WAKATI Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akitarajiwa kesho kutangaza nia yake ya kugombea urais mjini Arusha katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira amepanga kutangaza safari yake ya kuelekea Ikulu Jumapili, jijini Mwanza.
Wassira mwenye Shahada ya Uzamili katika Uchumi ambaye pia ni Mbunge wa Bunda mkoani Mara, anakusudia kutangaza nia yake hiyo ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Taarifa za kuaminika zilizoifikia Mpekuzi kutoka kwa watu wa karibu na Waziri Wassira zinaeleza kuwa pia atatangaza siku ya kwenda kuchukuwa fomu ya kuwania nafasi hiyo kwenye Ofisi za Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma.
“Ni kweli tarehe 31 mwezi huu 2015 siku ya Jumapili, Waziri Steven Wassira atatangaza kusudio lake la kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu kupitia CCM. Nia yake hiyo ataitangazia Mwanza katika ukumbi wa BoT.
“Mzee (Wassira) anahitaji kuwatumikia Watanzania kwa dhamira njema ya kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo dhidi ya wananchi. Yapo mambo mengi atayaeleza siku hiyo pamoja na tarehe rasmi ya kuchukua fomu,” alisema mtoa habari huyo aliyepo karibu na Waziri Wassira.
Wassira alizaliwa mwaka 1945 Wilaya ya Bunda mkoani Mara, alisoma Shule ya Msingi ya Balili na Kisangwa Middle School, Wilaya hiyo ya Bunda, baadaye alijiunga na masomo yake ya Sekondari katika Shule ya British Tutorial College.
Alipata masomo ya ngazi ya juu Marekani katika Shahada tatu za Uchumi na Utawala, Shahada ya kwanza ya Uchumi na Uhusiano wa Kimataifa, Shahada ya Uzamili ya Uchumi na Shada ya Uzamili katika Utawala, zote kutoka Chuo Kikuu cha Amerika (American University) Jijini Washngton D.C.
Mbali na kuwa mbunge kuanzia mwaka 1970, Waziri Wassira amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu serikalini, ambapo alipata kuteuliwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mwaka 1975 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, nafasi aliyoitumikia hadi 1982 alipoteuliwa kuwa Waziri na Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington D.C Marekani.
Nyadhifa nyingine alizowahi kuzishika Wassira ni Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990, Waziri wa Maji, Waziri Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika nafasi aliyonayo sasa.
No comments:
Post a Comment