Baada ya kutoa utangulizi, Spika Kificho
alianza kuwahoji wajumbe wanaokubali viongozi wa kitaifa waruhusiwe
kuingia ndani ya Ukumbi wa Baraza kwa kuwataja wakiwamo Rais wa
Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, mpambe wa Rais na
kuungwa mkono kwa kupigiwa makofi na sauti za ndiyo.
Hata
hivyo, alipomtaja Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad
wajumbe wote waliokuwapo katika Baraza hilo, ambao wote ni wa CCM,
walikataa wakisema kwa sauti “hapana,” kitendo ambacho kilimfanya Spika
kurudia kutamka jina hilo kwa zaidi ya mara tatu na majibu yalikuwa
hapana.
Hatua ya wawakilishi kumkataa Maalim Seif,
imekuja siku moja baada ya mawaziri na wajumbe wa CUF kutoka nje ya
Baraza wakisusa kujadili na kupitisha muswada wa sheria wa bajeti kuu ya
matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16 wakipinga pamoja na
mambo mengine, mchakato unaoendelea sasa wa uandikishaji wapigakura
katika Daftari la Kudumu.
“Mnakubali kutengua kanuni
kuruhusu viongozi wa kitaifa kuhudhuria katika shughuli yetu ndani ya
ukumbi? Wageni wetu ni Rais wa Zanzibar, mpambe wake, Jaji Mkuu na
Makamu wa Kwanza wa Rais,” alihoji Spika Kificho lakini alipingwa baada
ya kulitaja jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed
aliwasilisha hati ya Serikali kuhusu marekebisho ya kanuni za Baraza.
Waziri
Aboud alisema, Rais wa Zanzibar atakagua gwaride maalumu la Polisi
kabla ya kuhutubia Baraza hilo saa 9.30 alasiri na kuwataka wajumbe wote
kufika kabla ya kuwasili kwa Rais.
Kuhusu uamuzi wa
kumkataa Maalim Seif, Aboud alisema upo katika mamlaka ya wajumbe kwa
mujibu wa kanuni za Baraza hilo na kwamba hatua itakayofuata ni Spika
kumwandikia barua Maalim Seif ya kutohudhuria shughuli hiyo ili kulinda
uamuzi wa baraza hilo.
“Baraza ni chombo cha kikatiba,
Serikali hatuna uwezo wa kuliingilia na kanuni ndivyo zinavyosema.
Wageni ambao ni viongozi wa kitaifa lazima utengue kanuni kwa kuwauliza
wajumbe kama wanakubali au kukataa,” alisema.
Waziri
Aboud alisema SMZ haitaongeza muda wa Baraza ili kutoa nafasi ya
Mwakilishi wa Kwa Mtipura (CCM), Hamza Hassan Juma kuwasilisha hoja
binafsi ya kutaka wananchi waulizwe kama wanataka kuendelea na mfumo wa
sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au la akisema kwa mujibu wa
ratiba ya kikao cha bajeti, muda umemalizika na kumtaka kuangalia hoja
yake katika siku za baadaye.
Azimio lazua mjadala
Kaimu
Mnadhimu wa CCM, Ali Salum Haji ambaye pia ni Mwakilishi wa Kwahani,
alisema wajumbe walifikia hatua ya kumzuia Maalim Seif kuhudhuria
shughuli hiyo akisema ni Katibu Mkuu wa CUF, hivyo kitendo cha mawaziri
na wawakilishi kususia Baraza hilo, kwa vyovyote, kulikuwa na baraka
zake. “...hatujasikia kauli yoyote kutoka kwake ya kuwakemea na kama
tungemruhusu ingeonekana anawachuuza wenzake.”
Hata
hivyo, alisema kama Maalim Seif anataka kuhudhuria, anaweza kuingia
katika ukumbi wa wageni unaotumiwa kufuatilia matukio ya baraza hilo
lakini si kujumuika na viongozi wengine walioalikwa ambao watakuwa ndani
ya ukumbi.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail
Jussa Ladhu alisema wamesikitishwa na tukio hilo, lakini hawajashangazwa
kwa sababu wanaofanya hivyo ndio waliokuwa wakipinga kuanzishwa kwa
SUK.
Alisema tangu kuundwa kwake, SUK ilipata
misukosuko mikubwa ikiwamo baadhi ya mawaziri na wawakilishi wa CCM
kuwahamasisha wananchi wa majimbo yao kupiga kura za hapana wakati wa
Kura ya Maoni ya kuchagua kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2010.
“Kinachotokea
wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, kinaleta ufa ndani ya Serikali ya
pamoja na tayari tumeanza kuchukua hatua mbalimbali kuvilalamikia
vyombo vinavyohusika na dhamana ya uandikishaji, polisi na jumuiya za
kimataifa,” alisema Jussa.
Alisema inasikitisha wajumbe
wa Baraza wameshindwa kujadili hoja iliyojitokeza ya wao kususia kikao
cha bajeti ili kujua ukweli wake.
Jussa alidai kuwa
tangu kuanza kwa uandikishaji, kumekuwa na mambo yanayofanyika kinyume
na sheria yakiwamo watoto chini ya umri wa miaka 18 kuandikishwa katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura, vyombo vya ulinzi na usalama kutumika
kutisha watu pamoja na kuibuka kwa watu wenye silaha wakiwa wameficha
nyuso usoni (ninja) na wengine wakivaa vinyago.
Alisema
matatizo yanayojitokeza, hivi sasa, yamechangiwa na utata mkubwa katika
uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Kudumu na Usajili wa
Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Akizungumzia hatua
ya wajumbe wa CUF kususia vikao, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar,
Awadh Ali Said alisema walikuwa sahihi kwa vile utaratibu waliotumia ni
moja ya njia za kisiasa za kutoa hisia zao kidiplomasia.
“Mjumbe
wa Baraza la Wawakilishi anatumikia mabwana watatu kwa wakati mmoja,
jimbo na wananchi, chama chake cha siasa na maelekezo yake na Serikali,
ndiyo maana Tume ya Mabadiliko ya Katiba tulisema mawaziri wasiwe
wabunge au wawakilishi ili kutenganisha majukumu yao,” alisema Awadh
ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema
kwa kuwa wananchi ndio waathirika wa mambo ya uandikishaji na usajili
wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, mwakilishi hawezi kukaa kimya
hata kama ni waziri, kwa vile huo ndiyo wajibu wake.
Hata
hivyo, alisema kitendo cha kuzuiwa kwa Maalim Seif kushiriki katika
shughuli ya Baraza kinaweza kudhoofisha SUK kwa sababu wakati huu wa
kuelekea Uchaguzi Mkuu, Serikali inatakiwa kuwa na umoja pamoja na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi wake.
“Wawakilishi
walitakiwa kujadili hoja au malalamiko yaliyotolewa na wenzao
ikiwezekana waunde tume ya kufuatilia na kuchunguza ili kubaini ukweli
wa mambo, badala yake wamejadili kuondoka kwao badala ya chanzo cha wao
kususia kikao hicho ndani ya Baraza la Wawakilishi,” alisema mwanasheria
huyo.
Hata hivyo, alisema wakati bado unaruhusu kwa
viongozi wa vyama vyote vya CCM na CUF kukaa pamoja na kujadili kasoro
zinazojitokeza ili kuivusha Zanzibar salama.
No comments:
Post a Comment