Daesh wamiminia risasi waandamanaji nchini Libya - LEKULE

Breaking

13 Jun 2015

Daesh wamiminia risasi waandamanaji nchini Libya

Watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulizi la ufyatuaji risasi ovyo dhidi ya waandamanaji lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, mjini Derna Libya, wakati watu hao walipokuwa wakiandamana kupinga jinai za kundi hilo. Duru za habari nchini humo zimearifu kwamba, kwa uchache watu 10 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa, wakati wanachama wa kundi hilo la kitakfiri walipowafyatulia risasi waandamanaji hao. Maandamano hayo yaliyofanyika baada ya sala ya Ijumaa, yaliitishwa kulaani vitendo vya ukatili vinavyokinzana na mafundisho ya dini ya Kiislamu vinavyofanywa na magaidi hao wanaotenda jinai kwa jina la Uislamu. Ni vyema ifahamike kuwa, mji wa Derna na Sirte inadhibitiwa na wanachama wa kundi hilo la Daesh. Tangu serikali mbili nchini Libya zilipoingia katika mvutano baina yao, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na makundi mengine ya wabeba silaha yalitumia mwanya huo kuweza kujiimarisha nchini humo ikiwemo kudhibiti maeneo nyeti ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Shambulizi hilo la jana linatazamiwa kuibua hasira kali za Walibya katika maeneo mengine ya nchi hiyo dhidi ya kundi hilo.

No comments: