Waandamana Togo kupinga matokeo ya uchaguzi - LEKULE

Breaking

17 May 2015

Waandamana Togo kupinga matokeo ya uchaguzi


Maelfu ya watu wameandamana kwenye mji mkuu wa Togo, Lome kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwezi uliopita ambao ulimpa rais Faure Gnassingbe fursa ya kuendeleza utawala wa familia Gnassingbe kutimiza miaka 50 uongozini .

Waangalizi walisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa huru na haki lakini upinzani unasema kuwa ulikumbwa na udanganyifu.

Rais Faure Gnassingbe alitangazwa kuwa alipata asilimia 59% ya kura huku kiongozi wa upinzani Jean-Pierre Fabre akipata asilimia 35% ya kura .

Kumekuwa na madai ya wizi wa kura tangu wakati huo.

Adele Wavisso, 32 ambaye ni mchuuzi mjini Lome alinukuliwa akisema ''Wale wanaoshikilia madaraka hapa nchini wanafahamu fika kuwa sisi wananchi wa Togo hatukumpigia kura Faure .

''Sisi tunamtambua rais wetu ni fabre'',hatutalegeza kamba, wala hatutakubali''

Makundi ya upinzani yamekataa kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo Mahakamani wakidai kuwa mahakama inapendelea rais.

Babake Gnassingbe, Gnassingbe Eyadema aliongoza kwa karibu miaka 40 hadi alipoaga dunia mwaka 2005.

Utawala wa jeshi ulimteua mwanawe Faure kuwa rais na akashinda uchaguzi mwaka uliofuata licha ya madai ya wizi wa kura na maandamano makubwa yaliyosababisha vifo vya watu 500.

Wengine wengi walijeruhiwa katika maandamano hayo.

Gnassingbe alishinda tena uchaguzi uliofanywa mwaka wa 2010 ijapokuwa makundi huru ya wachunguzi walisema ulikuwa wa huru na haki.

No comments: