Akizungumza na waandishi habari katika kikao cha pamoja
na rais mwenzake wa Iraq, Rais Dakta Hassan Rouhani wa Iran amesema
kuwa usalama wa Iraq ni usalama wa Iran na kusisitiza kuwa Iran iko
tayari kuipa nchi hiyo jirani kila msaada inaohitaji kwa ajili ya
kulinda uthabiti na usalama wake na vilevile kupambana na magaidi.
Katika kikao hicho, Rais Muhammad Fuad Masum wa Iraq ameishukuru
Jahmhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake mkubwa kwa nchi hiyo katika
mapambano yake dhidi ya magaidi wa Daesh na kuongeza kuwa tokea siku ya
kwanza Iran imekuwa ikishirikiana bega kwa began a serikali ya Baghdad
katika utumaji silaha kwa Iraq na pia misaada ya kibinadamu kwa ajili ya
kuwasaidia wakimbizi wa nchi hiyo. Fuad Masum, ambaye anazuru Iran kwa
mara ya kwanza tokea awe rais wa Iraq, aliwasili mjini Tehran Jumanne
usiku kwa mwaliko wa Rais Hassan Rouhani. Hata kama viongozi wa nchi
mbili hizi jirani wamekuwa wakitembeleana mara kwa mara lakini safari
hii ya rais wa Iraq inapewa umuhimu mkubwa katika mazingira nyeti ya
hivi sasa kieneo.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Iraq na Iran zimekuwa
zikishuhudia kuimarika kwa ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara.
Mbali na hayo mamilioni ya raia wa nchi mbili hizi jirani wamekuwa
wakizuru makaburi na maeneo matakatifu katika pande mbili na hivyo
kufanya ushirikiano wa idara na mashirika ya kiutalii ya nchi hizi kuwa
jambo la dharura. Hio ndio maana mawaziri wa biashara na utalii wa Iraq
wakaandamana na Rais Fuad katika safari yake mjini Tehran. Waziri
mwingine muhimu anayeandamana na Rais Fuad katika safari hiyo ni Waziri
wa Mazingira wa Iraq. Tatizo la tufani za vumbi na changarawe na
vilevile kuenea kwa jangwa ni moja ya changamoto muhimu ambazo katika
miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikiwasumbua wakaazi wa miji ya Iran
inayopakana na Iraq, tatizo ambalo utatuzi wake unahitajia ushirikiano
wa karibu wa maafisa wa mazingira wa nchi mbili.
Kuhusu suala la usalama, Iraq inakabiliwa na changamoto
kubwa ya hujuma ya magaidi wa Daesh ambao hivi karibuni wameteka mikoa
kadhaa muhimu ya nchi hiyo. Hatua za haraka zilizochukuliwa na viongozi
wa Iraq kwa lengo la kuisaidia serikali ya Baghdad kupambana na magaidi
hao ni suala muhimu ambalo limepelekea viongozi wengi wa Iraq akiwemo
Rais Fuad kukiri kwamba Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuisadia Iraq
kupambana na magaidi waliotajwa. Kwa msingi huo mapambano dhidi ya
ugaidi ni miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa na viongozi wa
Baghdad na Tehran katika mazungumzo yao ya hivi sasa. Katika upande wa
siasa, nchi mbili hizi kwa sasa zina misimamo inayofanana kuhusiana na
hujuma ya kichokozi ya Saudia Arabia nchini Yemen. Jamhuri ya Kiislamu
ya Iran inataka kuwepo kwa usitishaji vita halisi na kufikishiwa misaada
ya kibinadamu wananchi wa Yemen ambapo Rais Fuad naye amesema kuwa
mzozo wa nchi hiyo hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi. Suala jingine
linalojadiliwa na viongozi wa nchi hizi jirani ni kuhusiana na udharura
wa kulindwa umoja wa ardhi ya Iraq. Siku chache zilizopita kulitolewa
ripoti kuwa Congress ya Marekani ina mpango wa kuigawa Iraq katika
sehemu tatu za Makurdi, Masuni na Mashia. Baada ya kufanya mazungumzo na
rais mwenzake wa Iraq, Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa nchi hiyo
ni moja na iliyo na mshikamano kamili wa kitaifa. Rais Fuad yuko nchini
Iran kwa ziara ya siku tatu ambapo atakutana na kuzungumza na viongozi
tofauti wa Iran kuhusiana na masuala muhimu ya pande mbili, kieneo na
kimataifa.
No comments:
Post a Comment