Hatimaye
kile kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kinachowahusisha pia marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin
Mkapa, kinatarajiwa kufanyika wakati wowote wiki hii kujadili mwenendo
wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.
Taarifa
kutoka chanzo kimoja ndani ya CCM kimeeleza kuwa Mwinyi, Mkapa na wazee
wengine wanaounda Baraza la Wazee la Ushauri, watapasua kichwa wiki hii
kujadili mwenendo wa urais ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia Julai
2, mwaka huu, inayoonyeshwa katika ratiba ya uchaguzi ya CCM kuwa ndiyo
siku ya mwisho ya kurejesha fomu kwa wanaowania urais.
Lengo
la kikao cha Wazee ni kujadili kwa kina mwenendo wa mchakato wa kumpata
mgombea urais na mwishowe kutoa mapendekezo yao juu ya namna bora ya
kumpata mgombea kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC)
"Kikao
hiki ni muhimu kwa hatma ya mchakato wa uchaguzi... baada ya
kutofanyika wiki iliyopita, sasa kitafanyika wiki hii, tena wakati
wowote kuanzia kesho (leo)," chanzo kilieleza.
Awali,
kikao hicho kilitarajiwa kufanyika Jumatano iliyopita jijini Dar es
Salaam lakini kikaahirishwa na Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee,
Pius Msekwa, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni baadhi ya viongozi
wakuu wa CCM kuwa safarini.
Alipoulizwa
jana iwapo watakutana kaunzia leo, Msekwa hakuwa tayari kueleza
kiundani na badala yake alimjibu mwandishi kwa kifupi: "Just pay
attention (wee jiweke tayari tu) kama umesikia juu ya kikao chetu."
Kikao
cha Baraza la Ushauri la Wazee ni mahususi kwa ajili ya ushauri juu ya
watia nia 42 wa urais waliojitokeza kutaka kuteuliwa na CCM kupeperusha
bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani
utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wanaounda baraza la wazee
Wanaounda
Baraza la Ushauri la Wazee kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM
mwaka 2012 katika katiba yake ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti),
Mkapa (Mjumbe), Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour
(Mjumbe).
Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
Mkutano huo wa Baraza la Wazee CCM ni utangulizi wa mfululizo wa vikao vingine vya chama hicho vitakavyoanza Julai 5, mwaka huu.
Vikao
vingine ambavyo viko katika maandalizi ya kukutana ni Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya Taifa itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC)
itakayokutana Julai 8, chini ya Rais Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha
NEC Julai 9, mwaka huu.
Jina
la mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu
wa mwaka huu litajulikana Julai 12 baada ya kupigiwa kura na Mkutano
Mkuu wa Taifa wa CCM, ambao ni maalum kwa ajili kuchagua jina la mgombea
mmoja kati ya watatu.
No comments:
Post a Comment