Wabunge wamkaanga Magufuli - LEKULE

Breaking

28 May 2015

Wabunge wamkaanga Magufuli

Dar/Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli amekuwa hapati wakati mgumu anapowasilisha bajeti ya wizara hiyo, lakini hali ilikuwa tofauti jana wakati wabunge walipoungana kueleza hofu yao katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara kutokana na madeni ya makandarasi.
Wabunge hao walidiriki kueleza kuwa kuna ufisadi katika ununuzi wa kivuko cha Bagamoyo na wengine kueleza kuwa miradi iliyotajwa kwenye hotuba ya bajeti ilishatekelezwa miaka ya 80 na 90.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Miundombinu kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti, Profesa Juma Kapuya, deni linalodaiwa na makandarasi ni kati ya Sh850 bilioni na Sh900 bilioni.
“Kamati haijaridhishwa kabisa na hali hii kwani deni hili sasa ni kubwa kuzidi hata bajeti inayotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hii, jambo ambalo linafanya bajeti hii kuonekana ni kiini macho tu,” alisema Profesa Kapuya.
Kambi ya Upinzani
Katika taarifa yake, Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) ilimshutumu Waziri Magufuli kwa kuandika hotuba ndefu ili kuwachanganya wabunge, huku hotuba hizo zikitaja hata miradi ya barabara zilizojengwa miaka ya 80 na 90.
Akiwasilisha maoni ya hiyo, msemaji wa KUB - Wizara ya Ujenzi, Felix Mkosamali alisema Serikali ya Awamu ya Nne inajigamba kwa kujenga kilomita 13,000 za barabara, lakini kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na kilomita 86,000 zinazotakiwa kujengwa.
Alisema KUB inaelewa vizuri mtandao wa barabara nchini na sehemu kubwa ya barabara hizo zilikuwa zimeshajengwa wakati wa Rais Benjamin Mkapa na sehemu ndogo tu zilikuwa zimebaki kuunganishwa.
“Kuna mtandao wa barabara wa Dar - Kagera, Dar - Kigoma, Dar - Songea, Dar – Tunduma na Dar - Masasi zilikuwa na lami wakati Serikali ya Mkapa inamaliza muda wake, nyingine zilikuwa zimebakiza vipande vichache vya kuunganishwa,” alisisitiza Mkosamali.
Alitoa mfano barabara ya Dar es Salaam – Chalinze yenye urefu wa kilomita 100, kuwa imetengewa Sh2.45 bilioni ambazo hatoshi kwa lolote.
Pia alihoji barabara ya Uyovu – Bwanga – Biharamulo, kilomita 112 ambayo imetengewa Sh4.97 bilioni bila ufafanuzi wa jinsi fedha hizo zitakavyotumika.
“Tutamwelewa Magufuli kama atatuambia ni shilingi ngapi zinajenga kilomita moja ya barabara kwa kiwango cha lami, kinyume cha hapo ni kupeana matumaini yasiyokuwepo,” alisema Mkosamali ambaye ni mbunge wa Muhambwe (NCCR - Mageuzi).
Kivuko Dar - Bagamoyo
Mkosamali alisema kivuko cha Dar es Salaam – Bagamoyo kilichonunuliwa kwa zaidi ya Sh8 bilioni ili kupunguza msongamano ni cha zamani na hakina uwezo.
Alilitaka Bunge kuunda tume kuchunguza ununuzi wa kivuko hicho kwa sababu ni kibovu na cha zamani na kilinunuliwa kwa gharama kubwa.
“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani au chakavu chenye spidi ndogo. Bakhresa ana meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na inabeba abiria 500 na kwa taarifa tulizonazo inauzwa kati ya Sh4 bilioni na Sh5 bilioni tu,” alisema.
“Mbwembwe na kelele za Magufuli kwamba watanunua meli kupunguza foleni zimegonga mwamba kwa kununua kivuko kibovu na cha kizamani kinachokosa abiria,” alisema.
Foleni Dar es Salaam
Mkosamali alisema Serikali haina dhamira ya kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam kwa sababu barabara za juu (flyovers) ambazo Dk Magufuli amekuwa akizisema, hazijajengwa licha ya kuwa wazo hilo lilitolewa katika hotuba yake ya bajeti ya 2011/12.
Alisema mpaka sasa, angalau ingekuwapo barabara moja ya juu na kueleza kushangazwa na taarifa ya Dk Magufuli kwamba mkataba kwa ajili ya ujenzi wa flyover ya Tazara utasainiwa Juni nchini Japan.
Suala hilo pia liliungwa mkono na Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu ambaye licha ya kukosoa bajeti kuwa haina lolote jipya, alisema wizara imeshindwa kujenga barabara za pembezoni mwa mji ambazo zingepunguza misongamano kwa kiasi kikubwa. Alisema suala hilo limekuwa likiwekwa kwenye bajeti katika miaka ya karibuni, lakini halitekelezwi na hali inazidi kuwa mbaya.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisema ili kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam, Serikali inatakiwa kuwekeza katika usafiri wa reli ili kupunguza magari yanayobeba makontena bandarini.
Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema Januari 13, 2009, alimwandikia barua Waziri Mkuu kumshauri asitishe ujenzi wa maghorofa katikati ya jiji, na kusisitiza kuwa ujenzi wa majengo makubwa yasiyopangiliwa limekuwa chanzo cha foleni.
“Kila siku Taifa linapoteza Sh4 bilioni kutokana na msongamano wa magari. Hizo ni fedha nyingi ambazo zingeweza kutufikisha mbali. Eti fedha za barabara wanapeleka kwenye BVR, tangu lini fedha za barabara zikapelekwa kwenye BVR,” alihoji mbunge huyo.
Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema wizara hiyo ndiyo pekee yenye deni kubwa na makandarasi wanashindwa kuendelea na kazi. Aliitaka serikali kulipa madeni hayo ambayo ni zaidi ya Sh850 bilioni.
Majibu ya Magufuli
Akijibu baadhi ya hoja za Wabunge, Dk Magufuli alisema suala la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam ni mtambuka na haliwezi kumalizwa na wizara yake pekee ambayo alisema imetimiza wajibu wake kadri ilivyoweza kulingana na rasilimali ilizonazo. Dk Magufuli alizitaka halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali wa maendeleo kuongeza nguvu ili kumaliza tatizo hilo.
“Nimeeleza mipango mingi tuliyonayo, flyover za Tazara na Selander, interchange ya Ubungo na barabara nyingine za mzunguko. Tuna Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), yote hii ikikamilika itapunguza foleni,” alisema.
Kuhusu kivuko cha Mv Dar es Salaam kuwa na kasi ndogo, waziri huyo alisema kinapojaribiwa huenda kwa kasi ndogo. Kikianza kufanya kazi rasmi kitakwenda kwa kasi ile ambayo ilikusudiwa. Alisisitiza kuwa safari ya kivuko hicho kwenda Bagamoyo ilikuwa ni majaribio yake kama ilivyofanyika kwenye treni. Aliwataka Wabunge kuwa wavumilivu na kuwahakikishia kuwa ni cha kisasa.
Kuhusu makandarasi, alisema mwezi uliopita, walilipwa Sh4 bilioni.
“Mimi ninawashangaa wanaosema hamna tulichofanya. Wakati tunapata uhuru tulikuwa na barabara zenye kilomita 1,300 tu. Baada ya awamu kwanza zilifika kilomita 6,000. Leo nikisema tuna kilomita 13,000 za barabara za lami, hayo ni mafanikio makubwa,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Nne ilikuta vivuko 15, lakini sasa vipo 28.
“Kule Kigoma ambako Mkosamali analalamika, hali ilikuwa mbaya. Tumejenga barabara na Daraja la Malagalasi lenye urefu wa kilomita 2.72. Ipo mifano mingi huko,” alisema.

No comments: