SNP yazoa viti 56 kati ya 59 Scotland - LEKULE

Breaking

8 May 2015

SNP yazoa viti 56 kati ya 59 Scotland

Chama ambacho kimewashangaza wengi katika uchaguzi mkuu wa Uingereza ni kile cha Scotland National Party The SNP.

Chama hicho ambacho kilichopata umaarufu haswa baada ya kura ya maoni ya kujitenga au kusalia katika muungano wa Uingereza kiliandikisha ushindi wa asilimia kubwa nchini Scotland.

SNP kimeshinda viti 56 kati ya viti 59.

Chama ambacho kilikuwa na ushawishi mkubwa nchini humo cha Labour kimesalia na mbunge mmoja tu Scotland.

Wimbi la SNP lilikuwa kubwa kiasi cha kumeza hata nyota na vigogo wa chama cha Labour Jim Murphy, Douglas Alexander na Margaret Curran miongoni mwa wengine wengi.

Chama cha The Liberal Democrats kilipoteza viti 9 huku mwakilishi wa Orkney and Shetland Alistair Carmichael akisalia mbunge wa pekee wa chama hicho huko.

Kwa upande wao chama kinachoongoza cha The Conservatives, kilihifadhi viti vya Dumfrieshshire na Clydesdale and Tweeddale.


Wadadisi wa maswala ya siasa nchini Scotland wamefananisha ushindi huo mkubwa na tufani iliyoanza baada ya hisia kali za kitaifa kuchochewa wakati wa kura hiyo ya maoni.

Aidha vigogo wa chama cha Lib Dems, Danny Alexander na Charles Kennedy pia hawakusazwa na wimbi hilo la SNP.

Makali ya chama cha SNP yalidhihirika katika eneo bunge la Kirkcaldy and Cowdenbeath, eneo lililokuwa likiwakilishwa na kiongozi wa kitaifa wa awali bwana Gordon Brown.

SNP ilitwa eneo bunge hilo kwa zaidi ya kura elfu kumi 10,000.
 Aidha chama hicho kilitwaa eneo wakilishi la Glasgow North East kwa zaidi ya asilimia 39.3%.

Ushindi huu mkubwa ni wa kwanza na mkubwa zaidi kwa chama hichi cha SNP.

Chama hicho kiliwahi kuandikisha ushindi wake mkubwa wa wabunge 11 katika uchaguzi wa mwaka wa 1974.

Katika uchaguzi wa mwaka wa 2010 chama hicho kilitwaa viti 6.

Kimsingi SNP kimetwaa viti vyote kutoka chama cha Labour huku kiongozi wa zamani wa chama hicho akirejea bungeni baada ya kutwaa kiti cha Gordon .

No comments: