Zanzibar. Siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuandikisha wapigakura wasio na sifa, tume hiyo
imeibuka na kukanusha vikali.
Mkurugenzi wa ZEC, Salum
Kassim Ali alisema jana kuwa hakuna majina ya marehemu yanayoendelea
kutumika katika Daftari la Kudumu la Wapigakura hivyo CUF iache
kuipotosha jamii.
Alikuwa anajibu madai ya Maalim Seif
kuwa ZEC iliandikisha na kuruhusu wapigakura wenye umri chini ya miaka
18, walioandikishwa mara mbili, wasiokuwa wakazi na waliotumia ama
majina au picha za watu wengine.
Seif ambaye pia ni
Katibu Mkuu wa CUF, alisema madai hayo yamebainika katika utafiti
uliofanywa na chama hicho ili kubaini hujuma zilizofanywa na SMZ na
taasisi zake ambazo zinaweza kufanyika pia katika uchaguzi ujao.
Katika
majibu yake, Ali alisema sheria na taratibu za uchaguzi kabla ya kupiga
kura, yaani daftari huhakikiwa na majina kubandikwa hadharani katika
vituo vya kupigia kura zilifanyika, hivyo kama kungekuwa na dosari,
zilipaswa kuwekewa pingamizi.
Alisema sekretarieti ya
ZEC inafanya kazi zake kwa maelekezo ya makamishna wake wakiwamo wawili
kutoka CUF ambao wanafanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa na hayakuwahi
kujitokeza malalamiko hayo.
Alisema kabla ya kuanza
uandikishaji mwezi huu, ZEC ilikutana na wadau vyama vya siasa na
kuwaeleza mambo manne yatakayofanyika ambayo ni uandikishwaji wa mwisho
kwa wapiga kura, kuhakiki daftari la wapigakura, ikiwamo kuondoa
waliokufa, kubadilisha taarifa na kuhamisha taarifa za wapigakura.
Alisema
endapo kungekuwa na kasoro, makamishna hao wa CUF ndiyo wangekuwa wa
mwanzo kulalamika kwa vile wapo jikoni na siyo viongozi wa chama
wanaolalamika kwenye vyombo vya habari.
“Kama kweli ana
ushahidi wa kile anachokizungumza, kwa nini haleti malalamiko yake ZEC
badala yake analalamika kwenye vyombo vya habari?” alihoji.
Mkurugenzi
wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma
Ame alisema viongozi wenye dhamana wanapaswa kufanya utafiti na kupata
ukweli kabla ya kutoa shutuma nzito ili wananchi wapate taarifa sahihi.
Alisema
kwa mujibu wa Sheria ya Mzanzibari Mkaazi, mtu yeyote kabla ya
kusajiliwa, anatakiwa awe na cheti cha kuzaliwa, barua ya sheha na
haiwezekani mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 kupewa kitambulisho
hicho.
Alisema kabla ya kuandikishwa kuwa mpiga kura,
lazima mtu awe na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na masharti ya
kukipata lazima awe na cheti cha kuzaliwa na sheha amtambue.
Mkurugenzi
huyo alikanusha madai ya kuwepo kwa kambi ya jeshi inayotumika
kuandikisha na kuwapatia watu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi bila
sifa, akisema idara yake haina uhusiano wowote na kikosi wala jeshi
lolote hapa nchini.
Alisema Maalim Seif ni Makamu wa
Kwanza wa Rais, hivyo ana uwezo wa kumwita ofisini kwake wakati wowote
kumwelezea madai yake, lakini hajawahi kufanya hivyo isipokuwa mara moja
baada ya mtoto wake wa kumlea kukwama kupata barua ya sheha ya
kumwezesha kupata kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.
Alisema
utafiti wa CUF una kasoro kubwa kwa vile mamlaka inazozishutumu
hazikupewa nafasi ya kujieleza dhidi ya malalamiko hayo, jambo ambalo ni
kinyume na taratibu za utafiti.
Kuhusu madai kuwa
baadhi ya wafuasi wa CUF hawapatiwi vitambulisho vya ukaazi, alisema
kuna zaidi ya vitambulisho 20,000 ambavyo havijachukuliwa na wahusika,
wengi wao kutoka Pemba.
Kuhusu Shein
Akizungumzia
madai kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatakiwa kuanza
kujitayarisha kisaikolojia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema Maalim Seif
hana ubavu wa kuiangusha CCM visiwani hapa.
Alisema kama alishindwa akiwa kijana hawezi kufikia malengo hayo akiwa mzee.
Vuai
alisema Dk Shein ana kila sababu za kushinda kutokana na kutekeleza
vyema ilani ya uchaguzi, kulinda misingi ya amani na umoja wa kitaifa na
ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeendelea kuwapo na kuhudumia
wananchi wake.
Vuai alisema endapo Maalim Seif
haridhishwi na utendaji wa ZEC alitakiwa kuzungumza ndani ya Baraza la
Mapinduzi na si kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo linazorotesha
malengo ya maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
No comments:
Post a Comment