Bajeti ya Uchaguzi yaongezeka kwa asilimia 16 - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

Bajeti ya Uchaguzi yaongezeka kwa asilimia 16

Dodoma/Dar.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya leo atawasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 ambayo wachambuzi wameielezea kuwa itakuwa na unafuu kwa wananchi kutokana na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Wakati wachambuzi wakiielezea kuwa ni bajeti ya uchaguzi, wabunge waliozungumza na Mwananchi jana walisema hawatarajii kitu kipya kwa kuwa kila mara wamekuwa wakiipitisha kwa makofi, lakini utekelezaji unakuwa mdogo na sababu zimekuwa ni ukosefu wa fedha.
Bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, ongezeko la asilimia 16 kulinganisha na bajeti ya mwaka 2014/15 ya Sh19.6 trilioni, inatarajiwa kuboreshwa kwenye maeneo kadhaa baada ya wabunge kuchachamaa wakati wa uwasilishaji wa bajeti za wizara mbalimbali.

Wabunge waligeuka mbogo wakati wa upitishaji wa bajeti za wizara hasa kutokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo kwa angalau asilimia 50 ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti inayomalizika, na wakati mwingine ilibidi Waziri Mkuya asimame kutoa ahadi kuwa masuala hayo yangepelekwa kwenye Kamati ya Bajeti kuboreshwa.

Hii ni mara ya pili kwa Waziri Mkuya kuwasilisha bajeti baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka jana alipowasilisha ya mwaka unaomalizika Juni 30.
Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/16 unaoanza Julai Mosi, Mkuya alisema Serikali imepania kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani na wafadhili kutoka asilimia 14.8 hadi asilimia 8.4 na kwamba itajikita zaidi katika kukusanya kodi kwa kuhimiza matumizi ya vifaa vya kielektroniki.

Wachambuzi walihojiwa na Mwananchi jana walielezea bajeti hiyo kuwa italenga zaidi kutoa matumaini kwa wananchi, lakini itakuwa vigumu kutekelezeka.
“Kwa mfano, kupunguza utegemezi kwa wahisani ni tumaini zuri, lakini shaka ni malimbikizo ya madeni kwa makandarasi, walimu na taasisi nyingine zinazojiendesha. Tatizo jingine ni bajeti kidogo iliyotengwa kwa maendeleo,” alisema Profesa Humphrey Moshi kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema bajeti hiyo haina matumaini kwa watumishi wa umma hususani walimu nchini kutokana na mambo mengi kutoonekana.
“Niliangalia kwa umakini bajeti ya elimu na kuichambua, lakini mambo mengi ya msingi hayajaonekana. Mfano fungu la kulipa madeni ya walimu wastani wa Sh20 bilioni halipo, bajeti ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu hakuna.”

Mbali na kupunguza utegemezi kwa nchi wahisani na wafadhili, Serikali pia ilitangaza nafuu kubwa katika ada na kodi mbalimbali za ardhi, baada ya kuzishusha kwa wastani wa asilimia 50, jambo linaloonekana kuwa la kuwapa matumaini wananchi wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Katika taarifa ya mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/16 unaoanza Julai Mosi, Mkuya alitangaza vipaumbele vyake, ikiwamo kugharamia uchaguzi mkuu, kukamilisha miradi inayoendelea, kuweka msukumo maalumu kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu.

Waziri Mkuya alisema Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala kwa lengo la kuongeza mapato kwa kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato.

Waziri wa Fedha alisisitiza matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa kodi ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na kudhibiti wa mapato.
Alisema anakusudia kuhakikisha kuwa taasisi, wakala, mamlaka zinazojitegemea na mashirika ya umma yanakusanya ipasavyo mapato yasiyo ya kodi ili kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu.
Pia atapitia upya baadhi ya viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali ili viendane na hali halisi ya utoaji wa huduma husika.

Mkuya alisema sura ya bajeti inaonyesha kuwa Sh22,480.4 bilioni zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika mwaka ujao wa fedha.
Jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh14,824.4 bilioni, sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote.

Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh1,888.2 bilioni sawa na asilimia 8.4 ya bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ambazo sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.

Baadhi ya mikakati ya Serikali katika mwaka huo wa fedha ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.7 ya Pato la Taifa pamoja na kuongeza mapato yatokanayo na kodi kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa.

Changamoto za 2014

Waziri Mkuya alizitaja changamoto za bajeti ya mwaka 2014/2015  kuwa ni kutokufikia malengo ya kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi; Wafanyabiashara kugomea matumizi ya mashine za kielektroniki za ulipaji kodi (EFD’s) na mapato ya ndani na nje kutokupatikana kama ilivyokadiriwa.
Bajeti pia iliathiriwa na sera kulazimika kutoa fedha kwa mashirika ya umma ya biashara kama vile ATCL, TRL na Tazara, mahitaji makubwa ya kuboresha miundombinu ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara ili kukuza uchumi na kuongeza ajira na mchakato mrefu wa kupata mikopo ya kibiashara.

Mkuya alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali itaboresha na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato, kuendelea kusisitiza matumizi kulipa kodi na tozo kwa kutumia EFD’s, kuhakikisha hakuna kuingia mikataba mipya ya miradi na huduma bila kuwa na uthibitisho wa kuwapo fedha; kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.

Wasiwasi wa wabunge

Wakizungumza katika mahojiano na Mwananchi jana, baadhi ya wabunge walionyesha wasiwasi kuhusu utekelezaji wa bajeti tajwa kwa kuwa tatizo lililopo ni upatikanaji wa fedha.
Walisema wanaandaa bajeti nzuri, iliyokamilika, lakini utekelezaji wake unakuwa wa nadharia, haitekelezeki na ikitekelezeka inakuwa asilimia 30.

Ezekiel Maige, Msalala (CCM), alisema kuwa ukisiaji wa mapato na nidhamu ndogo ya matumizi ndio tatizo kubwa. “Tunakadiria mapato na matumizi wakati hatuna fedha na matokeo yake fedha hazipatikani tunashindwa kufikia malengo.

“Vilevile, hata fedha zinazopatikana, nidhamu ya matumizi haipo, watu ‘wanapiga hela’ ukiangalia ripoti ya CAG unaweza kulia, uanzishwaji wa miradi isiyokuwa ya mipango na kutumia fedha kama; vitambulisho vya taifa, uandikishaji wa BVR, wanatumia mabilioni ya shilingi wakati hazikuwa katika mafungu. Kashfa zimejaa za ubadhirifu lakini iliyoonekana tu ni ya Richmond,” alisema Maige.

Mariam Msabaha (viti maalumu, Chadema) alisema, “Hapa ni yaleyale ya kila mwaka, tunajaribu kupitisha bajeti kwa kupiga makofi, lakini hakuna kinachofanyika na ukiuliza unaambiwa fedha hakuna na kama zipo utekelezaji wake ni chini ya asilimia 30.

Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleyman Khalifa alisema bajeti kuongezeka ni ishara njema kuwa sasa fedha zitapatikana zaidi na zitaelekezwa katika maeneo muhimu ya afya, elimu na kilimo.
“Tatizo hapa ni fedha, sasa Serikali ikitaka heshima, kile ambacho Bunge linapanga, fedha zipelekwe kama inavyohitajika na inavyokusudiwa,” alisema.

Kwa upande wake, Augustino Mrema (Vunjo-TLP), alisema imekuwa ni kawaida kuimba masuala ya bajeti lakini hakuna utekelezaji wa miradi.

“Hakuna cha kusema kuwa bajeti itakuwa na kipya kwa kuwa kila mwaka tunapanga bajeti lakini fedha haziendi kwenye miradi na zaidi ya hapo ni chini ya makadirio,” alisema Mrema.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema: “Hakuna kipya kama tunategemea fedha za wahisani, huwezi kuweka mipango kwa fedha ambayo hujui utaipataje na utaipata lini.”

Mbunge mwingine, Zarina Madabida (viti maalumu- CCM), alisema: “Tatizo Serikali inaangalia fedha za wahisani ambazo hazina uhakika. Kinachotakiwa ni Serikali kuongeza nguvu katika makusanyo yake ya vyanzo ambayo ndiyo vya uhakika zaidi.

“Ni muhimu Serikali kusimamia mapato yake yatokanayo na kodi, wanaokwepa kodi wabanwe, na idhibiti ukusanyaji,” alisema.

Salum Barwani (Lindi Mjini-CUF) alisema, “Kipindi chote cha bajeti ni funika kombe mwanaharamu apite. Bajeti ni tendo la kisheria, inatakiwa Bunge liambiwe mwaka jana kilifanyika nini na mwaka huu kuna nini. Mwaka jana tatizo lilikuwa nini na mwaka huu tufanye nini tusirudie njia ileile, kimsingi, hatutarajii mapya,” alisema.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisema,“Siamini kama kutakuwa na mabadiliko chanya. Kila mwaka tunatengeneza bajeti nzuri, tunaipigia makofi tukiamini sasa miradi inatekelezwa, lakini hakuna kinachofanyika.

“Sitarajii mabadiliko na ukiuliza unaambiwa tatizo ni upatikanaji wa fedha, ninadhani kitakachofanyika ni kucheza na tarakimu tu.”

William Ngeleja (Sengerema-CCM) alisema: “Matarajio si mapya, tunaamini mambo yatakuwa mazuri ikiwa Serikali itasikiliza ushauri wa Bunge.”

Katika hatua nyingine, wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wameitaka Serikali kuepuka utamaduni wa kutapanya fedha katika mgawanyo wa bajeti badala yake iwekeze fedha nyingi katika sekta chache na nyeti.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini Tanzania (CTI), Felix Mosha alitaja mambo manne yanayotakiwa kupewa kipaumbele ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Mambo hayo ni kilimo, reli, elimu na viwanda ambayo yanapaswa kutengewa angalau asilimia 50 ya bajeti yote ili kupunguza changamoto zilizopo katika maeneo hayo.

“Tumekuwa na sera ya kilimo kwanza lakini Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwapo changamoto katika utekelezaji wake, tulishindwa hata kufikia makubaliano ya mkataba wa Maputo, uliozitaka nchi za Afrika angalau kutenga asilimia 10 ya bajeti yake wakati tunatambua kilimo ndiyo muhimili wa uchumi wa Taifa,” alisema.

“Ukiangalia elimu, viwanda na njia za reli ni maeneo nyeti, lakini hakuna dhamira ya uwekezaji wa kutosha. Ningetamani kuona angalau asilimia 50 ikitengwa kwa ajili ya maeneo hayo tu kuliko kugawa kidogo kidogo, hatuwezi kufika.”

No comments: