Busungu asaini Yanga - LEKULE

Breaking

1 Jun 2015

Busungu asaini Yanga


Malimi Busungu akisaini mkataba na timu ya Yanga.

YANGA haitaki masihara hata kidogo linapokuja suala la kukiongezea nguvu kikosi chake! Licha ya vijana hao wa Jangwani kuongoza kwa kufunga mabao 52 katika michezo 26 ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, imeamua kumuongeza mchana nyavu mwingine, anaitwa Malimi Busungu ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Mgambo JKT.

Yanga imeizidi nguvu Simba kwa kumnasa straika huyo ambaye pia Wanamsimbazi walikuwa wakimwania.
Ingawa Busungu alifunga mabao tisa msimu uliopita akiwa na Mgambo, inaaminika Busungu atatisha zaidi mzimu ujao hasa kutokana na kutabiriwa kuunda kombinesheni hatari inayomjumuisha Simon Msuva, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima.

Yanga ilikamilisha dili hilo baada ya kumpatia nyota huyo ambaye ilianza kumsaka tangu msumu wa 2013/14, kitita cha Sh milioni 25.Hali hiyo iliwaumiza vichwa sana viongozi wa Simba ambao walikuwa tayari wameshamtengea Sh milioni 30 za usajili, mshahara wa milioni 2 kwa mwezi, gari pamoja na nyumba ya kuishi ambayo thamaini yake kwa mwezi ni Sh, 400,000, lakini akaichomolea ofa hiyo akitaka apewe sh milioni 40.

Meneja wa Busungu ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, Simba wenyewe ndiyo waliojichanganya baada ya awali kuonyesha kutokuwa na nia na mchezaji huyo.“Baada ya kuona hivyo, tukaamua kuachana nao, kwani tungeendelea kuwasikiliza, mwisho wa siku angejikuta anakosa kila kitu, hivyo tunaomba wasimlaumu juu ya hilo,” alisema meneja huyo.

Katika hatua nyingine, inadaiwa kuwa Yanga itakuwa ikimlipa mchezaji huyo mshahara wa Sh milioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi chote cha miaka miwili atakachokuwa akiitumikia klabu hiyo kwenye michuano ya ligi kuu na ile ya kimataifa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimedai kuwa, pia mchezaji huyo atakuwa akilipwa Sh 250,000 kila mwezi kwa ajili ya kodi ya nyumba atakayokuwa akiishi.“Kuhusu gari ambalo tulikubaliana naye katika mazungumzo yetu hapo awali kabla ya kumsajili kuwa tutampatia, ahadi hiyo tumeshindwa kuitekeleza kutokana na bajeti yetu kutubana.

“Lakini kuna mwanachama wetu amejitolea kumpatia gari aina ya Toyota IST na kesho (leo) watakwenda kwa mwanasheria kukabidhiana,” kilisema chanzo hicho cha habari.Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Busungu alisema ana mapenzi makubwa na Yanga, ndiyo maana aligoma kusaini Simba, badala yake akaamua kutimkia Jangwani.

“Nimeamua kusaini mkataba wa kuichezea Yanga kutokana na mapenzi yangu tu niliyonayo kwa muda mrefu juu ya kutamani siku moja kuja kuichezea klabu hii ya Jangwani.“Kabla ya kusaini hapa, nilikuwa na ofa nyingi, ikiwemo ya Simba ambao walikuwa tayari wameshaniwekea hadi mkataba wa kujiunga nao,” alisema Busungu.

Busungu alikuwa akizitesa klabu za Simba na Yanga kila zilipokabiliana naye na anakumbukwa kwa kufunga bao la pili wakati Mgambo ilipoichapa Simba mabao 2-0 Machi 18 na kuifutia rasmi matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

No comments: